Baadhi ya Eneo la Ekari Tisa za Mikarafuu lililounguzwa Moto na Watu
wasiojuilikana katika Shehia ya Mzambarauni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
*Sheria ya Maendeleo ya Karafuu itumike kuilinda sekta
hiyo
KARAFUU ni Zao la Kilimo
linalotegemewa sana na Wakulima wa zao
hilo na Wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo kwa kukodi mashamba na
vibarua wanaoajiriwa kuchuma kwa makubaliano ya kulipwa ujira kwa ajili ya
kuendesha maisha yao.
Pia zao la karafuu ni zao
kuu la Uchumi wa Zanzibar kutokana na kuingiza fedha nyingi za kigeni ambazo
hutumika katika kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, kusambaza umeme,
maji safi, miundombinu ya bara bara na huduma nyengine muhimu.
Takwimu zinaonesha kuwa zao la Karafuu ndilo linalochangia zaidi pato
la Taifa kuliko mazao mengine ya biashara, ambapo inakadiriwa kuchangia pato la
Taifa kwa wastani wa asilimia 20.5.
Kutokana na umuhimu wa zao
hili, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar kwa kushirikiana
na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) linaendesha mpango maalum wa kuongeza
idadi ya mikarafuu na kuongeza uzalishaji kwa kuotesha miche 1,000,000 kila
mwaka na kuwagaia Wakulima bila ya malipo.
Pamoja na jitihada hizo za
Serikali za kuimarisha zao la karafuu kwa maslahi ya Nchi na Wananchi wake
lakini tukio la hivi karibuni la watu wasiojuilikana kuchoma moto eka tisa za Mashamba
ya Mikarafuu linarudisha nyuma jitihada hizo.
Katika tukio hilo la
kusikitisha lililotokea Januari 22/2016 katika Shehia ya Mzambarauni Mtambwe,
Mkoa wa Kaskazini Pemba mikarafuu 151 imeungua moto ambapo kati ya hiyo 36
haiwezi kuota tena kutokana na athari hiyo ya moto.
Mikarafuu hiyo iliyoungua ni
kutoka katika mashamba matatu tofauti yaliyokuwepo katika sehemu moja ambapo
kwa pamoja yana ukubwa wa ekari tisa (9). Tukio hilo limesababisha hasara yenye
thamani inayokisiwa kufikia shilingi milioni 24.5.
Imeonyesha kuwa kitendo cha kuchoma moto
kwa mashamba hayo ni hujuma za makusudi kutokana na moto huo kutokea katika
maeneo tofauti. Kitendo hicho ni kibaya kwa sababu ni hujuma kwa uchumi wa nchi
na Wananchi wake.
Ni wazi kuwa kiitendo hicho kimewaumiza
sana Wakulima wa mashamba hayo kwa sababu Mkarafuu ni mti unaohitaji huduma kubwa katika
ukuaji wake, hata ukifikia hatua ya kuzaa Mkulima huwa kafanya kazi kubwa. Sasa
anapotokea mtu mwengine kufanya hujuma huyo ni maumivu makubwa kwa Mkulima.
Mkarafuu mmoja una uwezo wa kuzalisha
zaidi ya pishi ishirini kulingana na ukubwa wa mkarafuu wenyewe, kwa bei ya
sasa ni zaidi ya shilingi laki nne hivyo mikarafuu 151 iliyoungua moto imesababisha
hasara kubwa ya kiuchumi na kimazingira.
Kutokana na umuhimu na
thamani ya zao la karafuu kwa uchumi wa Nchi na Wananchi wake Serikali
ilipitisha Sheria ya Maendeleo ya Karafuu, Namba 2 ya mwaka 2014 ili kuulinda
Mkarafuu na karafuu zenyewe.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo ni
kosa kwa mtu yoyote kuchoma moto mikarafuu. Kifungu cha 13(1) (a), kinakataza kuchoma au
kutengeneza makaa, kuchimba
mawe, udongo au mchanga kuangusha,
kung’oa, kukata, kuharibu au kuathiri mikarafuu kwa aina yoyote ile.
Waliofanya
tukio hilo la uchomaji moto mashamba ya mikarafuu wajue kuwa wamefanya kosa kwa
mujibu wa Sheria ya Maendeleo ya karafuu. Ni vyema Jeshi la Polisi likafanya uchunguzi wa
kina kuwagundua waliofanya tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria.
Miongoni mwa madhumuni ya kuundwa kwa
Sheria hiyo ya Maendeleo ya Karafuu ya Mwaka 2014 ni kulinda na kuweka ulinzi
imara wa Mikarafuu na Karafuu zenyewe. Kuimarisha, kustawisha, kuthaminisha na
kuendeleza zao la karafuu Zanzibar, hivyo kuchoma moto mikarafuu ni kwenda
kinyume na Sheria hiyo.
Sheria hiyo pia inapiga marufuku kutumia mkarafuu kwa matumizi ya
aina yoyote, iwe kwa ujenzi wa nyumba, kuchonga mbao, kuchonga vinyago au mapambo
ya aina yoyote, hivyo Sheria hiyo inatoa ulinzi wa kutosha kwa sekta ya karafuu.
Linalotakiwa ni usimamizi wa utekelezaji wa Sheria hiyo.
Hujuma nyengine
inayokwaza jitihada za Maendeleo ya Sekta ya Karafuu ni kwa baadhi ya watu
kukata matawi na mikarafuu midogo kwa dhamira ya kuiba karafuu kutokana na
kuzoeleka kwa uuzaji na ununuzi wa karafuu kwa njia isiyokuwa rasmi ‘vikombe’.
Wakulima wengi
wamekuwa wakilalamika kukatiwa mikarafuu yao hasa wakati wa msimu wa uchumaji
jambo ambalo linachangiwa sana na kuwepo kwa baadhi ya watu wanaonunua karafuu
mbichi jambo ambalo ni kosa kwa vile Shirika la ZSTC ndio taasisi pekee iliyopewa
mamlaka ya kununua na kuuza karafuu.
Kwa mujubu wa
Sheria hiyo mtu atakaetiwa hatiani kwa kosa la kuuhujumu mkarafuu kwa aina
yoyote ni kulipa faini isiyopungua Shilingi Milioni tatu au kifungo
kisichopungua miaka mitatu (3) au vyote kwa pamoja kulingana na ukubwa wa kosa.
Shirika la ZSTC, taasisi ambayo ni
dhamana ya kuimarisha zao la karafuu kwa kushirikiana na wadau wengine limekuwa
likitoa elimu juu ya namna ya kuimarisha zao hilo na thamani yake kwa maendeleo
ya uchumi na ustawi wa jamii.
Mwezi
Disemba 2011, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein alitia saini Sheria mpya ya ZSTC Na. 11 ya mwaka 2011, inayoipa
Mamlaka na uwezo Shirika la ZSTC kulisimamia, kulihudumia, kuliimarisha
zao la karafuu na kuhakikisha linakuwa endelevu kwa maslahi ya wakulima,
wananchi na Taifa kwa ujumla, kuchoma moto mikarafuu kwa makusudi ni kurejesha
nyuma jitihada za uimarishaji wa zao hilo.
Kutokana na uchumi wa Zanzibar kutegemea sana zao la
karafuu, Sera ya Serikali juu
ya zao la hilo ni kumnufaisha Mkulima zaidi, hivyo Serikali inaendelea na azma
yake ya kutekeleza uamuzi wake wa kuwapatia Wakulima bei ya karafuu ya asilimia
80 ya bei ya kuuzia nje ya nchi ili kuwahamasisha Wakulima kuimarisha zaidi zao
hilo.
Zao
la karafuu ninawanufaisha wengi kutokana na kutoa ajira kwa Wananchi wengi na mzunguko
wa fedha unaotokana na biashara ya zao hilo unajenga ustawi wa Wananchi wengi na
kuongeza pato la Taifa, hivyo kuichoma kwa makusudi ni kuwakosesha kipato
Wananchi wengi.
Pia kuna athari za kimazingira ambapo
mikarafuu kama ilivyo miti mengine huwa ni chanzo kikubwa cha mvua. Unapochoma
moto mikarafuu unakaribisha jangwa katika eneo hilo na kuondoa uwezekano wa
kuwepo kwa mvua. Kitendo hicho husababisha kukosekana kwa mvua na kupelekea
ukame katika maeneo husika.
Moshi mwingi ambao hutolewa baada ya
uchomaji wa Mikarafuu huleta athari katika mfumo wa hewa. Pia uwepo wa mikarafuu
ni kinga kwa mmongonyoko wa ardhi ambapo katika maeneo ya mabonde ambapo
mikarafuu hupandwa husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia mmongonyoko wa ardhi.
Wito kwa Wakulima, Wafanyabiashara na
Wadau wote wa Zao la Karafuu na wananchi kwa jumla kutokufanya makosa kama hayo ya uchomaji wa
mashamba ya mikarafuu. Kuchoma moto mikarafuu ni kurudisha nyuma jitihada za
Serikali katika uimarishaji na uendelezaji wa zao hilo.
Ni vyema Wananchi wote wakasaidia katika
kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulinda mikarafuu yetu na ubora wake ili
kufanikisha azma ya Serikali ya kuifanya Sekta ya karafuu kuendela kuwa tegemeo
katika kukuza uchumi na kujenga ustawi wa Wananchi.



No comments:
Post a Comment