Mbunge wa Kisarawe (CCM) Bw. Suleiman Jafo akichangia mjadala wa bajeti ya wizara ya uchukuzi leo bungeni mjini Dodoma.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwezeshaji, Bi. Mary Nagu akizungumza na Waziri
wa Maliasili na Utalii Bw. Lazaro Nyalandu kwenye ukumbi wa Bunge mjini Dodoma
leo.
Na Fatuma Fatma Salum-Maelezo
SERIKALI kupitia Wizara ya Uchukuzi imesema
inakaribisha wawekezaji binafsi kwenye miradi mbalimbali ili kuboresha sekta za
uchukuzi na hali ya hewa hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe.
Dkt. Charles Tizeba wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizowasilishwa kwenye
mjadala wa bajeti ya wizara hiyo leo bungeni mjini Dodoma.
“Serikali inawakaribisha wawekezaji binafsi
kuwekeza kwenye miradi ya kuboresha miundombinu ya uchukuzi na hali ya hewa kwa
kuwa Serikali peke yake haiwezi kukamilisha miradi yote bila ya ushirikiano na
wengine”.
Dkt. Tizeba alisema Serikali ina mipango
madhubuti ya kuboresha miundombinu nchini ikiwemo reli, bandari na barabara na
kupitia dhana ya ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi (Public Private
Partnership) itaweza kufanikisha mipango hiyo kwa ufanisi na kwa wakati.
Aidha Dkt. Tizeba aliongeza kuwa kupitia
juhudi za Serikali baadhi ya miradi ipo katika hatua za awali ikiwemo
uboreshaji wa viwanja vya ndege 11 kwenye mikoa mbalimbali nchini ambapo
wataalamu wameshafanya upembuzi yakinifu (Feasibility Study) na fedha zikipatikana
vitafanyiwa matengenezo mara moja.
Akizungumzia upanuzi wa bandari ya Dar es
Salaam Dkt. Tizeba alibainisha kuwa taratibu za kumpata mzabuni zinaendelea na
akipatikana ujenzi wa gati namba 13 na 14 za bandari hiyo utaanza.
Leo Waziri wa Uchukuzi Mhe. Samuel Sitta
aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka
2015/2016 ambapo bunge lilikubali kupitisha zaidi ya shilingi bilioni 452.9.

No comments:
Post a Comment