TANGAZO


Friday, May 22, 2015

Taasisi za Dini Zanzibar zaaswa kutoegemea Chama chochote cha Siasa

Mwenyekiti wa Semina ya kuhamasisha viongozi wa Dini ya Kiislamu katika kusimamia Amani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 Sheikh Khamis Abdulhamid akiongoza washiriki wa semina hiyo.
Washiriki wa semina hiyo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwakilishwa kwenye Ofisi ya Jengo la Bima Mperani Mjini Unguja.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Zanzibar Dr. Muhyiddin Ahmad Khamis akiwasilisha mada  juu ya Nafasi ya Uislamu katika kujenga na kudumisha amani katika Jamii kwenye semina ya kuhamasisha amani wakati wa uchaguzi mkuu.
Mratibu wa GNRC  Zanzibar Mohd Hafidh akifunga semina hiyo. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar)
Imamu wa Msikiti Mkuu wa Msumbiji, Sheikh Othman Khamis Ali akichangia katika mkutano huo.
Picha No. 037- Katibu Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdulla Talib Abdulla akiwasilisha mada juu ya Nafasi ya Taasisi za kidini katika kufanikisha uchaguzi wa Amani na uadilifu 2015.

Na Ramadhani Ali, Maelezo Zanzibar 
22.05.2015
KATIBU Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdulla Talib Abdulla amesema Taasisi za dini  hazipaswi  kuegemea upande wa chama chochote cha siasa ama kushiriki katika kampeni za uchaguzi lakini zinawajibu wa kujenga jamii ishiriki kikamilifu kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kujenga matumaini makubwa ya kuwa na amani.

Sheikh Abdulla Talib ameeleza hayo alipokuwa akiwasilisha mada ya nafasi ya Taasisi za kidini katika kufanikisha uchaguzi wa amani na uadilifu katika Semina ya kuhamaisha Viongozi wa dini ya Kiislamu  kusimamia amani wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Amesema dini inamisingi muhimu inayoweza kutumika katika kujenga  amani  kwani kuna uhusiano mkubwa wa kinadharia baina ya dini na uchaguzi wa amani na uadilifu.

Ameongeza kuwa kufanya kazi ya kujenga amani ni kutekeleza dhamana ya dini kwani uislamu wakati wote unasisitiza umoja, upendo na  amani ya kila mtu.

 Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana amewaeleza washiriki wa semina hiyo ambao ni masheikh na wanazuoni kutoka mikoa mitatu ya Unguja kwamba wanadhima ya kusisitiza kufuatwa sheria na uadilifu kuanzia sasa mpaka  kutangazwa matokeo ya uchaguzi.

“Uchaguzi wa amani unahitaji kuwepo uadilifu, kufuatwa taratibu na miongozo katika mchakato wote, ushirikishwaji wa pande zinazohusika  kwa mujibu wa matakwa ya kisheria, kutolewa elimu ya kutosha ya uraia, uwazi na uwajibikaji pamoja na kuyakubali matokeo,”alieleza Sheikh Abdulla Talib.

Katika kufanikisha  uchaguzi  huru na haki Sheikh Talib ameshauri  kuwa na matumizi mazuri ya nyumba za Ibada na maeneo ya kidini  pamoja na matumizi mazuri ya aya, hadithi, nukuu za kihistoria na hekma nyengine.

“Kwa kuzingatia uhalisia wa uchaguzi, taasisi za kidini zinapaswa kutumia mbinu na taratibu za kidini na nyenginezo katika kulingania uchaguzi wa amani, ”aliongeza sheikh Abdulla Talib.

Aliwakumbusha wanazuoni hao kuwa Zanzibar ni nchi ndogo yenye watu wachache wenye uhusiano  wa karibu na tatizo linapotokea huzigusa familia nyingi hivyo amewashauri mahubiri yao  yalenge kufanyika uchaguzi katika misingi ya uhuru, uwazi, haki, amani na utulivu.

Washiriki wa semina hiyo wameiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa waadilifu na kufuata taratibu na sheria zote za uchaguzi kuanzia hatua za kuliboresha daftari  la wapiga kura hadi kukamilika zoezi  la uchaguzi bila ya kuingiza  ushabiki wa kisiasa.

Katika maazimio yao  masheikh hao wametaka kuhakikishiwa usalama wao wakati wa kutekeleza jukumu la kuwahubiria wafuasi wao kwani  wameingiwa na wasi wasi wa kukamatwa kutokana na  visingizio mbali mbali.

Semina hiyo iliyofanyika katika jengo la Ofisi ya Bima Mperani, iliandaliwa na Jumuiya ya JUMAZA na UKUEM kwa kushirikiana na mtandao wa kimataifa wa dini kwa ajili ya kulinda watoto (GNRC).

No comments:

Post a Comment