Katibu kutoka Filmmaking Clinic of Tanzania (FCoT) Bw. Ignas Mkindi (Kulia) akizungumza na wadau wa filamu (hawapo pichani) wakati wa kongamano la wadau hao jana Mkoani Morogoro. Kushoto ni mdau wa filamu na mratibu wa kongamano Bw. Kheri Mkamba.
Mkurugenzi kutoka Tansquare film house Bi. Christina Mroni akichangia mada wakati wa kongamano la wadau wa filamu lililofanyika Jana Mkoani Morogoro kujadili changamoto na namna ya kukuza tasnia ya filamu nchini. (Picha zote na Genofeva Matemu -Maelezo)
Na Genofeva Matemu -
Maelezo,
WADAU wa filamu
nchini wameiomba Serikali ya awamu ya tano kutoa kipaumbele kwa viwanda
vitakavyofufuliwa kuzalisha DVD tupu na vifungashio vya kazi za filamu vyenye
kiwango hivyo kuinua sekta ya filamu kwa kasi.
Rai hiyo imetolewa na
mdau wa filamu nchini Bw. Luhende Richard Luhende wakati wa kongamano la wadau wa filamu
lililoudhuriwa na watayarishaji na wazalishaji wa filamu jana Mkoani Morogoro.
Bw. Luhende amesema
kuwa Serikali ya awamu ya tano imelenga kukuza sekta ya filamu kwa kuandaa
ilani inayojali wasanii kama ilani hiyo ilivyoainisha katika ukurasa wake wa
219 pamoja na 220.
“Ilani ya chama cha
mapinduzi imelenga kukuza sekta ya fulamu hususani katika eneo la miundombinu,
ubora na weledi katika sekta na bidhaa zinazozalishwa pamoja na uimarishwaji wa
chombo chenye dhamana na filamu kwa maana ya bodi ya filamu, uanzishwaji na
uratibu wa mfuko ambao utawawezesha wasanii kupata mitaji hivyo kuzalisha
bidhaa zenye ubora” alisema Bw. Luhende.
Aidha Katibu Mtendaji
Bodi ya Filamu bibi. Joyce Fisoo amesema kuwa Serikali imekua ikitoa wito kwa wawekezaji
ambao wako tayari kujitokeza kuwekeza katika miundombinu ya filamu hususani
jumba changamani la filamu kwa lengo la kuinua
wasanii na kukuza tasnia ya filamu.
Bibi. Fisoo amewataka
wasanii kushirikiana, kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na wadau mbalimbali,
kujiunga na mafunzo ya muda mfupi kuongeza ujuzi, na kupunguza utamaduni wa
kuongelea masuala yasiyokua na tija bali kutumia muda walionao kufanya kazi kwa
bidii kama hari iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya awamu ya tano.
Naye mwakilishi
kutoka Proin Promotion Bw. Josephat Lukaza ameipongeza bodi ya filamu
kushirikisha wadau wa filamu kwenye matamasha mbalimbali yakiwemo matamasha ya
JAMA Festival, Nepal Afrika inayotarajia kufanyika Februari 2016, pamoja na
kwenda Misri kwa ajili ya tamasha la Script Writers litakalofanyika Desemba
mwaka huu, matamasha ambayo yanatoa fursa kwa wadau wa filamu kupata mbinu mpya
za kuendeleza tasnia ya filamu nchini.




No comments:
Post a Comment