TANGAZO


Friday, October 24, 2014

Prof. Tibaijuka: Magonjwa ya Mlipuko yatekelezwe Kimataifa


Na Anita Jonas-MAELEZO
Umoja wa Mataifa umeshauri  kuchukua  hatua za haraka kwa magongwa ya mlipuko yanayotokea Afrika kama Ebola kwani yanadhiri uchumi wa mataifa husika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka wakati wa Maadhimisho ya Miaka 69 ya Umoja wa Kimataifa leo Jijini Dar es Salaam.
Prof. Tibaijuka alisema kuwa Umoja wa Mataifa wanatakiwa kuchukua tahadhari ya milipuko ya magonjwa hatarishi na kuyachukulia kama ni magonjwa ya Kidunia kwani yanaathiri mifumo yote ya kimaendeleo.
“Mataifa yaliyoendelea yasingepuuzia mlipuko wa  ugonjwa wa Ebola ulipojitokeza  Afrika  hali isingekuwa  hatarishi kama ilivyo sasa, hivyo ni rai yangu kwa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na mataifa husika kuchukua  tahadhari wakati wote ”Alisema Prof. Tibaijuka.
Aidha, Prof. Tibaijuka alisema kuwa kutokana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi kuwa tishio miongoni mwa wengi duniani, wahisani wa maendeleo hawanabudi kusaidia Mataifa mengine ikiwamo utekelezaji wa Mfuko wa Kijani wa Hali ya hewa.
Akizungumzia kuhusu hatua ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete kutoa uraia kwa wakimbizi 162,000 kutoka Burundi, Prof. Tibaijuka alisema kuwa Tanzania imeonyesha ulimwengu kuwa suala la mapambano dhidi ya ukimbizi linaweza kufanyiwa kazi na kuwafanya wakimbizi kuishi maisha kama binadamu wengine.
Naye Mratibu muwakilishi wa makazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wamepanga kusaidia na kuboresha miundombinu ya kiusalama ili kuendeleza amani Duniani kwani bila amani maendeleo ni vigumu kupatikana.
Pia Bw. Rodriguez aliipongeza Tanzania katika kutekeleza Malengo ya Millenia katika sekta ya afya kwa ambapo asilimia 96 ya vituo vyote vya afya nchini vinatoa huduma ya afya ya uzazi kwa mama na mtoto.
Sherehe hizo zimebebwa na kauli mbiu ya “Leave no One Behind” ikiwa na mlengo wa kuleta maendeleo yenye usawa duniani.

No comments:

Post a Comment