Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Bw. Bahame Nyanduga akisisitiza
jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo hii jijini Dar es
Salaam wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi za
kuwapiga na kuwazalilisha Viongozi na Wafuasi wa CUF huko Mtoni Mtongani
Temeke, jijini. (Picha na Eliphace
Marwa-MAELEZO)
Na PIUS YALULA, Maelezo
20.05.2015 TUME ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora imelaani vitendo vya uzalilishaji vilivyofanywa kwa Viongozi wa
Chama cha Wananchi (CUF) Januari 27 mwaka huu (2015) wakati wa maandamano ya
Chama hicho Mtoni Mtongani Wilaya ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo (Mei 20, 2015) Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame
Nanduga, alisema uchunguzi wa tukio hilo umekamilika kwa kuzingatia kifungu cha
130 [1] [c], [f] na [g] cha katiba ya jamhuri ya Muungano.
Aidha aliongeza kuwa sheria
nyingine zilizotumika kuchunguza tukio hilo ni pamoja na kifungu cha 6[1][c]na
[g] vifungu 15[1][a] na 28[1][a],[b] na f vya Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora Na.7 ya mwaka 2001, sheria ya polisi na polisi wasaidizi, sura
322, na sheria ya vyama vya siasa, sura 258.
Nyanduga alisema Tume yake imebaini
ukikwaji mkubwa wa haki za binadamu
waliofanyiwa viongozi na wanachama chama cha wananchi CUF katika maandamano yao
ya shughuli za kichama, hivyo Tume ilibaini kuwa jeshi la polisi lilitumia
nguvu kupita kiasi, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na udhalilishaji wa
wanachama wawili wa kike wa CUF.
“Tume imetoa mapendekezo
kwa jeshi la pilisi kuzingatia kanuni, sheria,
haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake
ya kila siku na kuhakikisha maafisa wake wanajipanga vyema katika kuratibu na
kusimamia utekelezaji wa operesheni zake” alisema Nyanduga.
Kwa mujibu wa Nyanduga tume
hiyo pia imewataka Viongozi na wanachama wa CUF kutafuta namna ya kuboresha
mahusiano na jeshi la polisi, ili kuondoa
mivutano isiyo na tija.
Tume imepanga kuitisha
mafunzo na mikutano mbalimbali kwa kushirikiana na vyama vya siasa,Tume ya Taifa
ya Uchaguzi [NEC], pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi
na Magereza, msajili wa vyama vya siasa, na asasi za kiraia ili kupanga
taratibu zote katika kujua haki za binadamu na utawala bora.


No comments:
Post a Comment