TANGAZO


Wednesday, February 18, 2015

UN yataka juhudi zaidi kukabili mauaji ya Albino

DSC_0233
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza na binti wa miaka 19 ambaye ni mlemavu wa ngozi na kutosikia, Masalu Masuka ambaye  anaishi katika kituo cha watoto walemavu cha Buhangija baada ya kukimbia kwao Bariadi kukwepa wauaji wa albino. Binti huyo alijifungua mtoto wake akiwa kituoni hapo bila msaada wa muuguzi. 

Na Mwandishi wetu
MRATIBU wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, na Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Maendeleo la umoja huo (UNDP), Alvaro Rodriguez amehimiza serikali kuchukua hatua zaidi kukabili mauaji ya watu wenye albinism.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo kufuatia taarifa ya kutekwa na kuuawa kwa binti mwenye albinism wa umri wa mwaka mmoja, Yohana Bahati, alisema pamoja na juhudi zilizopo sasa za kukabili mauaji dhidi ya watu wenye albinism  lazima ziongezwe.

Maiti ya Yohana Bahati (1)  aliyetekwa Februri 15 mwaka huu imekutwa katika kijiji cha Shilabela Mapinduzi , kilomita chache kutoka nyumbani kwao Ilelema.

Mwili huo umekutwa na polisi katika hifadhi ya Biharamulo jana Februari 17, 2015 majira ya saa 9 alasiri huku ikiwa imenyofolewa miguu na mikono.

 Mama yake, Ester Jonas (30) bado hoi hospitalini Bugando akitibiwa majeraha yaliyotokana na mapanga wakati akijaribu kumuokoa mtoto wake.
DSC_0386
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiwa amembeba mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Ghoke Maliwa anayelelewa kwenye kituo cha Buhangija Jumuishi kilichopo mkoani Shinyanga alipofanya ziara ya kukitembelea kituo hicho hivi karibuni mkoani humo.

Aidha dada yake Tabu bahati (3) bado yuko katika ulinzi wa polisi wakati dada yao mkubwa Shida Bahati (12) akiwa kwa ndugu zake kijiji kingine.

Alisema katika taarifa yake kwamba katika kipindi cha miezi miwili Tanzania imeshuhudia kutekwa nyara kwa watoto wawili katika kanda ya ziwa.

Desemba mwaka jana mtoto Pendo alitekwa  na kusababisha kizaazaa kikubwa lakini pamoja na juhudi za kumtafuta  mtoto huyo mpaka leo hajulikani alipo.

Taarifa hiyo imesema kwamba Umoja wa Mataifa unasikitishwa na vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya watoto hao wawili.
 Mashambulio dhidi ya watu wenye albinism yanaelezwa kuwa yanasababishwa na imani za kishirikina na kwamba kutoka mwaka 2000 hadi sasa watu wenye albinism 74 wameshauawa.
“ Mashambulizi haya yanaambatana na ukatili mkubwa, na wakati serikali inafanya kila juhudi kukabili tatizo hili, juhudi kubwa zinastahili kufanywa ili kukomesha mauaji na  kulinda kundi hilo dogo la watu ambao wako katika hatari kubwa “ inasema sehemu ya taarifa hiyo.
DSC_0351
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akisoma ujumbe unaosema “DREAM BIG” kwenye T-shirt ya mtoto Agnes Kabika mwenye ulemavu wa ngozi anayelelewa kwenye kituo cha Buhangija Jumuishi alipofanya ziara ya kutembelea kituo hicho hivi karibuni.

Umoja wa Mataifa umesema kwamba mashambulio dhidi ya albino hayavumiliki, si halali kwa namna yoyote na yanaweza kukomeshwa.

Wakati taifa hili linaelekea katika uchaguzi, yapo madai kuwa maisha ya watu wenye albinism wako katika hatari kubwa.
Mratibu huyo amesema kwamba pamoja na kupongeza juhudi za serikali katika kukabiliana na wimbi hilo la mauaji hayo, Umoja wa Mataifa unataka Mamlaka husika kuhakikisha haki za raia zinalindwa na utawala wa sheria unazingatiwa.
“ Tunataka mwaka 2015 kuwa mwaka ambapo haki za Watanzania wote zitaheshimiwa wakiwemo albino” Taarifa imesisitiza.
Mratibu huyo wa umoja wa Mataifa  amesema kwamba amezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatma Mwassa na chama cha Maalbino nchini TAS.

Amesema Mkuu huyo wa mkoa alimhakikishia kwamba wanafanya kila linalowezekana kukomesha madhila dhidi ya maalbino, huku TAS ikitaka kuhakikisha kwamba huu  ni mwaka wa kukomesha mauaji.

Aidha Mratibu wa The Same Sun (UTSS) nchini, Vicky Ntetema, amemweleza mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa mashaka yake wakati taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu.

No comments:

Post a Comment