TANGAZO


Tuesday, August 18, 2015

Rais Jakaya Kikwete aongoza mazishi ya Diwani Mazongera

Rais Jakaya Kikwete akiweka mchanga kwenye kaburini la aliyekuwa Diwani wa Kata ya Yombo, jimboni Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Ubwa Idd Mazongera aliyefariki Agost 17 na kuzikwa leo, Agosti 18, huku Waziri wa Ujenzi Dkt John Magufuli akisubiri zamu yake, katika makaburi ya Kichangani, Bagamoyo. (Picha zote na Omary Said) 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri wa Ujenzi Dkt John Magufuli wakimfariji mjane wa marehemu Iddi Ubwa Mazongera aliyekuwa Diwani wa Kata ya Yombo, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani aliyefariki jana na kuzikwa leo kwenye makaburi ya Kichangani, Bagamoyo. Wa pili kushoto ni mke wa Rais, Mama Salma Kikwete. 
Rais Jakaya Kikwete akiweka mchanga kwenye kaburi la aliyekuwa Diwani wa Kata ya Yombo, jimboni Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Ubwa Idd Mazongera leo.
Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli akiweka mchanga kwenye kaburi la Diwani wa Kata ya Yombo, Jimbo la Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, Ubwa Idd Mazongera aliyefariki Agost 17 na kuzikwa leo, Agosti 18 ambapo Rais Kikwete aliwaongoza maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali mkoani humo, kushiriki maziko hayo. 
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete akiweka mchanga kwenye kaburi la Diwani wa Kata ya Yombo, Jimbo la Bagamoyo, mkoani Pwani, Ubwa Idd Mazongera aliyefariki Agost 17 na kuzikwa leo, Agosti 18.

Na Omary Said, Yombo
Agost 18
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete Agost 18 amewaongoza maelfu ya wakazi katika mazishi ya Diwani wa Kata ya Yombo, Jimbo la Bagamoyo, Mkoa wa Pwani aliyemaliza muda wake, Ubwa Idd Mazongera aliyefariki Agost 17.

Katika mazishi hayo, Rais Kikwete aliwaongoza wananchi kutoka kila kona ambao walihudhuria mazishi ya diwani huyo, ambaye ameiongoza kata hiyo kwa vipindi viwili vya mwaka 2000 hadi 2005 na 2010 na 2015.

Katika mazishi hayo, Rais Kikwete aliongozana na mkewe, Mama Salma Kikwete, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Evarist na viongozi mbalimbali.

Katika mazishi hayo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Kombo Kamote akisoma wasifu wa Mazongera alieleza kwamba katika kipindi chake cha udiwani alitoa mchango mkubwa wa kuwatumikia wananchi kwa kushirikiana ipasavyo na serikali katika kuhakikisha wanawatumikia vema wananchi wao.

“Katika uhai wake na utumishi, Mazongera alipigania maendeleo ya Kata na Wilaya ambapo katika vikao mbalimbali vya Halmashauri alikuwa mstari wa mbele kuchangia mada ambazo kwa kiasi kikubwa zilileta maendeleo,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Kombo.

Aidha, taarifa hiyo, imeeleza kuwa marehemu Mazongera ametoa ardhi ya familia ambayo imejengwa Kituo cha Afya kinachoelekea ukingoni mwa ujenzi wake, ndani ya kata hiyo.

“Chama tunatoa wito kwa viongozi wa kuchaguliwa Madiwani na Wabunge kuhakikisha wanatimiza ahadi ambazo zilitolewa na chama mwaka 2000 hadi 2005 na 2010 na 2015 ambapo umati umefika. 

Chama hicho kupitia kwa diwani huyo na wengine ili kuwapatia imani wananchi dhidi ya serikali yao,” ilimalizia sehemu ya taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment