Baadhi ya waandishi wa Habari waliohudhuria Mkutano
wa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa
Hawa Ghasia, Katika Ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es
Salaam. (Picha zote na Hassan Silayo)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu Mikakati Madhubuti ya ukusanyaji mapato na Matumizi bora ya
fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Mikoa na
Halmashauri zote nchini, wakati wa Mkutano na waandishi a habari leo, jijini Dar
es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene.
Baadhi ya waandishi wa Habari waliohudhuria Mkutano wa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa Hawa Ghasia, ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), leo jijini Dar es Salaam.
Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI imesema itaendelea kuboresha Sekta ya elimu nchini ili kuongeza wataalamu watakaosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa Mh. Hawa Ghasia wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Waziri Ghasia alisema kuwa baada ya Serikali kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini kukamilisha ujenzi wa shule za kata hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa shule hizo zinakuwa na vitabu, maabara za kisasa pamoja na walimu wakutosha.
Akifafanua zaidi alisema shule kongwe za Sekondari nchini ni miongoni mwa shule zitakazoboreshwa ili kutoa wanafunzi wenye ubora na uwezo ili kulisaidia taifa katika siku za usoni kuwa na wataalamu wakutosha katika maeneo yote yatakayosaidia kuwaletea wananchi maendeleo.
Pia Waziri Ghasia alieleza kuwa maboresho hayo yanakwenda sambamba na kuongeza idadi ya vyuo vya Elimu ya kati na vile vya Elimu ya juu .
Katika kutekeleza mpango wa kuboresha elimu Waziri Ghasia amesema kila Mtendaji katika Mkoa na halmashauri zote nchini anatakiwa kusimamia vyema utekelezaji wa mpango huo ili kuinua kiwango cha elimu na wale watakaoshindwa Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu.
Katika Hatua nyingine Waziri Ghasia amesema Serikali itahakikisha kuwa mfumo mpya wa ukusanyaji mapato katika Halmashauri zote nchini unafungwa kufikia mwaka 2015/16 ili kusaidia kuongeza mapato na kuboresha huduma za jamii kama hosipitali, Elimu na maji.
Alitaja Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kuwa miongoni mwa halmashauri zilizokwisha anza kutumia mfumo wa kielektroniki katika kukusanya mapato yake ambapo mfumo huo unaainisha vyanzo vyote vya mapato katika eneo husika hivyo kurahisisha ukusanyaji wa mapatao hayo.
Akifafanua zaidi alibainisha kuwa kufuatia maboresho yanayoendelea Kufanywa na Serikali hati safi katika Halmashauri zimeongezeka kutoka halmashauri 53 za mwaka 2005/2006 hadi Halmashauri 104 za mwaka 2011/12.
Pia Serikali Imeendelea kuchukua hatua za kinidhamu na Kisheria kwa watumishi wachache waliobainika kujihusisha na ufujaji wa mali za umma ambapo hadi Septemba, 2013 jumla ya wakurugenzi 53, Wakuu wa Idara 65 na watumishi 749 walichukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma.





No comments:
Post a Comment