Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius Likwelile (katikati) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu Serikali ilivyojipanga kuboresha na kuhudumia sekta mbalimbali nchini ikiwemo elimu, umeme, maji na miundombinu. Kulia ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alfayo Kidata na kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu akisistiza wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu mapato na matumizi ya Serikali yalivyo boreshwa na uchumi wa nchi kuimarika na kutengemaa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius Likwelile leo jijini Dar es salaam kuhusu Serikali ilivyojipanga kuboresha na kuhudumia sekta mbalimbali nchini ikiwemo elimu, umeme, maji na miundombinu. (Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango)
SERIKALI imetoa
jumla ya Sh. Bilioni 318.406 kwa mwezi wa Januari mwaka 2016, kwa ajili ya
miradi ya maendeleo nchini na Sh. Bilioni 538.5 kwa mishahara ya watumishi wa
Umma.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Servacius Likwelile alisema kuwa
Serikali inajivunia kufanikiwa kutumia fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya
maendeleo ambapo hadi sasa Serikali imetumia kiasi cha Sh. Bilioni 71.2 tu
kutoka fedha za nje.
Dkt. Likwelile
alisema mapato yanayokusanywa nchini yamewezesha kutekeleza sera ya elimu bure
ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali
ilitoa kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili
ya ruzuku, ada na chakula kwa shule za bweni pamoja na mahitaji mengine ambapo
mwezi wa Januari 2016 Serikali imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa ajili ya kutekeleza
Sera hiyo.
Aliongeza kuwa
katika ulipaji wa madeni ya wakandarasi nchini , Serikali imetoa Sh. Bilioni 130
kwa mwezi Januari mwaka 2016 ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 ilitoa Sh. Bilioni
193.
Kwa upande wa Mfuko
wa Barabara, Katibu Likwelile alifafanua mradi huo umetengewa kiasi cha Sh.
Bilioni 47.89 na kuongeza kuwa Benki kuu ina fungu la mfuko huo ambapo nayo
imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 76.3.
Dkt. Likwelile alisema
kuwa Halmashauri zitapelekewa kiasi cha Sh. Bilioni 20.52 kwa ajili ya kuboresha
barabara na jumla mfuko huo kufikia kiasi cha Sh. Bilioni 274.71.
Akifafanua kuhusu
miradi ya umeme, Dkt. Likwelile alisema kuwa mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali
ililipa deni la TANESCO kiasi cha Sh. Bilioni 80 za mradi wa Kinyerezi II na
kwa mwezi Januari mwaka 2016 kiasi cha Sh. Bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya
mradi huo.
Hali hii imefikisha
kiasi cha Sh. Bilioni 120 kwa ajili ya kulipa madeni na kuendeleza uzalishaji
wa umeme nchini.
Alisema kiasi cha
Sh. Bilioni 21.959 kimetengwa kwa ajili ya mradi wa umeme vijijini na Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) ina mfuko wa mradi huo ambao kwa sasa una kiasi cha Sh. Bilioni
21.9 na kuongeza kuwa huduma ya umeme kwa wananchi itaimarika.
Alifafanua kuwa Serikali
imeanzisha mfuko wa maji Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo mpaka sasa mfuko huo
una jumla ya kiasi cha Sh. Bilioni 46.3.
Aidha, BoT imetoa Sh.
Bilioni 12.5 kuendeleza miradi ya maji ambapo kwa Januari mwaka 2016 Serikali
imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 7.7.
Serikali imetenga
kiasi cha Sh Bilioni 82.2 kwa mwezi wa Januari ili kuweza kulipa pensheni za
wastaafu, na kwa wale wastaafu walio katika daftari la kudumu ambapo
wametengewa kiasi cha Sh. Bilioni 33.3 kwa ajili ya malipo yao.
Wabunge wametengewa
kiasi cha Sh. Bilioni 35.5 kwa ajili ya mkopo wa magari ambapo kila mbunge
atapata kiasi cha Sh. Milioni 90, kiasi cha Sh. Milioni. 45 ni ruzuku na Sh.
Mil. 45 ni mkopo ambao utalipwa ndani ya miaka 5.
Aidha, Serikali
imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 784.3 kwa ajili ya kulipa deni la taifa.
Naye Kamishna wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alibainisha kuwa hali ya
makusanyo ya mapato nchini iko vizuri ambapo kwa mwezi Januari 2016, makadirio
yalikuwa Sh. Trilioni 1 na Bilioni 45 na hadi kufikia sasa kiasi cha Sh. Trilioni
1 na Bilioni 31 zimeshakusanywa.
Matarajio ya TRA ni
kukamilisha kukusanya kiasi cha Sh. Billioni 14 zilizosalia.
Aidha, Kidata alibainisha
kuwa uingizaji wa bidhaa kupitia bandarini bado uko vizuri licha ya minong’ono
kuwa uzuiaji wa mianya ya ukwepaji kodi imepunguza uingizaji bidhaa ambapo kwa
mwezi Januari Bilioni 111 zimekusanywa kutokana na ushuru wa forodha.
Kidata alitoa wito
kwa kila mtanzania kulipa kodi na kutoa taarifa za wakwepa kodi ili kuweza
kukuza mapato ya nchi.
Kwa upande wake Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu amepongeza juhudi za
ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.
Alisema kuwa uchumi
umekua na unazidi kuimarika licha ya changamoto za kiuchumi duniani ambapo
uchumi wa nchi umekua kwa asilimia 7 na unategemewa kukua miezi ijayo kutokana
na kuongezeka kwa uzalishaji nchini.
Mfumuko wa bei
unaendelea kubaki ndani ya kiwango cha tarakimu moja, licha ya ongezeko dogo
katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kupanda kwa bei za vyakula.
Alisema kuwa mfumuko
wa bei ulikuwa asilimi 6.8 mwaka 2015, ukilinganishwa na asilimia 6.1 kwa mwaka
wa fedha ulioishia Juni 2015.
Wakati huo huo
mfumuko wa bei usiojumuisha chakula na nishati uliendelea kubaki katika viwango
vya chini ya asilimia 2.5 kutokana na hatua mbalimbali za kisera
zilizochukuliwa na BoT.
Prof. Ndulu
alifafanua mapato ya fedha za kigeni yanaendelea vizuri ingawa bei ya dhahabu
imeshuka kutoka Bilioni 2.5 hadi Bilioni1.3.
Sekta ya utalii
imesaidia kuimarisha fedha za kigeni kwani mapato yameongezeka kutoka Bilioni 1.5
hadi Bilioni 2.2.
Sekta ya viwanda nayo
imeshika nafasi ya pili katika kuongeza fedha za kigeni nchini ambapo mwaka 2015 mapato yalikuwa Bilioni 1 na kwa sasa
yamefikia Bilioni1.5.
Aidha, Prof. Ndulu
aliongeza kuwa sekta ya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi imesaidia kuimarisha
fedha za kigeni ambapo mapato yamefikia Dola Bilioni11 kwa mwaka.
Hadi kufikia sasa
Tanzania imenufaika kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika uingizaji bidhaa
hiyo kwa asilimia 44.
Serikali inatarajia
kuendelea kuimarisha uchumi ili kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati
hadi ifikapo 2025.
Imetolewa
na Wizara ya Fedha na Mipango
Kitengo
cha Mawasiliano





No comments:
Post a Comment