TANGAZO


Monday, November 30, 2015

Maonesho ya Jua Kali kufunguliwa rasmi Jumatano

Mwenyekiti wa Shirikisho la wajasiriamali Afika Mashariki Bw. Josephat Rweyemamu (katikati) akiangalia bidhaa zinazotokana na karanga  kutoka kwa wajasirialiamali katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dare s salaam  kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Ajira kutoka Wizara ya Kazi Ajira na Bw. Ali Msaki. (Picha zote na Raymond Mushumbusi -Maelezo)
Baadhi ya bidhaa zinazopatika katika maonesho ya Jua Kali yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya wajasiriamali  kutoka nchi wanachama wa jumuia ya Afrika Mashariki wanaoshiriki maonesho ya Jua Kali yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Kikundi cha Jivunie Tanzania Sanaa Group kutoka Mbagala Jijini Dar es Salaam wakitumbuiza katika maonesho ya Jua Kali yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Na Jacquiline Mrisho- Maelezo 
MAONESHO ya Jua Kali yanayoshirikisha wajasiriamali kutoka  jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (EAC) yatafunguliwa rasmi Disemba 2 mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira Bw. Ridhiwani Wema kwamba maandalizi yanaendelea na washiriki toka nchi wanachama wameshafika kwa ajili ya maonesho hayo na takribani wajasiliamali 700 wanatarajia kushiriki maonesho hayo.

Akizungumza  katika maonesho hayo, Mkurugenzi kutoka Wizara ya Kazi na Ajira Bw.Ally Msaki amesema kuwa maonesho haya yanafanyika kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali waweze kupata masoko, kujifunza mbinu mbalimbali toka kwa wenzao na kuwawezesha kupata ajira.

Aidha Mwenyekiti wa Shirikisho la wajasiriamali wasiorasimishwa Afika Mashariki  (CISO) Bw. Josephat Rweyemamu alielezea umuhimu wa maonesho hayo kuwa ni ushirikiano wa wajasiriamali kutoka umoja wa Afrika Mashariki, kujitangaza kibiashara, kujifunza kutoka kwa wenzao, wajasiriamali   kujua taratibu za kurasimisha biashara zao na kuongeza wigo wa biashara zao.

“ Tumezialika taasisi mbalimbali kama Benki ya CRDB, mfuko wahifadhi ya  jamii wa NSSF na Mamlaka ya Usajili wa biashara (BRELA) ili kutoa elimu kwa  wajasiriamali juu ya upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu, kuwekeza katika mifuko ya jamii na jinsi ya kurasimisha biashara zao,” alisema Rweyemamu.

Bw. Josephat Rweyemamu ameendelea kusema kuwa Serikali inatoa mchango mkubwa katika kufanikisha maonesho haya kwa kuwapa eneo na kutowatoza kodi za ndani kwa washiriki ingawa wanatakiwa kuchangia kiasi cha shilingi elfu arobaini kama ada ya ushiriki.

Mmoja kati washiriki toka Uganda Bi Josephine Ikiri-g amesema ni mara yake ya pili kushiriki katika maonesho hayo na kuna changamoto zinazowakabili ambazo  ni  elimu ndogo kwa wajasiriamali, kutoelewana  kwa kuwa hakuna lugha rasmi ya kuunganisha wajasiriamali na wateja, ukosefu wa masoko wa bidhaa zao kwani waafrika wengi hawataki kutumia bidhaa asili zinazotengenezwa ndani ya nchi.

Mjasiriamali kutoka Mkoani Morogoro Wilaya ya Kilosa Bw Leonard Mtunda amesema ni mara yake kwanza kushiriki katika maonesho hayo na ameweza kupata elimu ya ujasiriamali iliyoratibiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) iliyotolewa kwa wajasiriamali 150 kabla ya kuanza maonesho hayo.

Maonesho ya Jua Kali yalianzishwa Novemba 1991 wakati wa kusaini mkataba wa jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya wakuu wa nchi wa umoja huo kupendezwa na maonesho na  kuazimia yafanyike Novemba ya kila mwaka pindi wanapokutana katika mkutano wao  kwa kukutanisha wajasiriamali toka nchi wanachama na kufanya maonesho ya bidhaa mbalimbali.

No comments:

Post a Comment