Vikosi vya Ulinzi vikiwa katika hatua za mwisho za matayarisho ya upambaji uwanja wa Amaan wakitandika Zulia jekundu litakalopamba sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zanzibar. Mjumbe wa Kamati ya sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Kanal Shaaban Lissu akiwa makini kusimamia na kuhakikisha kazi hiyo inakwenda kwa mujibu ilivyopangwa.
Jukwaa maalum la kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein limeshakamilika matayarisho yake kwa ajili ya kazi hiyo.
Vikosi vya ulinzi na usalama vikimaliza matayarisho ya mwisho ya sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hapo uwanjwa wa Michezo Amaan Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi akikiongoza Kikao cha Kamati hiyo kwenye ukumbi wa Watu mashuhuri (VIP) uliopo Uwanja wa Amaan.
Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na
Maadhimisho ya Kitaifa wakitafakari na
kujaribu kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa matayarisho ya mwisho wa
sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dr. Ali Mohammed Shein. (Picha na – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/3/2016.
JAJI Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar Othman Makungu
anatarajiwa kumuapisha Rais Mteule wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein Alhamis ya Tarehe 24 mwezi huu baada ya
kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa marejeo uliofanyika Jumapili iliyopita.
Dr. Ali Mohammed Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alishinda
uchaguzi baada ya kupata kura Laki 299,982 sawa na asilimia 91.4% ya kura zote zilizopigwa kwenye
uchaguzi huo.
Matayarisho kwa ajili ya sherehe hizo za uapishwaji
zitakazofanyika katika uwanja wa michezo wa Amani Mjini Zanzibar yamekamilika rasmi ambapo Vikosi vya ulinza
na usalama vya SMT na SMZ vimeshajiandaa
kwa kuzipamba sherehe hizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya
Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akiwa pamoja na Makamanda wa Vikosi hivyo
na baadhi ya watendaji wakuu wa Serikali alipata wasaa wa kuangalia
mazoezi ya mwisho ya wapiganaji hao.
Sherehe hizo zitapambwa na Vikosi vya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM),
Mafunzo, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) , Valantia (KVZ) na Kikosi cha Zimamoto
na Uokozi (KZU).
Viongozi wa Dini tofauti watakaoambatana na Jaji
Mkuu wa Zanzibar katika sherehe hizo za
uapishwaji wanatarajiwa kutoa Dua kwa nia ya kumtakia Uongozi Mwema Rais
atakaeapishwa pamoja na Zanzibar kwa ujumla.
Baadaye Wajumbe wa Kamati ya sherehe za Maadhimisho
ya Kitaifa walipata fursa ya kukutana
ili kukamilisha changamoto zilizojitokeza kwenye matayarisho ya Sherehe hizo
hapo katika Ukumbi wa Watu Mashuhuri (VIP) ya uwanja wa Aman.
Asilimia kubwa ya Wajumbe hao wameonyesha kuridhika
kwao hatua iliyofikiwa ya maandalizi hayo wakitarajia mafanikio makubwa
ya sherehe hizo katika Historia za chaguzi za vyama vingi hapa Zanzibar.
Akizungumza na vyombo vya habari nje ya Uwanja wa
michezo wa Amani baada ya kukamilika
kwa maandalizi ya Sherehe hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho
ya Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi
aliwahimiza Wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye sherehe hizo.
Balozi Seif alisema utaratibu maalum umeandaliwa
kupitia kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya zote wa jinsi wananchi
watakavyoingia kwenye uwanja kushuhudia sherehe hizo.
Aliwaasa wananchi wote kuelewa kwamba uchaguzi
umekwisha na lililobakia kwa wakati huu
ni kuhakikisha kila mwananchi anaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa Taifa hata
kwenye kazi za amali ambazo kwa namna moja au nyengine zinasaidia uchumi wa
Nchi.
Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 Kifungu cha 31 (1)
inaelewa wazi kwamba Mtu anayechukuwa madaraka ya Urais, kabla ya kuanza
wadhifa huo,atakula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kazi kama kitakavyowekwa na
Baraza la Wawakilishi lakini kwa hali yoyote itabidi ashike madaraka hayo kabla
ya kupita siku saba baada ya kuchaguliwa.
No comments:
Post a Comment