Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akifuatana na mgeni wake Balozi wa Jamhuri ya Uholanzi nchini Tanzania Mhe,Jaap Fredriks alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiagana na mgeni wake Balozi wa Jamhuri ya Uholanzi nchini Tanzania Mhe,Jaap Fredriks alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao.
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa hatua za mwanzo zinazoendelea
katika ujenzi wa wodi mpya ya mama wajawazito na watoto katika hospitali ya Kuu
ya Mnazi Mmoja chini ya Mradi wa ORIO zinaleta matumaini katika kuimarisha
sekta ya afya hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Mhe.
Jaap Fredriks yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo
hayo Dk. Shein aliipongeza Serikali ya Uholanzi kwa hatua yake ya kuunga mkono
juhudi hizo za ujenzi wa wodi hiyo mpya chini ya Mpango wa ORIO ambapo alisema
hatua hiyo inaonesha azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuimarisha sekta ya
afya na kukuza huduma kwa jamii.
Dk.Shein alisema
kuwa hatua za awali za ujenzi huo zimekuwa zikienda vizuri na kueleza matumaini
yake makubwa ya kukamilika kwa mradi huo kwa wakati uliopangwa ili uweze kuleta
manufaa kwa wananchi sambamba na kukuza sekta ya afya.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa mashirikiano hayo yanayotolewa na Serikali ya Uholanzi katika
ujenzi wa wodi hiyo mpya ya akina mama na watoto yatasaidia zaidi katika
kufikia lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Afya
ya kuifanya hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa ya rufaa.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Uholanzi kwa kuendelea na juhudi zake za
kuunga mkono na kutoa ushirikiano wake katika utekelezaji wa Mradi wa ORIO
katika ujenzi wa Kiwanda cha dawa na vituo vya afya hapa Zanzibar.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alipongeza azma na utayari wa Uholanzi wa kuendelea kutoa mafunzo kwa
wataalamu mbali mbali juu ya sekta ya nishati hapa nchini kwa kutegemea
mahitaji ya serikali.
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Uholanzi kwa kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo na kuahidi kuwa
Zanzibar itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake kati yake na
Uholanzi.
Nae Balozi wa
Uholanzi nchini Tanzania Mhe. Jaap Fredriks alimueleza Dk. Shein juhudi
zinazochukuliwa na Uholanzi katika kuhakikisha mradi huo wa ujenzi wa wodi mpya
unakwenda vizuri ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Alisema kuwa
Uholanzi itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za
maendeleo ikiwemo sekta ya afya na nyenginezo kwa kutambua malengo yake ya
kukuza uchumi wake na kuimarisha sekta za kijamii sambamba na kupambana na
umasikini.
Balozi Fredriks,
alisema kuwa Uholanzi kupitia Mradi wake wa ORIO utahakikisha mradi huo wa
ujenzi wa wodi mpya ya akina mama na watoto unaleta tija kwa Serikali na
wananchi kwa jumla hasa akina mama na watoto ambao ndio walengwa wakuu.
Pamoja na hayo,
Balozi huyo wa Uholanzi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema kuwa
mbali ya Mradi huo Serikali ya Uholanzi pia, inaendelea kuunga mkono ujenzi wa
Kiwanda cha Madawa na vituo vya Afya kupitia Mradi wake huo wa ORIO.
Kwa upande wa
vituo vya Afya, Balozi Fredriks alisema kuwa juhudi za makusudi zinachukuliwa
na Ubalozi wake katika kuangalia utekelezaji huo unafanikiwa vyema kwa upande
wa Unguja na Pemba.
Nae Mratibu wa
Kanda anaeshughulikia nishati kwa nchi ya Tanzania na Msumbiji Bibi Marijn
Noordam alimueleza Dk. Shein azma na
utayari wa Uholanzi wa kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Zanzibar juu ya
sekta ya nishati.
Alisema kuwa
tayari mipango maalum imeshawekwa juu ya utoaji wa mafunzo hayo kwa kutegemea
mahitaji ya Serikali.
Uholanzi na
Zanzibar zimekuwa na mahusiano mazuri na ya kihistoria ambapo mahusiano hayo na
ushirikiano huo uliimarika zaidi pale Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipofanya ziara nchini humo mnamo mwezi
Ogasti mwaka juzi.
Katika ziara yake
hiyo Dk. Shein alifanya mazungumzo na viongozi mbali mbali wa Serikali ya
Uholanzi pamoja na wakuu wa Kampuni za kibiashara, Watanzania wanaoishi nchini
humo na kutembelea sehemu za kihistoria.
Wakati huo huo,
mnamo Februari 20 mwaka jana Waziri wa Biashara za Nje na Ushirikiano wa
Maendeleo Bibi Lilianne Ploumen alifika nchini akiongoza ujumbe wa wawakilishi
wa Makampuni 25 ya kibiashara ya Uholanzi.
No comments:
Post a Comment