Mshehereshaji
kwenye madhimisho ya siku ya redio duniani, Bi. Usia Nkhoma Ledama
akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua rasmi
maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).
Na Mwandishi wetu, Arusha
VYOMBO
vya habari hususan redio za jamii zimetakiwa kutanguliza uzalendo na
kutetea maslahi ya taifa ili kuliepusha taifa katika migogoro na
mitafaruku inayoweza kusababisha machafuko nchini hasa katika kipindi
cha uchaguzi mkuu ujao.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha Nyerembe
Munasa wakati wa kuadhimisha Siku ya Redio duniani iliyofanyika mwishoni
mwa wiki.
Akizungumza
na watangazaji wa redio za jamii na wadau mbalimbali wa habari nchini
katika ufunguzi wa maadhimisho hayo Munasa alisema redio ina nguvu kubwa
kuchambua na kutengeneza mustakabali wa taifa na hasa vijana iwapo
itatumika vizuri badala ya kuwa chanzo cha matatizo na uchochezi mambo
ambayo yanaweza kulisambaratisha taifa.
Amewataka
waandishi na watangazaji wa redio jamii kuzingatia maadili ya kazi zao
kwa lengo la kuleta mabadiliko katika maisha ya Watanzania na kujenga
taifa endelevu .
Mkuu
wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, Nyerembe Munasa akizungumza katika
ufunguzi wa kuadhimisha siku ya redio duniani iliyofanyika mwishoni mwa
wiki jijini Arusha.
“Mnatakiwa
kutafiti, kutathmini na kupeleka taarifa zenye tija na kuhamasisha
vijana kujituma kufanya kazi kwa bidii ili kuondoa wimbi la umaskini kwa
wananchi na hasa vijana, mkitekeleza wajibu wenu kwa kujua nini
mnachofanya mtachochea mabadiliko kwa haraka katika jamii”.
Akizungumzia
fursa zilizopo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru ametoa wito pia kwa
vyombo vya habari hususani radio za jamii kuwawezesha vijana wa
Kitanzania kutambua na kutumia fursa zilizopo za uchumi wa gesi na
mafuta ili kujiondoa katika umaskini unaolalamikiwa kusababishwa na
ukosefu wa kazi.
“Pamoja
na utengenezaji wa vipindi vyenye kuelimisha jamii redio jamii lazima
ziwajibike kibinafsi na kijamii hadi ngazi ya taifa kwa kuwapa vijana
taarifa zilizosheheni fursa zilizopo na namna ya kuzifanyia kazi, ili
vijana waondokane katika migogoro na maandamano yasiyokuwa na tija kwa
sababu watakuwa wanajua nini cha kufanya ndani ya sheria na utengamano
wa amani”.
Amesema
vyombo vya habari jamii iwapo vitatumia vyema Katika kuwashirikisha
vijana vina uwezo na nguvu kubwa kubadilisha fikra za wananchi kwa
kutengeneza vipindi ambavyo vitachochea mawazo endelevu kwa kuzingatia
mila na utamaduni wa taifa la Mtanzania kuwakomboa vijana kuepukana na
utamaduni tegemezi unaosababisha kulemaa kwa vijana kutafuta njia za
mkato na kutopenda kufanya kazi jambo ambalo linasababisha mwendelezo wa
umaskini nchini.
Akizungumza
kwa wakilishi wa redio za jamii, waandishi na wadau wengine wa habari
mjini hapa, Munasa alisema majukumu matatu ya utangazaji wa redio,
yamekuwa hayafikiwi inavyotakiwa kutokana na wengi wa wahusika
kutofahamu vyema majukumu yao au kutowajibika kikamilifu.
“Utakuta
mwandishi wa habari hasa watangazaji anaingia studio hajajiandaa kwa
kufanya utafiti wa somo linalozungumziwa, hana mwongozo wa kipindi
(script), hana mpango kazi wa kipindi (programme matrix) na wala
mlolongo wa uendeshaji wa kipindi kinapoanzia na kuishia, hili ni tatizo
sio utangazaji!”
Baadhi
ya washiriki kutoka redio mbalimbali za jamii nchini wakimsikiliza
mgeni rasmi wakati akifungua rasmi sherehe za maadhimisho ya siku ya
redio duniani.
Pamoja
na kuwakumbusha watangazaji umuhimu wa kutangaza katika vyombo vya
habari hususan redio mkuu huyo wa wilaya aliwataka washiriki kubadili
mtazamo wa muziki kwa kupiga muziki wa asili kwa lengo la kupeleka
ujumbe mzito na wenye manufaa kwa taifa badala ya muziki uliojaa mahadhi
ya mapenzi na matusi.
“Muziki
una nguvu kubwa katika maisha ya binadamu watangazaji lazima mfahamu na
mjue namna ya kuupangilia kutokana na vipindi mnavyovitayarisha na muda
wa aina ya muziki husika. Sio wakati wote ni wakati wa kusikiliza
muziki wa mapenzi, kwa sababu redio husikilizwa na watu mbalimbali kwa
sababu mbalimbali pia.”
Suala
la mpangilio wa muziki, kuuelewa na thamani yake katika redio na umma
lilielezwa kwa undani zaidi na nguli wa masuala ya muziki katika vyombo
vya habari Masoud Masoud ambaye alisema kuwa watangazaji wa kisasa
wamekuwa hawaelewi maana ya muziki na faida zake Katika kuendeleza taifa
kitamaduni na kimaendeleo.
“Vijana
wengi wamekuwa wakitayarisha muziki wanaoupenda wao na sio unaopendwa
na kufufaisha umma, wakati umefika kwa kutafuta mbinu au jitihada zozote
za kuwafundisha muziki ni nini, unachezwa wakati gani na kwa manufaa ya
nani.”
Sherehe
hizo ambazo huandaliwa kila mwaka tarehe 13 Februari, ziliandaliwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na
ujumbe wa mwaka huu ni “Nguvu ya Redio na Ushiriki wa Vijana katika
Maendeleo”.
Ujumbe
kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova katika kuadhimisha
siku hiyo na kusomwa kwa niaba yake na mwakilishi wa UNESCO nchini
Bokosha Spencer umesisitiza nguvu ya radio katika kujihusisha na masuala
ya kijamii kwa vijana wenye umri chini ya miaka 30, ambao ni zaidi ya
nusu ya idadi ya watu duniani .
Afisa
Habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma
Ledama akifurahi jambo na baadhi ya washiriki kutoka redio mbalimbali za
jamii wakati Mkuu wa Wilaya ya Arumeru akibariki ufunguzi wa
maadhimisho ya siku ya redio duniani yaliyofanyika jijini Arusha
mwishoni mwa wiki.
“Vijana
wanawake na wanaume hawashirikishwi vema katika vyombo vya habari -
hutengwa mara nyingi kunakoashiria kusahaulika kwa mapana yake katika
masuala ya kijamii, kiuchumi na kidemokrasia. Redio kama chombo cha
mshikamano, kinachokuza elimu na utamaduni ushirikishwaji wa vijana ni
muhimu”.
Bokova
aliitaka jamii kuwasaidia vijana kwa kuwapa sauti kubwa zaidi na
kujenga hisia ya jamii kwa njia ya usambazaji wa habari kwa kutayarisha
na kusikiliza vipindi vya redio.
Bw.
Spencer Bokosha akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya redio
duniani kwa niaba ya Mkuu wa ofisi ya Shirika la UNESCO, Tanzania
Zulmira Rodriguez.
Mwenyekiti
wa mkutano wa sherehe maadhimisho ya siku ya redio duniani ambaye pia
ni Meneja wa Maadili wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. Allan Lawa
akiendesha akitoa mada chokonozi ni kwa namna
gani radio inaweza kutumika kama jukwaa la ushiriki kwa vijana katika
mabadiliko ya kidemokrasia? Utafiti unaogusa Watanzania wakielekea
katika uchaguzi mkuu.
Mwandishi
mkongwe na mkufunzi wa tasinia ya habari kutoka chuo kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Ayub Rioba akitoa mada Je uwekaji huru wa mawimbi ya
radio kumesababisha mambo mabaya zaidi kuliko mazuri: Mitazamo na
matarajio kuhusiana na ushiriki wa vijana wakati wa sherehe za
maadhimisho ya siku ya redio duniani.
Makamu
Mwenyekiti wa mtandao wa redio za jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni
Meneja wa redio jamii Sengerema FM ya mkoani Mwanza Bw. Felician
Ncheye, akiwasilisha mada inayohusu ushiriki wa vijana katika vipindi
vya Redio, ambapo amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Redio za jamii
kuhakikisha zinawafikia watu wote kwenye jamii huku wakiwalenga vijana
ambao ndio wana idadi kubwa ambayo inaweza kuchochea mabadiliko ya
kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.
Meneja
wa Redio Kahama FM, Marco Mipawa akichangia mada ya kuonesha nguvu za
vijana na vyombo vya habari vya jamii pamoja na kujadili kanuni bora
zilizojitokeza katika utekelezaji wakati sherehe za maadhimisho ya siku
ya redio duniani zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha.
Mwandishi
wa habari mkongwe, mzee Gervas Moshilo akitoa mada ya Uandishi wenye
maadili na uwakilishi wa vijana kupitia vyombo vya habari wakati wa
sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani.
Meza kuu ikifuatilia mada na michango mbalimbali iliyokuwa ikitolewa na washiriki.
Pichani
juu na chini ni watangazaji wa redio za kijamii walioshiriki kwenye
sherehe za maadhimisho ya siku ya redio duniani wakichangia mada
mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment