TANGAZO


Monday, February 2, 2015

BUNGENI LEO MJINI DODOMA

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira James Lembeli akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Kamati yake kwa Kipindi cha Mwaka 2014, Bungeni mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Said Nkumba akiwasilisha taarifa ya kamati yake.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba akijibu maswali wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni leo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela akijibu maswali ya wabunge.
Baadhi ya Mawaziri wakiwa kwenye ukumbi wa Bunge jana.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Juma Nkamia Bungeni mjini Dodoma.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Diana Chilolo akiuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Katiba na Sheria kuhusu Mahakama ya Wilaya ya Iramba mkoni Singida.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola akichangia taarifa za kamati zilizowasilishwa leo Bungeni mjini Dodoma.
Baadhi ya wageni ambao ni wanafunzi wa Shule ya Awali ya Mchepuo wa Kiingerea ya Labi ya mkoni Dodoma wakiwa na walezi wao, wakifuatilia Bunge. (Picha zote na Lorietha Laurence-MAELEZO, Dodoma)
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Stephen Wassira (kulia) akijadili jambo na wabunge wenzake baada ya kuahirishwa kikao cha asubuhi Bungeni mjini Dodoma leo.Wengine kutoka kulia ni Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid akijadili jambo na Mbunge wa Kuteuliwa Margaret Sitta, nje ya ukumbu wa Bunge.
Naibu Waziri wa Fedha Adam Malima akizungumza na Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji baada ya Bunge kuahirishwa leo asubihi. (Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma)  

Mapambano dhidi ya ujangili nchini yaonesha mafanikio makubwa

Na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma
KAMATI ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imesema kuwa hatua za Serikali za kupambana na ujangili nchini zimeonesha mafanikio makubwa.

Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema kuwa pamoja na mafanikio mengine hatua hiyo imefanikiwa kukamata silaha 2000.

Alisema hadi kufikia mwaka 2013, hali ya ujangili wa tembo ilikadiriwa kufikia tembo 30 kwa siku, lakini Serikali ilichukua hatua ya kuzuia na kutokomeza uhalifu huo kwa kuanzisha Operesheni Tokomeza.
“Pamoja na madhara yalijitokeza operesheni hiyo ilisaidia kuanza kupungua kwa kesi za ujangili wa tembo nchini” alisema Lembeli.
Alifafanua kuwa baada ya Operesheni hiyo Serikali iliendelea kuchukua hatua zaidi kwa lengo la kutokomeza kabisa tatizo hilo.

“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuajiri askari wa wanyamapori zaidi ya 500 na wengine 300 waliajiriwa ikiwa ni askari wa kujitolea”alisema.
Hata hivyo aliishauri Serikali kuendelea na harakati za kupambana kwa nguvu zote na ujangili  na kuweka wazi hali ya ujangili nchini ili wananchi na wadau wa hifadhi nchini waungane na Serikali.

Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni ya simu inayotoza gharama za maunganisho zaidi ya zile zinazodhibitiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Naibu Waziri Makamba alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde lililotaka kujua kwa nini kampuni moja inawatangazia wananchi kutoza gharama walizotumia.
Alisema TCRA inasimama ipasavyo kudhibiti huduma za mawasiliano kulingana na sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na kudhibiti hujuma mbalimbali zinazofanywa na kampuni za simu.


Alifafanua kuwa katika kuimarisha udhibiti pamoja na hujuma hiyo, Kitengo Maalum kimeanzishwa ndani ya TCRA kinachoshughulika na malalamiko ya wateja yanayohusu huduma za mawasiliano.

Serikali kuondolewa wananchi changamoto za upatikanaji wa viza

Na Lorietha Laurence- Maelezo Dodoma
02/02/2015
SERIKALI ya Tanzania inafanya jitihada za kuhakikisha kuwa inaondoa usumbufu wa upatikanaji wa viza za Uingereza na nchi nyingine ili kupunguza changamoto zinazowakumba wananchi wakati wa kuomba viza hizo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim, wakati akijibu swali la mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Jaku Ayoub aliyetaka kujua kauli ya Serikali kwa wananchi wanaopata usumbufu wakati wa kuomba viza za Uingereza.

Alisema Wizara yake inaendelea kuzisihi nchi hizo kulegeza masharti yao ya viza kwa Watanzania ili wananchi wa Tanzania waendelee kufaidika na uhusiano mzuri uliopo.

Alitoa wito kwa  wananchi wenye dhamira ya kwenda Uingereza kufanya maombi ya viza mapema ili kuepuka usumbufu unaojitokeza pale wanapohitaji kusafiri.

Alibainisha kuwa Ubalozi wa Uingereza nchini  haujafungwa ingawa huduma za  viza  zinatolewa kupitia wakala ambapo utaratibu wa upatikanaji wake ni ndani ya siku 18.

 “Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu  kuwa, Serikali inaendelea kufanya jitihada kuhakikisha usumbufu wa upatikanaji wa viza za Uingereza na nchi nyingine unapungua kwa kiasi kikubwa” alisema Waziri Maalim.

Kuhusu mchango wa uamuzi wa Tanzania kuwa na Ubalozi nchini Uingereza, Naibu Waziri Maalim alisema uamuzi huo umesaidia kukuza uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza.

“Uhusiano ambao umetuwezesha kushirikiana katika nyanja za Elimu, Biashara, Utalii na Uwekezaji.
Wanafuzni wa Tanzania wamekuwa wakinufaika na ufadhili wa Serikali ya Uingereza katika mafunzo ya Elimu ya Juu hususani Shahada za Uzamili na Uzamivu” alisema.

Aliongeza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya Kidiplomasia na uchumi  inaendelea kutangaza fursa za uwekezaji  zilizopo nchini  ikizingatiwa kuwa Uingereza ni mdau mkubwa  katika kuchangia  bajeti ya taifa kupitia misaada mbalimbali wanayoitoa kupitia  umoja wa Ulaya.

No comments:

Post a Comment