TANGAZO


Wednesday, December 16, 2015

Balozi Seif Iddi akutana na Ujumbe wa Kampuni ya Uwekezaji kutoka China katika Sekta ya Mafuta mjini Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Ujumbe wa Kampuni ya Uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar. 
Mkuu wa Taaluma ya Miamba kutoka Kampuni ya Uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China (CNOOC) Bwana  Cui Hanyun akimfahamisha Balozi Seif nia ya Kampuni yake ya kutaka kuwekeza miradi ya Kiuchumi Visiwani Zanzibar. 
Bwana  Cui Hanyun akisisitiza mazingira mazuri yaliyopo katika Visiwa vya Zanzibar yaliyoushawishi Uongozi wa Kampuni yake kutaka kuanzisha miradi ya Uwekezaji Zanzibar. 
Balozi Seif akiuhakikishia Ujumbe wa Kampuni ya Uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China kwamba SMZ itatoa ushirikiano utakaoiwezesha Kampuni hiyo kuanzisha miradi yake katika kipindi kifupi. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
16/12/2015.
KAMPUNI ya Uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China iko tayari kushirikiana na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza miradi ya pamoja kwenye sekta hizo endapo itapatiwa fursa katika mpango wa  uendelezaji wa miradi ya pamoja.

Mkuu wa Taaluma ya Miamba kutoka Kampuni  hiyo ya Kimataifa ya  CNOOC Bwana  Cui Hanyun akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Kampunin hiyo alisema hayo wakati wa mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Cui Hanyun na Ujumbe wake  ambao pia waliambatana na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Yun Liang alisema Kampuni hiyo yenye kutoa huduma katika Mataifa tofauti Ulimwenguni pia inajihusisha na uwekezaji katika Benki za Ufukweni (Off Show Banking).

Alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umeridhika na mazingira bora yaliyopo katika Visiwa vya Zanzibar na kushawishika  katika kutaka kuwekeza miradi yao ili kuunga mkono hatua za SMZ za kuwashawishi wawekezaji  wa ndani na nje ya Nchi kuanzisha miradi yao ya kiuchumi katika sekta tofauti Nchini.

Mtaalamu huyo wa Miamba wa CNOOC alimueleza Balozi Seif  kwamba Kampuni hiyo iko tayari kuweka nguvu zaidi katika sekta ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaonyesha msisitizo kwa mujibu wa mahitaji halisi ya Taifa na Wananchi walio wengi.

Bwana Cui Hanyun alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imeshatoa baraka na kuyaruhusu Makampuni ya Nchi hiyo kuanzisha miradi ya Benki za Ufukweni kwa vile  tayari imeshakuwa na wataalamu na uzoefu wa kutosha wa miaka mingi kwenye sekta hizo.

Naye Meneja wa Biashara wa Kampuni hiyo Ukanda wa Bara la Amerika Bwana Hu Gencheng alieleza kwamba Kampuni hiyo mbali ya uzalishaji pia  imekuwa ikipokea Gesi  kutoka Mataifa ya Indonesia, Qatar, na Autralia.  

Kwa upande wa Bara la Afrika  Bwana  Hu Gencheng  alisema CNOOC iko katika uendelezaji wa miradi ya Benki za Ufukweni  katika  Mataifa ya Nigeria, Equitorial Guinea, Congo Brazaville, Kenya na Uganda.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza ujumbe huo wa Kampuni ya Kimataifa ya uwekezaji wa Mafuta na Gesi ya Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeshajizatiti katika kutoa ushirikiano wa kina kwa Taasisi au Kampuni ye yote iliyoonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi Zanzibar.

Balozi Seif alisema Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar  zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu jambo ambalo  ushirikiano utakaotolewa kwa  Kampuni hiyo ya Mafuta na Gesi  ya China ni muendelezo wa uhusiano huo.

“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wa Karibu katika kuona malengo ya Kampuni ya CNOOC yanafanikiwa vyema “. Alisema Balozi Seif.

Alisema Suala la Mafuta na Gesi kwa  sasa tayari limeshapatiwa maamuzi na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutolewa ndani ya Mambo ya Muungano ili kuipa fursa pana Zanzibar kushughulikia yenyewe katika dhana nzima ya kujiimarisha Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alisema Zanzibar itaanza matayarisho kamili ya umiliki wa Sekta hiyo pamoja na Kuunda Shirika litakaloshughulikia Sekta ya Mafuta na Gesi mara baada ya kukamilika rasmi kipindi cha mpito cha uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment