*Udhibiti Viwanja vya Ndege na mipakani waimarishwa
Mtaalam wa ufuatiliaji wa magonjwa
ya binadamu wa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Vida Mmbaga akitoa ufafanuzi kuhusu historia ya ugonjwa
wa Ebola, Virusi vyake , dalili na namna unavyoenea wakati wa mafunzo maalum
kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Aron Msigwa –MAELEZO)Mtaalam wa ufuatiliaji wa magonjwa ya binadamu wa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Vida Mmbaga akitoa ufafanuzi kuhusu historia ya ugonjwa wa Ebola, Virusi vyake , dalili na namna unavyoenea wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Binadamu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Janeth Mghamba akifungua wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa ugonjwa wa Ebola jijini Dar es Salaam.
Ofisa Afya Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anayeshughulikia
maeneo ya Bandari, Viwanja vya ndege na mipakani Dkt. Chacha Mung’aho akizungumza namna walivyojipanga kukabiliana
na tishio la ugonjwa wa Ebola kupitia
wasafiri wanaoingia nchini Tanzania.
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
17/8/2014. Dar es Salaam.
IMEELEZWA kuwa Tanzania
kwa sasa haina raia yeyote aliyeingia nchini kutoka mataifa mengine aliyebainika
kuwa na maabukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Ebola kufuatia zoezi linaloendelea la
uchunguzi wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege na maeneo
mengine.
Hayo yamebainishwa kwa
nyakati tofauti na wataalam wa ufuatiliaji wa magonjwa ya binadamu wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii wanaoshughulikia magonjwa ya milipuko wakati wa mafunzo
kuhusu ugonjwa wa Ebola kwa waandishi wa
habari jijini Dar es salaam.
Wamesema kuwa ugonjwa
huo licha ya kuleta madhara na maafa makubwa katika maeneo ya nchi za Afrika
Magharibi kama zinavyoonyesha taarifa za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa
(WHO) bado haujaingia nchini Tanzania na kuongeza kuwa tayari Serikali kupitia
wizara ya Afya imechukua hatua za
udhibiti kupitia timu ya wataalam wa
afya walio katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Chacha Mung’aho ambaye
ni Afisa Afya Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anayeshughulikia
maeneo ya Bandari, Viwanja vya ndege na mipakani akizungumzia namna
walivyojipanga kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola kupitia wasafiri wanaoingia nchini Tanzania amesema
kuwa tayari Serikali imetenga maeneo
maalum, vifaa vya uchunguzi na huduma kwa wasafiri watakaobainika kuwa na
dalili za maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa wataalam
waliopo kutoka Wizara ya Afya wanaendelea
kushirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Uhamiaji na
Wizara ya Kilimo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuendesha zoezi la
uchunguzi wa afya ili kupata taarifa za wasafiri kulingana na mataifa
wanayotoka.
“Kwa sasa tunafanya
kazi kwa kushirikiana na tunapata taarifa sahihi za abiria kutoka kwa mashirika
ya ndege wanayotumia kusafiria jambo linalotusaidia kuwabaini wasafiri
waliotoka katika nchi za Liberia, Ivory Coast na Guinea zilizoathiriwa na
ugonjwa huo” Amebainisha Dkt. Chacha.
Amesema tangu kugunduliwa
kwa ugonjwa huo mwezi Machi mwaka huu huko Afrika Magharibi mataifa mbalimbali duniani kote yamekuwa katika
mapambano kudhibiti ugonjwa huo kuendelea kusambaa na kuleta maafa katika
maeneo mengine duniani ambako haujafika.
Naye Dkt. Vida Mmbaga
akitoa ufafanuzi kuhusu historia ya ugonjwa wa Ebola, Virusi vyake , dalili na
kuenea kwake amesema kuwa kwa mara ya kwanza uligunduliwa mwaka 1976 nchini Zaire
maeneo ya mto Ebola ukihusishwa binadamu kula nyama ya wanyama jamii ya Sokwe,
Nyani na Popo.
Amesema kuwa katika
nchi za Afrika ya Magharibi ambako sasa ugonjwa huo umeshika kasi chanzo kimetajwa
kuwa ni binadamu kula nyama ya wanyama jamii ya Sokwe na Popo huku wengine
wakiambukizana kupitia kugusana na mgonjwa, majimaji, kushika damu ya mgonjwa,
mate, mavazi au mwili wa mtu aliyekufa kwa Ebola.
Kuhusu kipindi cha
mgonjwa kuanza kuonyesha dalili za kuambukizwa ugonjwa huo kinaazia siku ya 2
hadi ya 21 na kufafanua kuwa dalili hizo huambatana na kutokwa na damu zehemu
za wazi, maumivu makali ya mwili na kichwa na kuongeza kuwa mgonjwa asipopatiwa
tiba ya dalili hizo mapema hupoteza maisha.
Amesema serikali
kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya
habari juu ya namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari na endapo watabaini uwepo wa mtu mwenye dalili za
Ebola pia kuratibu mipango yote ya vifaa tiba,matibabu na mazishi endapo
ugonjwa huo utaingia nchini kupitia kamati ya maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu .
Aidha, amesema licha ya
ugonjwa huo kuibuka na kupotea katika vipindi tofauti katika mataifa mengine ya
bara la Afrika na nchi jirani za Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda, wataalam hapa nchini wanaendelea kufanya
utafiti juu ya chanzo kinachohifadhi Virusi hao kutokana na tabia yao ya
kupotea katika kipindi fulani na kuibuka tena.
No comments:
Post a Comment