Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Kamati ya Kitaifa ya Sherehe za Maulidi ya Kuzaliwa kwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad (SAW) aliyokutana nayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kushoto kwa Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh Sherali Shamsi akifuatiwa na Mjumbe wa Kamati Hiyo Bwana Moh’d Baloo. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
11/12/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kufuta mikataba yote ya makubaliano ya ukodishwaji wa Nyumba za Serikali zilizojengwa maalum kwa kuwasaidia Wananchi wa kipato cha Chini unayofanywa kijanja na baadhi ya watu pamoja na Kampuni binafsi kwa kukodisha watu wengine.
Alisema tabia hiyo iliyojengeka kwa muda mrefu sasa imekuwa ikitumiwa na wajanja hao wanaokodishwa Nyumba na Serikali na baadaye kubuni mikataba mipya ya kuwakodisha watu wengine kwa nia ya kupata faida kubwa zaidi (maarufu kilemba).
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kufuatilia Mikataba ya Wafanyabiashara waliokodishwa milango ya Maduka katika Jumba la Maendeleo Nambari Kumi Michenzani Mjini Zanzibar ambayo baadhi ya waliokodishwa milango hiyo na Serikali tayari wameshaikodisha kwa watu wengine.
Alisema tabia ya baadhi ya Watu hao kutumia mali za Serikali walizopewa kwa misingi ya kupata tahfifu ya kupunguza ukali wa maisha na kuwauzia au kuwakodisha watu wengine waelewe kwamba wanafanya dhulma na dhambi kubwa.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) kwa uamuzi iliyochukuwa ya kuwafutia mikataba wajeta wake wa mwanzo iliyowapa milango la Maduka na wakaamua kuikodisha tena kwa watu wengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba tabia kama hiyo imejengeka pia katika Nyumba zilizowekwa Wakfu na kuishauri Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar kufanya utafiti na kuwabaini wapangaji wake wenye tabia kama hiyo.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Zanzibar Nd. Moh’d Hafidh Rajab alisema Watendaji wa Shirika hilo wameanza ukaguzi Maalum wa kuzipitia Nyumba zote za Serikali zilizokodishwa kwa watu na Taasisi tofauti hapa Nchini.
Nd. Hafid alisema ukaguzi huo utatoa fursa kwa Uongozi wa Shirika hilo kufanya marekebisho ya kodi zilizofungwa katika mikataba ya zamani ili iende na wakati na soko liliopo hivi sasa.
Alisema Shirika la Nyumba la Zanzibar lililoasisiwa hivi karibuni baada ya kupata baraka za Baraza la Wawakilishi Zanzibar linahitajika lijitegemee lenyewe badala ya kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali Kuu.
Akitoa shukrani zake Mmoja wa wamiliki wa Maduka yaliyopo Michenzani ambae ni Meneja wa Kampuni ya A l – Salam na Seib Ruila Bwana Yussuf Juma Msanif aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika lake la Nyumba kwa uamuzi wake wa kukagua majengo yake mbali mbali.
Bwana Yussuf alisema uamuzi huo wa busara na hekima umewapa faraja wao binafsi na Kuliomba Shirika la Nyumba kufikiria upya kodi zake inazotoza kwa lengo la kuwapa tahfifu Wafanyabiashara wachanga ili waweze kuwa na uwezo mzuri wa kulipa kodi.
Mlango mmoja wa Duka hapo Michenzani ulikuwa ukikodishwa Mteja kutoka Serikalini kwa Shilingi Thamanini Elfu kwa Mwaka wakati mkodishwa huyo anaamuwa kukodisha tena kwa Mtu wa Pili wa Dola za Kimarekani mia 450 kwa mwaka sawa na Shilingi Laki Tisa na Thamanini (980,000) za Kitanzania.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Kamati ya Taifa ya Sherehe za Maulidi ya kuzaliwa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad (SAW).
Kamati hiyo aliyokutana nayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wake Sheikh Sherali Shamsi alimuelezea matayarisho yanayoendelea ya Maulidi hayo yanayofanyika Kitaifa kila mwaka hapa Nchini.
Sheikh Sheral alisema kikawaida Maulidi hayo yanayoadhimishwa Usiku wa Mwezi Kumi na Moja Mfunguo Sita hufanyika katika Viwanja maarufu vya Maisara alakini endapo itanyesha Mvua shughuli hiyo itahamia katika Ukumbi wa salama Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.
No comments:
Post a Comment