1.0 UTANGULIZI
Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza
kukutana tarehe 28 Aprili hadi tarehe 4 Mei 2014 Jijini Dar es Salaam, kutekeleza
Majukumu yake, kabla ya Mkutano wa Bunge Bajeti uliopangwa kuanza mjini Dodoma tarehe
6 Mei na kudumu hadi tarehe 27 Juni, 2014.
Kwa kawaida, Kamati za Kudumu za
Bunge hupaswa hukutana wiki mbili kabla ya Mkutano wa Bunge, ama Dar es Salaam,
Dodoma au Zanzibar kuendana na matakwa ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la
Aprili 2013.
Hivyo, Wabunge wote wanapaswa kuwa
wamewasili jijini Dar es Salaam ifikapo Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 tayari
kwa kuanza vikao siku ya Jumatatu tarehe 28 Aprili, 2014.
2.0 SHUGHULI ZITAKAZOTEKELEZWA
Wakati wa vikao vya Kamati, zitatekelezwa kazi
zifuatazo:-
2.1 Siku ya Jumatatu na Jumanne Tarehe 28 na 29 Aprili, 2014 Kamati zote za sekta pamoja na majukumu mengine, zitapitia
masuala yote yaliyojitokeza wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya Maendeleo
2.2 Siku ya Jumatano tarehe 30 Aprili, 2014 Wabunge
wote kwa ujumla wao watakutana katika Ukumbi wa Julius Kambarage Nyerere
kupokea Mapendekezo ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali ya
2014/2015 kwa mujibu ya matakwa ya Kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge
Toleo la 2013. Baada ya shughuli hiyo, Kamati zote za Kisekta zitaendelea na
uchambuzi wa Bajeti kuanzia tarehe 1 hadi 4 Mei, 2014
2.3 Kamati zisizo za kisekta zikiwemo Kamati
ya Bajeti, Kamati ya Masuala ya UKIMWI, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitaendelea na utekelezaji wa
Majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la
2013.
2.4 Tofauti na kamati nyingine, Kamati ya
Serikali za Mitaa na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitaanza kazi
zake mapema ambapo zitatakiwa kuwasili Dar es Salaam tarehe 25 April na kuanza
kazi zake tarehe 26 Aprili, 2014
3.0 SHUGHULI NYINGINE
Shughuli za Kamati zitamalizika
tarehe 4 Mei, 2014 Jijini Dar es Salaam ambapo Mkutano wa Bunge wa Bajeti
utaanza tarehe 6 Mei, 2014 Mjini Dodoma na unategemewa kumalizika tarehe 27
Juni, 2014.
Aidha, Bunge linatarajiwa kupitisha Mapendekezo
kwamba Bunge liwe likikutana kuanzia saa Tatu Asubuhi hadi saa Saba Mchana kila
siku na kisha kuendelea Jioni saa Kumi hadi saa Mbili Usiku ikiwa ni pamoja na
Siku za Jumamosi.
Hata hivyo, siku ya Ijumaa Bunge
litakutana kuanzia saa Tatu asubuhi hadi saa Sita Mchana na kuendelea saa kumi
Jioni hadi saa Mbili Usiku. Utaratibu huu ukiafikiwa utawezesha muda wa
kujadili Bajeti kuongezeka zaidi licha ya siku kupungua
Ratiba za shughuli za Kamati zote zitapatikana
kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz
Imetolewa na:
Idara ya
Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya
Bunge
DODOMA
25 Aprili 2014
No comments:
Post a Comment