Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Morogoro (Moruwasa), Mhandisi Nicholaus Angumbwike, akizungumza na waandishi wa habari.
Hussein Makame-MAELEZO
MAMLAKA
ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya
Morogoro (MORUWASA), imepanga kuongeza uwezo wa bwala la Mindu mara mbili zaidi
ili liweze kukusanya maji mengi zaidi kukidhi mahitaji ya maji ya wakazi wa
manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari
waliomtembelea ofisini kwake mjini Morogoro, mwisho mwa wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka
hiyo Mhandisi Nicholaus Angumbwike, alisema pia wamepanga kujenga
mtambo mwengine wa kutibu maji ili kuongeza kiasi cha maji kutoka chanzo hicho.
Alisema
tayari mkandarasi ameshaandaa pendekezo la mradi (proposal) kupitia awamu ya
kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na kwamba imeshakamilika na ameiwasilisha Wizara ya Maji
kwa ajili ya utekelezaji.
Mhandisi Angumbwike aliongeza kuwa wanatarajia
kwamba utekelezaji wa mradi huo utafanyka katika awamu ya pili ya WSDP iliyoanza
Juni mwaka jana iwapo Wizara itawapatia fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
“Kuna utafiti imeshafanyika kuhusu bwawa la Mindu,
kuna uwezekano kwamba uwezo wa bwala la Mindi ukaongezeka mara mbili zaidi
yaani uwezo wa kukusanya maji mengi zaidi kuliko ilivyo sasa na tukajenga
mtambo mwengine wa kutibu maji ili kuongeza kiasi cha maji yanayotoka chanzo
cha bwawa la Mindu” alisema Mhandisi Angumbwike na kuongeza:
“Hii kazi imeshafanyika katika mradi wa WSDP awamu
ya kwanza, mkandarasi amefanya akaandaa proposal yake na tuna matumaini kwamba
ameshakamilisha na amewasilisha Wizara ya Maji, tunatarajia katika hii awamu ya
pili kama Wizara ikitufikiria tuweze kutekeleza mradi huo”
Alisema kinachotakiwa kufanyika ni kuongeza tena
urefu wa tuta la bwawa hilo kwa urefu wa mita 2 na kujenga mtambo mwingine wa
kutibu maji kwani mtambo ulipo una uwezo wa kutibu maji kwa siku lita milioni
27 tu.
Aliongeza
kuwa gharama za mradi huo wa kuongeza uwezo wa chanzo hicho cha maji cha bwawa
la Mindu na mtambo wa kutibu maji, kwa mwaka 2008 ilikuwa ni shilingi Bilioni
35.
Alisema mbali na juhudi hizo MORUWASA imekuwa
ikitafakari vyanzo vingine vya maji kukidhi mahitaji ya wakazi 315,000 wa
manispaa ya Morogoro ikiwemo kufikiria kwenda juu zaidi ya milima ya Uluguru
kutafuta vyanzo hivyo.
Alisema wanaangalia uwezekano wa kuchimba visima
virefu lakini changamoto iliyopo ni kwamba ni shida kupata maeneo ambayo
watapata maji baridi kwa sababu maeneo mengi ya Morogoro ukichimba unapata maji
ya chumvi.
Kwa upande wa uboreshaji wa miundombinu chakavu,
Mhandisi Angumbwike alisema wamepokea fedha kiasi cha shilingi Milioni 240
kutoka Wizara ya Maji ambayo itatusaidia kubadilisha kilomita kadhaa ya miundombinu
ya maji iliyochakaa ili kuboresha upatikanaji wa maji.
Katika kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji
vilivyopo, Mhandisi Angumbwike alisema wanashirikia na wadau wengine kama Ofisi
ya Bonde la Maji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manispaa ya Morogoro, katika kulinda vyanzo hivyo.
“Tumekuwa tukifanya kazi pamoja, tunakutana pamoja
tunakwenda kwenye miradi (sites) tumeainisha maeneo ambayo yanataka kuyatunza,
tumetoa elimu kwa wananchi watambue kwamba jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni
la kila Mtanzania na wao wakiwemo”alisema na kuongeza:
“Wananchi wanatakiwa watambue kwamba jukumu la
kutunza vyanzo vya maji ni muhimu kwa manufaa ya Watanzania wote”
Kuhusu wizi wa maji,
Mkurugenzi huyo alisema wana Operesheni za kukamata watu wanaojiunganishia maji
kwa kupita nyumba kwa nyumba ili kuwabaini na kuwakamata watu ambao wanatumia
maji bila kuyalipia.
“Wapo watu ambao wanataka
wapate maji bila kuyalipia, tunafanya operesheni nyumba kwa nyumba na tunapowakamata
tunawatoza faini na kuwachukulia hatua lakini shida kubwa ni uunganishaji
mwingine ni ngumu kuubaini” alisema Mkurugenzi huyo na kuongeza:
“Wapo tuliowakamata kwa ushirikiano na wananchi na
tunatoa motisha wa fedha kwa wananchi wanaotupa taarifa hizo. Pia tunacho
kikosi maalum kinachopita mitaani na katika hoteli mbalimbali kuchunguza mifumo
ya maji ili kubaini watu wanaoiba maji.
Tumeshakamata baadhi ya hoteli zimejiunganishia
maji, tukawauliza wanasema wamechimba kisima lakini baada ya kupima sampuli ya
maji tunakuta kwamba ni maji ya Morowasa”
Hivyo aliwataka wananchi
kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuwafichua wezi wa waji au watu
wanaojiunganishia maji kiholela ili kudhibiti asimilia 40 ya maji ambayo
hayaipatii mapato MORUWASA.
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Maji (WSDP) ya mwaka 2006 hadi
2025, inatekelezwa kwa awamu ya miaka mitano mitano ambapo awamu ya Kwanza
ilianza mwaka 2007 na kukamilika 2014 na awamu ya Pili ilizunduliwa na Waziri
wa Maji Juni mwaka jana tayari kwa utekeleaji.
No comments:
Post a Comment