Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva
Na Magreth Kinabo
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa watakwenda kuchukua fomu pamoja na wafuasi wao kuzingatia suala la amani na utulivu.
Aidha Tume hiyo imewataka viongozi hao kuwa waangalifu na matamshi ambayo yanaweza kuhatarisha amani na utulivu.
Kauli hiyo, imetolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, wakati akizungumza na waandishi habari katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo kuhusu mchakato wa uchukuaji fomu za wagombea wa kiti cha urais utakaoanza Agosti Mosi mwaka huu.
Alisema kila mwananchi anayohaki na uhuru wa kushiriki shughuli za utawala wa nchi ikiwa ni pamoja haki ya kuchagua na kuchaguliwa au kuanzisha na kujiunga na vyama vya siasa kama ilivyo katika Ibara za 20 na 21 za Katiba ya mwaka 1977.
Jaji Lubuva aliongeza kwamba shughuli hizo kwa mujibu wa Katiba zimewekewa mipaka chini ya Ibara ya 30 ya Katiba. Kwamba, haki ya kushiriki isifanywe kwa namna ya kuingilia kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.
Alisema shughuli zinazoanza kesho na siku zinazofuata za kuchukua fomu vyama vyote ni lazima zifuate na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Sheria.
Hivyo lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato wote tangu mwanzo wa kuchukua fomu na kuzirudisha na baadaye yatakayofuata hadi mwisho wa kampeni na kupiga kura unafanyika kwa amani na utulivu nchi nzima.
“Viongozi mbalimbali wanaokuja kuchukua fomu kutoka tume , waje kwa amani na waondoke kwa amani pamoja na wafuasi wao.
“Shamrashamra zitakazoambatana nao zisiwe chanzo cha vurugu au kusababisha adha kwa wananchi wengine. Uchaguzi si ugomvi kati ya wagombea au wafuasi wao. Vinginevyo sheria itachukua mkondo wake,” alisema Jaji Lubuva.
Aidha, tume hiyo imewakuambusha wagombea hao na vyama vyama vyao kuzingatia maadili ya uchaguzi yaliyotiwa saini Julai 27, mwaka huu.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar esSalaam Kamishna Suleiman Kova alisema jeshi hilo liko katika mkakati wa hali ya juu ya kuhakikisha uchaguzi ufanyika kwa amani na usalama, hivyo halivumilia vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani, hatua kali za kisheria zitaweza kuchukuliwa.
Kamanda Kova aliongeza kwamba shughuli za kijamii zitaendelea kama kawaida wakati wa uchukuaji fomu.
Alisema wagombea hao pamoja na wafuasi wao watatakiwa kutumia barabara ya Oboma hadi klabu Jimy Cana jijini Dar es Saam ambapo watawaacha washabiki wao baada ya kuchukua fomu watawapitia ili kuweza kupunguza msongamano.
Jaji Lubuva aliongeza kuwa kesho wagombea wa kiti cha urais kutoka vyama vitatu watafika NEC kuchukua fomu, ambao ni UPDP saa 3:00 asubuhi, TLP saa 6:00 mchana na DP saa 8:00 mchana.
Alivitaja vyama vitakavyofuata kuwa ni Agosti 4, mwaka huu na Agosti 5, mwaka huu kuwa ni ADC saa 3:00 asubuhi na TADEA saa 4:00 asubuhi.
Akizungumzia kuhusu ratiba ya uchukuaji fomu, kwa wagombea wa kiti cha urais, ubunge na udiwani, Mkuu wa Idara ya Uendeshaji kutoka NEC Clothilde Komba alisema inaanza Agosti Mosi, mwaka huu na kumalizika Agosti 21,mwaka huu saa 10:00 jioni.


No comments:
Post a Comment