Rais Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akisalimiana na Wauguzi
waliovalia mavazi maalumu tayari kutoa huduma kwa abiria atayekutwa
na ugonjwa wa Ebola mara atapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha zote Benedict Liwenga, Maelezo-DSM)
Baadhi ya Wahudumu wakiwa wakivalishana mavazi maalumu wa Wodi Maalumu
iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola iliyoko katika eneo la Hospitali ya
Temeke jijini Dar es Salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili toka kushoto) akiwaangalia
Wahudumu waliopata mafunzo maalumu ya kumhudumia mgonjwa wa Ebola wakati
alipokagua Wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola iliyoko
katika eneo la Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM
22/09/2014.
EBOLA ni ugonjwa unaosababishwa na
virusi vya homa ya hemoraji ikimaanisha ugonjwa
wa kumwagika damu bila kuganda (Viral
Haemorrhagic Fevers).
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, ugonjwa
huu ni hatari na unasababishwa na kirusi kiitwacho ebola kwani kirusi hicho ni
moja kati ya familia ya virusi watatu toka katika familia ya filoviridiae.
Kuna aina tano za kirusi cha ebola ambao
ni bundibugyo ebolavirus (BDBV), Zaire
Ebolavirus (EBOV), Reston Ebolavirus (RESTV), Sudan Ebolavirus (SUDV) na Tai
Forest Ebolavirus (TAFV).
Ni ugongwa unaoua kwa kasi na tafiti zinaonyesha kwamba katika
orodha ya watu 10 walioambukizwa na virusi vya ugonjwa huo, basi wastani kati
ya watano au tisa hufariki.
Aina hizo tatu za virusi, yaani BDBV,
EBOV na RESTV, ndiyo inayongoza kwa kusababisha mlipuko wa ugonjwa huo Barani
Afrika wakati aina nyingine za virusi hao wanapatikana katika nchi za Asia,
yaani Ufilipino na Thailand.
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa kwa
mara ya kwanza ugonjwa huu uliripotiwa kutokea mnamo mwaka 1976 katika nchi ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na taarifa zinaeleza kuwa hatari ya mgojwa
kupoteza maisha ni asilimia 90.
Tafiti zinaonyesha kuwa, kuwa Popo
wanaopenda kula matunda wanaeneza ugonjwa huo bila wao kuaathirika na katika
jamii yetu ugonjwa huo huweza kuambukizwa kutoka mtu mmoja mwenye maambukizi
kwenda kwa mwingine baada ya kugusana na damu au maji maji kupitia michubuko au
majeraha yaliyopo juu ya ngozi.
Pia watu ambao wako katika hatari ya
kupata ugonjwa huo ni jamii inayoishi karibu na jamii ya wanyama ambao mara
nyingi ni Nyani, Sokwe, Tumbili pamoja na Popo.
Licha ya watu walio na maambukizi ya
ugonjwa huo kapata nafuu, lakini bado wanaweza kuwaambukiza wengine kwa njia
mbalimbali, mfano kwa njia ya kujamiana.
Wataalam
wanaamini kuwa virusi vya ugonjwa huo huwa havienei kwa njia ya hewa bali kwa
mtu kugusana na majimaji ya mwili, kama vile matapishi, mate, jasho, machozi,
ama manii au shahawa ya mtu aliyeathirika na ugonjwa huo.
Kwa upande
mwingine hata Madaktari na wauguzi, wanaowatunza wagonjwa wa ebola, watu wenye
uhusiano wa karibu na mtu aliyeambukizwa, watu wanaogusa maiti ya mtu mwenye
virusi hivyo wapo katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Ebola.
Ishara na dalili muhimu ya ugonjwa huu ni hali ya kutokwa na damu
katika sehemu tofauti za mwili kama vile katika ufizi, pua, katika njia ya haja,
lakini kabla mgonjwa hajafikia daraja hilo, kwanza mtu huwa na homa kali,
viwango vya joto vya mwili hupanda sana, kisha anaweza kuwa anajisikia
kutapika, na hata kutapika kwenyewe, kuharisha, na pia kuwa mnyonge huku viungo
vyake vikiwa na maumivu.
Ili kuweza kutambua mtu ama mgonjwa ameambukizwa na ugonjwa huo, njia
ya pekee ya kuthibitisha hilo ni kupitia vipimo vya maabara.
Huduma ya kwanza ambayo mgonjwa wa Ebola anaweza kupewa kwanza
kabisa ni vema kumfikisha mgonjwa huyo katika Kituo cha Afya haraka kwa haraka
kwani kuvigundua virusi vya ebola kunahitaji maabara ambayo ina uwezo wa
kutosha.
Katika
kuzingatia matibabu ya mgonjwa wa Ebola jambo la kwanza ni kuchunguza na
kuhakikisha kwamba mtu ana virusi hivyo, pili ni kumtenga na watu wengine ili
yeye mwenyewe asidhurike zaidi na asiwadhuru wengine na katika kufanya hivyo
haimaanishi kwamba mgonjwa huyo anatengwa kwa kunyanyapaliwa, lengo ni kuepusha
maambukizi yasiendelee kwa watu wengine ambao hawana ugonjwa huo.
Taarifa
nyingi kuhusiana na ugonjwa huu zinasema kuwa mpaka sasa hakuna dawa maalumu
ambayo inatumika kuwatibu wale walio na virusi vya ugonjwa huo kwani dawa
zilizoko sasa ni zile ambazo ziko ngazi ya majaribio ili kuweza kuona namna
gani zinaweza kukabiliana na ugonjwa huo.
Shirika la
Afya Duniani (WHO) lilitoa kauli ya kwamba hatari ya kuambukizwa kwa ugonjwa
huo kwa njia ya safari za ndege ni chini sana, hata hivyo, watu hushauriwa kuwa
waangalifu kuhusiana na hali yao na afya na ile ya wasafiri wengine.
Tahadhari ni
bora kuliko kinga, ili kujihadhari na ugonjwa huo endapo utakuwa umeonekana
kuingia nchini mwetu hatunabudi kujiepusha kugusana na majimaji yote yanayotoka
kwenye mwili wa mtu ambaye atakuwa ameathirika na ugonjwa huo, na pia ni vema
tukatumia dawa za kuuwa vijidudu katika choo, katika matapishi, katika mate na
majimaji yoyote ya mgonjwa.
Bila shaka ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika endapo
tu sote tutachukua hatua, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuwajibika katika hili
na kutoa taarifa mapema kwa Viongozi wa Serikali na wa huduma za Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizochukua
tahadhadhari kubwa na mapema ingawa hakuna kesi yoyote iliyoripotiwa juu ya uwepo
wa ugonjwa huo hapa nchini.
Kwa kuanzisha mafunzo maalum kwa Kikosi Kazi yenye lengo la kudhibiti
ugonjwa wa Ebola, Serikali imetoa mafunzo kwa mamia ya Watumishi wa Afya
watakaokwenda kuhudumia abiria wanaoingia na kutoka nje ya nchi.
Sambamba na
hilo, Serikali imeweza kufanikisha kuingiza nchini sehemu ya vifaa vya kubaini
hatua za awali za ugonjwa wa Ebola kwa kupima hali ya joto la mwili kwa
wasafiri kutoka nje nchi wanaotumia viwanja vya ndege vilivyokuwa
vimeagizwa na Serikali vilikwisha wasili jijini Dar es Salaam.
Vifaa hivyo
vinavyohusisha kamera zenye uwezo wa kubaini joto la mwili wa msafiri kwa
umbali wa mita 100 bila kumgusa muhusika ambayo viliagizwa kutoka nchini Afrika
ya Kusini.
Wakati wa siku
ya kukabidhi vifaa hivyo kwa Wataalam wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Kebwe Steven Kebwe alisema kuwa
kuwasili kwa vifaa hivyo ni moja ya juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa wananchi
wanakuwa salama kwa kuuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.
Aidha alisema
kuwa vifaa hivyo vitapelekwa katika maeneo ya Viwanja vya ndege na maeneo
yanayotumiwa na raia wa kigeni kuingia nchini vikiwemo vya Dar es Salaam,
Zanzibar, Kilimanjaro, Mbeya na Mwanza.
Licha ya kuwepo
kwa juhudi hizo, bado Serikali inaendelea na mpango wa kuagiza vifaa zaidi vya
kuwezesha shughuli ya upimaji wa afya kwa wasafiri wanaotembea yaani vifaa vya (Scanners) vitakavyowezesha kubaini afya
za wasafiri wengi zaidi kwa wakati mmoja.
Aidha,
aliwataka wataalam wa afya kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa kwa kuhakikisha
wanawapima abiria wote wanaotoka nje ya nchi bila kujali hadhi walizonazo ili
kuweza kubaini kama wana maabukizi au dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.
“Nataka mfanye
kazi yenu kwa kuzingatia weledi wa taaluma yenu na kwa kuzingatia yale
mliyojifunza, mvitumie vifaa hivi kupima kila abiria ili kubaini joto lake bila
kujali cheo wala hadhi yake maana janga hili ni kubwa” Alisema Dkt. Kebwe.
Akizungumzia
kuhusu matunzo ya vifaa hivyo, aliwataka wataalam hao kuhakikisha wanavitunza
vifaa hivyo ili viweze kudumu na kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kuwasaidia
wananchi kutokana na vifaa hivyo kugharimu fedha nyingi.
Katika hatua
nyingine Mh. Kebwe alifafanua kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendelea
na shughuli ya utoaji wa Elimu ya Afya kuhusu ugonjwa wa huo ili kuwawezesha
wananchi kuchukua tahadhari na kuzielewa dalili za ugonjwa huo na namna ya
kujingika endapo utagundulika nchini.
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Bw. Cosmas Mwaifwani ambaye Ofisi
yake ilihusika katika uagizaji wa vifaa hivyo alisema kuwa mahitaji ya vifaa
hivyo kwa sasa yameongezeka kutokana na umuhimu wake na jinsi vinavyofanya kazi
kwa ufanisi mkubwa.
Alisema kuwa upimaji
kwa kutumia vifaa hivyo unatumia teknolojia ya kubaini mionzi ya joto kutoka
katika mwili wa binadamu pindi vinapoelekezwa katika maeneo ya macho na masikio
ya mwili wa binadamu.
“Vifaa hivi
vinauwezo wa kutunza picha na kumbukumbu za msafiri, muda, joto la msafiri na
tarehe aliyoingia nchini na vifaa hivi vina uwezo wa kupata takwimu kutoka
kwenye hali ya majimaji au jasho la Binadamu pindi kinapoelekezwa kwake”,
alisema Mwaifwani.
Mwaifwani aliongeza
kuwa MSD inaendelea kuimarisha uwezo wake kwa kuongeza vifaa zaidi kutoka nchi
za Ubelgiji na China huku akisisitiza kuwa Bohari hiyo imejiandaa kukabiliana
na ugonjwa wa Ebola kwa kujenga uwezo wa kuwa na dawa za kutibu hali ya
magonjwa yanayoambatana na homa hiyo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege nchini, Bw. Moses Malaki akizungumza kwa niaba
ya Viwanja vya ndege nchini alielezea hali hiyo ya upatikanaji wa vifaa
katika maeneo hayo kuwa itaongeza ufanisi wa uchunguzi wa afya kwa wasafiri na
kuondoa usumbufu kutokana na uwezo wa vifaa hivyo kumpima msafiri akiwa mbali.
Pamoja na juhudi za serikali katika kuzuia usiingie nchini ugonjwa
huo na hali ya kukaa kwa tahadhari, jamii nchini hainabudi kuzingatia elimu
itolewayo na wataalam wa afya juu ya namna ya kujikinga ili kuweza kuudhibiti
vema ugonjwa huo kwani mpaka hivi sasa tayari Shirika la Afya Duniani (WHO)
limetangaza kuwa zaidi ya watu 560 wamepoteza maisha nchini Sierra Leone na wengine
zaidi 2,600 wamefariki dunia huko Afrika ya Magharibi.
No comments:
Post a Comment