TANGAZO


Tuesday, August 19, 2014

Sekta ya Elimu yapokea Bil. 203 kutoka Benki ya Dunia






Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Bw. Likwelile akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati wa kusaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu, Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Philippe Dongier.





Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Sifuni Mchome akifafanua jambo wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia kuisaidia sekta ya Elimu nchini, Dar es Salaam leo. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius B. Likwelile na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi, Bw. Philippe Dongier.





Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Dk. Deo Mtasiwa akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu, Dar es Salaam leo. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Sifuni Mchome.



Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Dk. Deo Mtasiwa (kushoto), akizungumza wakati wa hafla hiyo. Wapili ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Sifuni Mchome, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Servacius B. Likwelile (wapili kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi, Bw. Philippe Dongier. (Picha zote na Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini – WHVUM)



Na Rose Masaka - MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imesaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu wa shilingi bilioni 203 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu katika mpango wake wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Mkataba huo umesainiwa na Katibu mkuu wa wizara ya fedha Dk. Servacus Likwelile huku ukiwashirikisha  Katibu Mkuu wa Wizara ya Elinu na Naibu Katibu Mkuu kutoka TAMISEMI leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya kusaini mkataba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dk. Servacus Likwelile ameishukuru Benki ya Dunia kutoa mchango huo kusaidia sekta ya elimu nchini na kuwataka TAMISEMI na Wizara ya Elimu kusimamia vizuri pesa hizo ili kuleta mafanikio zaidi kufikia malengo ya matokeo makubwa sasa.
Aidha Dk. Likwelile amewataka waajiri wote katika sekta ya elimu kutoa kipaumbele kwa walimu ili waweze kuboresha elimu nchini na kuwataka kupeleka majina na akaunti namba za walimu wote Hazina ili Hazina iweze kuwawekea mishahara yao katika akaunti zao kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome amesema kuwa Wizara ya Elimu kwa sasa imepiga hatua kubwa katika kufanikisha lengo la matokeo makubwa sasa linalolenga kukuza na kuendeleza elimu katika ngazi ya shule za msingi na sekondari hivyo fedha hizo zinatumika kutatua matatizo katika sekta ya elimu ambapo kwa sasa shule nyingi zimeanza kuonesha matokeo mazuri.
Akitoa mchango wake wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Philippe Dongier amesema kuwa  Benki ya Dunia imeona kuna umuhimu wa kuisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ili kuleta ujuzi na kuvumbua vipaji kwa vijana wadogo  watakaosaidia kuleta maendeleo hapo baadae.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI Dk. Deo Mtasiwa ameahidi kusimamia fedha hizo kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa zinawafikia walengwa wote hadi ngazi ya chini waweze kufaidika na pesa hizo.

No comments:

Post a Comment