Baadhi ya waumini wa Dini ya
Kiislamu wakisubiri ibada ya sala ya Maiti kwa ajili ya kumuombea Dua zee
Ibrahim Amaan kwenye Msikiti wa Ijumaa aliokuwa mioingoni mwa watu
waliouanzisha Kijijini kwake Nyamanzi.
Waumini wa Dini ya Kiislamu
wakiongozwa na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali walimsalia
Mzee Ibrahim kwenye msikiti wa Kijiji hicho. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/3/2016.
MWANAMAPINDUZI wa Zanzibar katika mapinduzi ya mwaka 1964 ambaye pia
ni muanzilishi wa Chama cha Mapinduzi Mzee Ibrahim Amaan aliyefariki Dunia jana
mchana amezikwa leo Kijijini kwake Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa
Mjini Magharibi.
Mzee Ibrahim aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya
baridi pamoja na Uzee alilazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja akipatiwa
matibabu kutokana na afya yake.
Mamia ya Wananchi, waumini wa dini pamoja na Viongozi wa Kitaifa walihudhuria
mazishi hayo yaliyojumuisha pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi, Rais Mstaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na Makamu wa
Rais Mstaafu wa SMT Dr. Mohammed Gharib
Bilal.
Mzee Ibrahim Amaan alizaliwa mwaka 1930 katika
Kijiji cha Nyamazi na alipofikia umri wa kusoma Wazazi wake wakampelekea kupata
elimu ya Quran iliyoambatana na ile ya Dunia katika ngazi ya Msingi.
Wakati wa ujana wake marehemu Mzee Ibrahim Amaan
alijishughulisha na kazi za ukulima na uvuvi ili kujipatia kipato
kilichomuezesha kuanza kujitegemea katika maisha yake ya kawaida.
Mwaka 1957 Mzee Ibrahim alijiunga na Chama cha Afro
Shirazy Party ambapo kutokana na
uzalendo pamoja na umakini wake alifanikiwa kuwa muanzilishi wa Umoja wa Vijana
wa ASP Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika Uhai wake marehemu Mzee Ibrahim aliwahi
kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Chama cha Afro Shirazy Party na
kushiriki kuuangusha Utawala wa kisultani Mwaka 1964 na baadaye kujiunga na
Jeshi la Ukombozi la Unguja akifikia cheo cha Kanal.
Akisoma Risala ya wakfu wa Marehemu Mzee Ibrahim
Makungu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Ikulu na Utawala Bora Dr. Miwinyihaji Makame alisema Chama cha
Mapinduzi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania zimepokea kwa masikitiko kifo cha Mwanamapinduzi huyo aliyejitolea
muda wake wa maisha kulitumikia Taifa hili.
Dr. Mwinyihaji alisema Ushujaa wa Mzee Ibrahim ulimpelekea
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein
kumtunukia Nishani ya Ushujaa wa Mapinduzi kwenye sherehe hizo za mwaka 2014.
Alisema Mzee Ibrahim miongoni mwa majukumu yake kwa Taifa aliwahi pia kuwa Mbunge wa Bunge la
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Katibu wa
CCM Idara ya Umma Afisi kuu ya CCM Kisiwandui pamoja na Mwenyekiti wa
kazi za njia na nnguvu za umeme.
Dr. Mwinyihaji alifafanua zaidi kwamba Mzee Ibrahim
alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wazee la Chama cha Mapinduzi wadhifa ambao
aliendelea nao hadi mauti yalipomfika.
Mzee Ibrahim
Amaan aliyezaliwa mwaka 1930 na kufikisha umri wa Miaka 86 ameacha
kizuka Mmoja na Watoto Thalathini.
Yarabi aiweke roho ya Marehemu Mzee Ibrahim Amaan
mahali pema Peponi amin.




No comments:
Post a Comment