TANGAZO


Thursday, February 19, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd aufungua mkutano wa Siku mbili wa Kanda wa Changamoto za Ukuaji wa Miji, jijini Dar es Salaam

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa Kanda  unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjayo Mjini Dara es Salaamu. 
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Siku mbili unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif pamoja na Viongozi na washiriki wa Mkutano huo wakifuatilia mada inayohusu Miji inavyoweza kukuza uchumi iliyotolewa na Mtaalamu wa masuala ya Uchumi kutoka Sweden Dk. David Simon. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu (Uongozi Institute), Profesa Joseph Semboja wakielekea kwenye ukumbi wa Mikutano kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/2/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ujenzi wa nyumba za Mkopo pamoja na bei nafuu na kulengwa kwa wananchi wenye kipato cha kawaida katika maeneo ya Miji na vitongoji vyake ndio njia pekee itakayosaidia mfumo mzuri katika uwekaji wa mipango Miji.
Alisema ujenzi holela usiozingatia Mipango Miji unaoendelea kukua siku hadi siku katika maeneo ya miji hasa ile ya Jumuyia ya Afrika Mashariki mara nyingi huleta athari wakati yanapotokea mafuriko au majanga ya moto.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiufungua Mkutano wa Siku mbili wa kanda  unaozungumzia changamoto za ukuaji wa Miji pamoja na kushughulikia hali ya baadaye ya Miji ya  Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjayo Mjini Dara es salaamu.
Mkutano huo uliopewa jina la Maisha ya baadaye ya Nchi za Afrika Mashariki, jinsi gani tunataka kuishi mwaka 2050 umeandaliwa na Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu { UONGOZI INSTITUTE }.
Alisema asilimia kubwa ya wananchi wa kawaida huishi kwa kujenga makaazi yao kwenye maeneo hatarishi ambayo wakati yanapotokea maafa au mafuriko Wananchi hao wanashindwa kupata huduma muhimu za lazima kutokana na uharibifu wa mazingira na matokeo yake hukumbwa na miripuko ya maradhi yanayosababisha kupoteza idadi kubwa ya maisha ya watu.
Balozi Seif alizinasihi Taasisi, wataalamu na Viongozi wanaosimamia Mipango Miji kuelewa kwamba ili kufikia malengo ya maisha bora ya Jamii pamoja na kukuwa kwa miji bado ipo haja ya kuimarishwa miundo mbinu ya huduma muhimu za lazima katika Halmashauri za Mikoa, Wilaya na Vijiji ili kupunguza kasi ya ukuaji wa miji Mikubwa.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Afrika kwa Maendeleo endelevu { Uongozi Institute } Profesa Joseph Semboja alisema upo uwiano mkubwa wa ongezeko la watu Barani Afrika na Dunia kwa ujumla.
Profesa Semboja alisema ongezeko hilo linasababisha msongamano wa  shinikizo la uhaba wa makaazi ya watu , ufinyu wa fursa za ajira hasa kwa vijana pamoja na huduma za Kijamii.
Alisema ukanda wa Afrika Mashariki unaendelea kukumbwa na changamoto mbali mbali za tabia nchi, mazingira sambamba na ongezeko kubwa la idadi ya wakaazi wake katika Miji ya Nchi hizo.
“ Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi { UN Habitat } hali ya Miji ya Afrika 2014, Afrika Mashariki inashika nafasi ya chini katika Miji inayokuwa Duniani lakini ndio kanda inayoongoza katika kasi ya ukuaji wa Miji yake kwa sasa “. Alisema Profesa Semboja.
Alifahamisha kwamba ifikapo mwishoni mwa muongo huu wa sasa idadi ya wakaazi waishio Mijini itaongezeka kwa asilimia 50% na jumla ya idadi ya wakaazi wa mijini ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa mara tano ya mwaka 2012.
Profesa Semboja alieleza kwamba lengo la Mkutano huo wa kanda unaokutanisha Viongozi na watunga sera kutoka nchi za Afrika mashariki umelenga kujadili namna ya kutatua  changamoto hizo na kufikiria miji ambayo itatimiza matakwa yaliyokusudiwa.
Akitoa salamu za shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi { UN Habitat } Mwakilishi wa shirika hilo Dr. Remy Sietchiping alisema nguvu za Viongozi wa Kisiasa zitumike katika kusaidia Taaluma ya ujenzi wa Mipango Miji.
Dr. Remy alisema mipango hiyo lazima iende sambamba katika kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu.
Alifahamisha kwamba Shirika hilo la Habitat litahakikisha kwamba linatumia nguvu na uwezo wake katika kusaidia Taaluma ya upangaji wa Miji Barani Afrika.
Washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi za Burundi, Ethiopia,, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudani ya Kusini, Uganda na wenyeji Tanzania wengi wao ni watendaji wa ngazi za juu Serikalini, mshirika ya Kikanda na Kimataifa, Miji Mikubwa, wasomi, Sekta Binafsi na Taasisi za Kiraia.

No comments:

Post a Comment