Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa Bodi ya Huduma za Makataba Tanzania (Bohumata), Bw.Comfort Komba
Na Frank Mvungi
Na Frank Mvungi
SERIKALI imejenga vituo 22 vya kutolea huduma za makataba katika Mikoa mbalimbali hapa nchini ili kuimarisha mfumo wa kutoa elimu kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mipango toka Bodi ya Huduma za makataba (Bohumata), Bw. Comfort Komba wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Komba amesema kuwa huduma za maktaba zimefika katika Mikoa 22, Wilaya 19 na tarafa 2 ikilinganishwa na vituo 17 vilivyokuwa Mikoani na 15 katika Wilaya mwaka 2005.
“Bohumata imeshirikiana na Halmashauri za Wilaya za Ruangwa, Chunya, Masasi, Mbulu na Ngara katika kuanzisha na kuimarisha Maktaba Mpya katika Halmashauri hizo.” Alisisitiza Komba.
Aliongeza kuwa uanzishwaji wa maktaba katika maeneo mbalimbali hapa nchini umesaidia kuongeza na kuhamasisha utamaduni wa kujisomea miongoni mwa wanajamii ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa maktaba hizo .
Akitaja mafanikio mengine Komba amesema ni ongezeko la kiwango cha elimu, maarifa, taarifa na ujuzi miongoni mwa wanajamii.
Pia Komba alitoa wito kwa watanzania na wasio watanzania kujenga utamaduni wa kutumia maktaba za umma kwa kuwa zipo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.
Bodi ya Huduma za maktaba Tanzania (Bohumata), ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 6 mwaka 1975 ikiwa na jukumu la kuanzisha, kusimamia, kuongoza, kuimarisha, kutunza na kuendeleza maktaba za umma ili kujipatia elimu, maarifa, taarifa, mbalimbali zitakazowasaidia katika kujiletea maendeleo.
No comments:
Post a Comment