TANGAZO


Tuesday, September 8, 2015

Makamu wa Rais Dk. Gharib Bilal ataka vifaa vya Taasisi ya Upasuaji wa Moyo vitunzwe

Naibu waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Stephen Kebwe akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa mkutano wa waganga wakuu wa mkoa na wilaya katika hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Magreth Kinabo – Maelezo) 
Naibu waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Stephen Kebwe akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi wa mkutano wa waganga wakuu wa mkoa na wilaya katika hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waganga wakuu wa mikoa na wilaya wakiwa katika mkutano huo. 
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani WHO, Dkt Rufaro Chatora akizungumza katika mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika Hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es Salaam. 
Mwakilishi kutoka Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) Dkt.Jama Guleid mkutano wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya katika Hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es Salaam. 
Wasanii wa Mjomba Band. Mrisho Mpoto (kushoto) na wenzake wakitumbuiza katika mkutano huo. 
Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal akifungua mkutano wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya katika hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es salaam. 
Makamu wa Rais akitoa tuzo kwa mdau wa Afya, Profesa Philemon  Sarungi kwa kutambua mchango wake katika sekta ya afya nchini.
Katibu Mkuu wa  Wizara ya Afya na Ustawi  Jamii, akipokea  tuzo ya kutambua mchango wake katika sekta ya afya kutoka kwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal  katika mkutano wa waganga wakuu wa mkoa na wilaya katika hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal (katikati) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kifungua mkutano wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya katika hoteil ya Blue Pearl leo jijini Dar es Salaam.

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
8/09/2015
MAKAMU wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal ametoa rai kwa wataalamu wa Taasisi ya Upasuaji Mkubwa wa Moyo katika Hospital ya Taifa  ya Muhimbili (MNH) kutunza vifaa vya taasisi hiyo kwa kuvifanyia matengenezo kinga kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa.

Dkt. Bilal ameyasema hayo wakati akizindua mkutano wa mwaka wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya sambamba na maadhimisho ya miaka 40 ya mpango wa Taifa wa Chanjo uliyofanyika leo jijini Dar es salaam.

Aidha Makamu  wa Rais amesisitiza kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iandae utaratibu wa kutoa motisha kwa wataalamu wanaotoa huduma katika taasisi hiyo ili waendelee kuwepo na kutoa huduma stahiki na kushauri wataalamu zaidi kuongezwa.

Mbali na hayo Makamu wa Rais ameipongeza wizara,hiyo  kwa kuanzisha huduma ambazo hazikuwepo awali kwani kuanzishwa kwa huduma hizi kumeiwezesha Serikali kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Kwa upande mwingine Dkt Bilal amewapongeza wataalamu wa afya dhidi ya mapambano ya UKIMWI, kifua kikuu(TB), Malaria, pamoja na jitihada katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola na pia mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliyotokea hivi karibuni.

“Endeleeni kuwaelimisha wananchi namna bora ya kujinginga na kupambana na maradhi haya ya mlipuko yanayotokea nchini”aliongeza Dkt Bilal.

Kwa upande wake Naibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Stephen Kebwe amesema kuwa wizara yake,  inaendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu sugu kwa kufanya ugatuzi wa matibabu yake hivyo vituo vitano vimeanzishwa katika mikoa ya Dar es salaam, Geita, Mwanza pamoja na Zanzibar.

“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 90% ya wagonjwa wa kifua kikuu walioanza matibabu wanapona, ikilinganishwa na kiwango cha uponyaji kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani(WHO) cha asilimia 85% hivyo tumevuka lengo”aliongeza Dkt. Kebwe.

Dkt Kebwe ameongeza kuwa wizara inaendelea kuelimisha jamii kujiunga na bima mbalimbali ya afya nchini  ili wananchi waweze kupata huduma  hiyo ya afya kwa gharama nafuu na kwa uhakika.

Pia ameongeza kuwa maboresho mengi yamefanyika katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NIHF) ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia Mfumo wa Malipo wa Kieletroniki kwa vituo 228 kati ya vituo 250 vilivyokusudiwa. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Donan Mmbando amesema kuwa sekta ya afya inahitaji kuwa na ufanisi na uwajibikaji na kuboresha uratibu kwa masuala ya afya nchini kwani uchumi wa dunia umeadhirika na mtikisiko wa rasilimali fedha hivyo kuadhiri nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

 “Hivyo tunatakiwa kujiimarisha na kujiendesha wenyewe kwani Serikali na wadau wengine wanapenda kuona thamani ya fedha inakwenda sambamba na matumizi.

“Tuimarishe vyanzo vya ndani vya mapato vya sekta ya afya.Fedha za misaada hazipo tena. Mkutano huu utajadili  namna ya kuimarisha vyanzo hivi vya mapato tunahitaji  umakini katika mjadala huu,” alisema Dkt. Mmbando.

Aliongeza kwamba  mifumo ya vyanzo hivyo  inapaswa kuimarishwa katika kufanikisha mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) katika sekta ya afya watunga sera huamini ya kwamba sekta ya afya ni chanzo muhimu cha ukuaji wa  uchumi nchini hivyo kushauri utunzwaji wa vyanzo hivyo vya mapato.

Naye mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani WHO Dkt Rufaro Chatora amesema kuwa shirika hilo linaendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika sekta ya afya ili kufanikisha malengo ya Milenia (MDGs).

Alisema leo katika mkutano wamesaini cheti cha kutoa cha kutoa dola za Marekani  619,000 kwa ajili ya vifaa tiba na ukusanyaji wa taarifa na kuboresha mifumo ya taarifa ya sekta ya afya.

Mwakilishi kutoka Shirika la Watoto Duniani UNICEF Dkt.Jama Guleid ameipongeza Serikali kwa kufanikiwa kupunguza vifo vya  watoto chini ya umri wa miaka mitano na wakina mamawajawazito kwa kiasi kikubwa. Aliongeza vifo hivyo vimepungua na kuwepo kwa huduma za chanjo.

“Ninapenda kuishauri Serikali ya Tanzania kutafuta njia ya kuwapa motisha madaktari na waguuzi waliotoa mchango katika sekta kwa ajili ya kupambana na magonjwa mbalimbali,” alisema Dkt Guleid.

Mkutano huo utakaofanyika kwa muda wa siku tatu umebeba kauli mbiu isemayo”uwajibikaji wa watumishi wa ngazi zote ndio msingi imara katika utoaji wa huduma za afya na ustawi wa jamii zenye ubora unaotakiwa, Ewe mtumishitimiza wajibu wako” pamoja na “chanjo ni zawadi ya maisha-chanjo ni haki ya kila mtu”.

Sambamba na mkutano huo wadau mbalimbali wa afya wakiwemo wastaafu wa afya kutoka serikalini, makatibu wakuu na maafisa wa afya walipatiwa tuzo kutambua mchango wao katika sekta ya afya na pia wataalamu walioshiriki kutoa huduma kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini Siera Leone na Liberia walipatiwa vyeti.

No comments:

Post a Comment