Mji wa Durban, nchini Afrika Kusini, umeteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Jumuiya ya Madola, mwaka wa 2022, na kuwa mji wa kwanza barani Afrika, kuandaa mashindano hayo.
Jiji hilo lililoko pwani ya Mashariki ya Afrika Kusini, ndilo pekee lililokuwa limesalia kati ya miji iliyotaka kuwa mwenyeji baada Edmonton ya Canada kujiondoa Februari kwa sababu za kifedha.
Michezo hiyo itaanza Julai 18, tarehe ambayo ingelikuwa siku ya kuadhimisha miaka 104 ya kuzaliwa kwa rais wa zamani wa Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela na kumalizika Julai 30.
Itakuwa ni mara ya 22 ya kuandaliwa kwa mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka minne.
Wanariadha kutoka zaidi ya mataifa 50, mengi ambayo yalikuwa koloni za Uingereza, watashiriki.

Tangazo hilo lilitolewa katika mkutano mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF) mjini Auckland.
Rais wa kamati ya michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola mwanamfalme Tunku Imran amesema "Kama kundi, tuko pamoja katika kuunga mkono michezo ya kwanza kabisa kufanyika barani Afrika,"
Miundo mbinu mingi itakayotumika tayari ipo, huku eneo la mbio likitarajiwa kuongezwa uwanja wa Moses Mabhida, uliojengwa kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2010.
Inaaminika hatua ya kukubali michezo hiyo iandaliwe katika jiji la Afrika kwa mara ya kwanza huenda ikaifanya Afrika Kusini kujaribu tena kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki.
Jiji la Cape Town lilimaliza nambari tatu katika kinyang'anyiro cha kutafuta mwenyeji wa michezo ya 2004.
Michezo ya Jumuiya ya Madola iliandaliwa mara ya mwisho Glasgow 2014, na jiji la Gold Coast, Australia ndilo litakuwa mwenyeji wa mashindano hayo 2018.


No comments:
Post a Comment