TANGAZO


Thursday, January 29, 2015

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM SAIDI MECK SADIKI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WIKI YA SHERIA KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecki Sadiki akizungumza na waandishi wa habari.

Ndugu wananchi wa Mkoa wa
Dar es Salaam,
Nachukua fursa hii kuwaarifu kuhusu maadhimisho ya wiki ya Sheria itakayofanyika Mkoani Dar es Salaam na Kama mnavyofahamu Mahakama huadhimisha kila Mwaka siku ya Sheria ambayo huashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama katika Mwaka husika. Kwa Mwaka huu wa 2015, utaratibu wa kuadhimisha siku ya Sheria umebadilika. Badala ya kuadhimishwa siku moja, sasa imeonekana ni busara maadhimisho hayo yakatanguliwa na maonyesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mahakama kwa siku tano kabla ya maadhimisho ya kilele cha siku ya Sheria.

Ndugu wananchi,
Lengo la Maonyesho hayo ni kutoa fursa pana zaidi kwa wananchi kukifahamu chombo chao cha Mahakama na shughuli zake. Aidha, wananchi watapata fursa ya kuelimishwa juu ya mambo mbalimbali ya kisheria  na kujibiwa dukuduku zao hususani kwenye masuala ya kisheria na taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika ngazi mbalimbali za kimahakama

Ndugu wananchi,
Mwaka huu wa 2015 Wiki ya Sheria itaadhimishwa kuanzia tarehe 30/01/2015 kwa kufanya maonyesho katika Viwanja vya Mnazi Mmoja hadi tarehe 03/02/2015 na Kilele cha siku ya Sheria kitakuwa tarehe 04/02/2015 katika kiwanja cha Mahakama kilichopo Mtaa wa Chimala karibu na  Hospitali ya Saratani ya Taifa “Ocean Road”.

Ndugu wananchi,
Wiki ya Sheria itazinduliwa rasmi na Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya pili Mhe. Ally Hassan Mwinyi baada ya kuongoza matembezi ambayo yataanzia Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenda Mnazi Mmoja kupitia barabara za Serena - Ohio, Gymkhana – Obama , Ikulu, Mahakama ya Biashara, Kivukoni, Sokoine, Railway, Nkurumah, Lumumba, Mkunguni hadi Mnazi Mmoja, siku ya tarehe 01/02/2015 kuanzia saa 12.00 Asubuhi. Natoa wito kwa wananchi wa fani mbalimbali kujitokeza kwa wingi katika matembezi hayo.

Ndugu Wananchi,
Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa ya Jirani mnaombwa kujitokeza kwa wingi katika Maonesho yatakayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ili kupata maelekezo ya kina na yenye ufasaha  kuhusu shughuli za Mahakama ya Tanzania na utoaji wa haki kwa wakati.
Aidha, Napenda nitoe rai kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kuelekeza magari yao ya abiria kwenda Uwanja wa Mnazi Mmoja  ili kurahisisha usafiri kwa wananchi, na ninarudia kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kwenye Maonesho hayo kwani hii ni fursa pekee kwa wananchi kutambua haki zao za msingi kwa mujibu wa Sheria.

Asanteni kwa kunisikiliza.
Saidi Meck Sadiki
MKUU WA MKOA WA
DAR ES SALAAM
29/1/2015


No comments:

Post a Comment