Mkurugenzi Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano
toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Bw. Cosmas Mwaisobwa akiongea
na waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu maandalizi ya utoaji mikopo kwa
mwaka wa masomo 2014/2015, wakati wa mkutano uliofanyika leo, jijini Dar es
Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi
Kawawa.
Baadhi ya Waaandishi wa Habari wakimsikiliza
Mkurugenzi Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano toka Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu Bw. Cosmas Mwaisobwa wakati wa mkutano uliofanyika
leo Jijini Dar es Salaam.
1.0
MAANDALIZI YA UTOAJI MKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2014/2015
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitangaza
mwongozo na vigezo vya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 kupitia magazeti na tovuti yake mnamo wezi Aprili 2014. Mwongozo
huo, pamoja na mambo mengine, uliainisha sifa za waombaji mikopo na ruzuku, vipengele
vya Mikopo, programu za vipaumbele kwa waombaji wa shahada ya kwanza, shahada
za uzamili na uzamivu waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu zinazotambulika.
Maombi ya mikopo kwa waombaji wapya yalifanyika kwa njia ya mtandao kwa anuani
ya http://olas.heslb.go.tz
au kupitia anuani ya tovuti ya Bodi ya Mikopo ambayo ni: www.heslb.go.tz.
Kulingana na Mwongozo wa Utoaji Mikopo na Ruzuku kwa
mwaka wa masomo 2014/2015, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
ilifungua maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao (OLAS) kuanzia Aprili 23, 2014 na kuendelea kupokea
maombi hayo hadi Julai 31, 2014.
Mabadiliko machache yamefanyika, kubwa likiwa ni kwa wanufaika
wanaoendelea na masomo, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita, hawakutakiwa
kujaza tena fomu kuthibitisha uhitaji wao wa mikopo kwa mwaka unaofuatia,
isipokuwa kwa wale ambao waliopenda kusitisha kuendelea kupokea mkopo kutoka
Bodi. Wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo wataendelea kupata mikopo yao
kulingana na viwango walivyopangiwa awali.
1.1
Maombi yaliyopokelewa
Jumla ya maombi 58,037
yalikuwa yamepokelewa hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2014. Kati ya maombi hayo, jumla ya maombi 37,689 ni ya waombaji wa kiume na
maombi 19,592 ni ya waombaji wa kike. Uchambuzi zaidi wa waombaji wa mikopo unaonyesha
kuwa Waombaji wa kundi la diploma ya ualimu wa sayansi ni 480 (Me – 324, Ke – 156), Waombaji wa shahada ya uzamili/uzamivu (kwa
vyuo vya ndani ya nchi) ni 276 (Me –
194, Ke – 82), Waombaji wa shahada ya kwanza (kwa vyuo vya ndani ya nchi) ni 56,922 (Me – 37,460, Ke – 19,462),
Waombaji wa shahada ya uzamili/uzamivu (nje ya nchi) ni 126 (Me- 88, Ke – 38) na Waombaji wa shahada ya kwanza (nje ya
nchi) ni 233 (Me – 141, Ke – 92).
1.2 Uchambuzi wa Maombi
Baada ya kufungwa rasmi kwa kipindi cha kupokea maombi ya
mikopo, hatua inayoendelea kwa sasa ni uhakiki (verification) wa taarifa za waombaji,
kwa kuzipitia nyaraka mbalimbali zilizoambatanishwa na waombaji mikopo ambazo
ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya taaluma, vielelezo vya mdhamini, saini ya
mwombaji na mdhamini wake na ushuhuda wa Mwanasheria au Hakimu kwamba vivuli
vya nyaraka zilizowasilishwa kwenye Bodi ni halisi.
1.3 Upangaji wa mikopo
Mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo utakamilika
baada ya majina ya wanafunzi waliodahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU)
kujiunga na vyuo mbalimbali yanapowasilishwa rasmi kwenye Bodi ya Mikopo.
Udahili wa wanafunzi unafanywa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwa mfumo wa pamoja
wa udahili (CAS) unaotumiwa na vyuo takribani vyote vya elimu ya juu nchini. Kwa
vyuo ambavyo havimo katika mfumo wa pamoja wa udahili (CAS) hutuma TCU majina
ya wanafunzi ambao vimewadahili ili waweze kuthibitishwa kabla ya kupatiwa
mikopo. Taarifa za udahili ni muhimu
katika zoezi la upangaji wa mikopo kwa kuwa zinatoa mwongozo wa gharama halisi
za programu za mafunzo. Wanafunzi wanaostahili na waliotimiza masharti na
vigezo vya ukopeshaji ndio hupangiwa mikopo kulingana na bajeti iliyotengwa na Serikali.
1.4 Kutangazwa
kwa majina ya wanafunzi waliopata mikopo
Majina ya wanafunzi waliopata mikopo kulingana na udahili
yatatangazwa kwenye tovuti ya Bodi na taarifa hiyo pia itatangazwa katika
vyombo vya habari ili kuwataarifu wadau wote ikiwa ni pamoja na wanafunzi, vyuo
vya elimu ya juu, wazazi na umma kwa ujumla. Nakala za majina ya wanafunzi
waliopangiwa mikopo zitatumwa kwenye vyuo husika.
2.0
WANAFUNZI WA MASOMO YA STASHAHADA YA UALIMU
Kwa
kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi na kukabiliana na upungufu
wa
walimu wa masomo hayo katika ngazi ya shule za
Msingi na Sekondari, mwaka huu serikali imetoa fursa ya mikopo kwa
wanafunzi watakaojiunga na masomo ya Stashahada maalum ya Ualimu wa masomo ya
Sayansi na Hisabati.
Wanafunzi wapatao 5,000
wanatarajiwa kujiunga na Stashahada hii maalum katika Chuo Kikuu cha Dodoma na
wote watanufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
3.0
HITIMISHO
Kwa Taarifa hii, Bodi inapenda kuwataarifu wadau wote
kuwa mchakato wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 unaendelea vema.
Aidha, Bodi inawasisitizia waombaji wa Mikopo,
wazazi/walezi na umma kwa ujumla kutambua kuwa Mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya
juu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Uchangiaji wa Elimu ya juu na hivyo
iwapo kuna waombaji wanaoweza kujigharamia, wasiombe mikopo ili kutoa nafasi
kwa wahitaji wengi zaidi kunufaika.
Imetolewa
na:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA
ELIMU YA JUU
No comments:
Post a Comment