Na Lilian Lundo, MAELEZO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete amezipongeza sekta binafsi kwa kukubali kusaini hati ya ahadi ya uadilifu katika harakati za mapambano dhidi ya rushwa na utovu wa nidhamu.
Rais alisema hayo katika wakati akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa hati hizo zinazojumuisha sekta ya Umma na Binafsi katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais alisaini hati tatu ambazo ni Hati ya ahadi ya uadilifu ya Viongozi wa Umma, hati ya ahadi ya uadilifu ya Utumishi wa Umma na hati ya uadilifu ya Sekta Binafsi.
“Ushiriki wa sekta binafsi katika hati hii utasaidia kuleta mabadiliko ya kuwa na mwenendo wa kimaadili ya mapambano dhidi ya rushwa” alisema Mhe. Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa badala ya wananchi na sekta binafsi kulalamika pembeni ni vyema kuwasilisha malalamiko yao katika sehemu husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Aidha, Rais aliongeza kuwa baadhi ya sekta binafsi zimekuwa zikiombwa na kutoa rushwa ili kupewa upendeleo wa kupata tenda serikalini, hivyo kwa kusaini hati hiyo ya ahadi ya uadilifu kutaondoa mianya ya upokeaji na utoaji rushwa katika sekta hiyo.
Hati ya ahadi ya uadilifu inakumbusha Makampuni, Viongozi na Watumishi wa Umma juu ya wajibu wao wa kuzingatia kanuni za maadili na mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Wazo la kuwa na ahadi ya uadilifu liliibuliwa katika maabara ya Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambapo ilionekanakuwa rushwa bado ni tatizo katika uendeshaji wa shughuli za Umma na Binafsi hususani utoaji huduma kwa umma na biashara.
mwisho
No comments:
Post a Comment