TANGAZO


Monday, February 10, 2014

Ushindi wa Udiwani, CCM Iringa yatuma salam kwa Mbunge Msigwa wa chadema

Wafuasi wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Nduli, Jimbo la Iringa mjini, wakiwa wamemnyanyua juu Diwani mteule wa kata hiyo, Bashir Mtove baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa kata hiyo, dhidi ya mpinzani wake Ayub Mwenda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uliofanyika jana. (Picha na Francis Godwin Blog)

Na Francis Godwin, Iringa 
KUFUATIA  ushindi wa uchaguzi mdogo  wa udiwani Kata  zote  tatu  Mkoa  wa Iringa ikiwemo kata ya Nduli jimbo la Iringa mjini, Chama  Cha mapinduzi (CCM), Wilaya ya Iringa mjini kimetuma salam kwa Mbunge wa jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kuwa aanze safari ya kufungasha  virago katika jimbo hilo, ili 2015 akabidhi jimbo CCM.

Kaimu  Katibu  wa CCM, Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga  ambaye  pia ni Kaimu Katibu  wa CCM mkoa  huo, akikaimu nafasi ya  aliyekuwa katibu  wa CCM mkoa marehemu Emmanuel Mteming'ombe alisema kuwa ameletwa mkoani Iringa kwa kazi moja pekee ya kuhakikisha mbunge wa jimbo  hilo mchungaji Msigwa anaondoka madarakani  kwa kukabidhi jimbo hilo kwa CCM mwaka 2015 kama  alivyokabidhiwa mwaka 2010 .

Alisema kasoro  zilizojitokeza mwaka 2010 kwa CCM asitegemee  zitajirudia  tena na  kuwa wamejifunza vya kutosha na  kuwa hata  wana Iringa  waliotegemea makubwa  kutoka kwa mbunge Msigwa  wameishia kushuhudia vurugu  zisizo na mwisho  za Chadema .

Mtenga  alitoa kauli  hiyo  wakati  akiwashukuru  wana  Nduli , Ibumi na Ukumbi kwa  kukiwezesha  chama  cha  CCM kuibuka na ushindi  wa kishindo na  kukionyesha Chadema kuwa mahitaji ya  wana Iringa si Helkopta bali ni maendeleo  na  sera  safi  na  si sera  za vurugu na maandamano.

Huku  mwenyekiti wa CCM mkoa  wa Iringa Jesca Msambatavangu akisema  kuwa mwendo  huo ambao  CCM imeanza  nao katika chaguzi hizo ni mwendo ambao  kitakwenda nacho  hadi  katika  uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2015.

Msambatavangu  alisema  kuwa wananchi  wa mkoa  wa Iringa wamepata  kukionyesha Chadema  kuwa mahitaji  yao  si Helkopta   wala vurugu  ambazo  Chadema wamekuwa wakizifanya  hivyo kushindwa  vibaya kwa Chadema ni fundisho kubwa  na ushahidi wa kweli kuwa  CCM bado itaendelea  kubaki madarakani.

Alisema  kuwa kitendo cha Chadema  kutumia mamilioni ya  shilingi kwa  kukodisha Helkopta tatu na kupata kata  tatu na kuambulia patupu mkoani Iringa ni aibu kubwa ni wazi hata  mbunge  wao Msigwa wananchi  wa jimbo la Iringa mjini  wameonyesha kumchoka.

Mkoa Iringa kata tatu ikiwemo ya Nduli, Mjini Iringa na Ukumbi na Ibumu wilayani Kilolo zilishiriki uchaguzi huo ikiwa ni matokeo ya waliokuwa madiwani wake, wote kupitia CCM kwa nyakati tofauti kufariki dunia.

Katika chaguzi hizo Chadema ilionekana kuwekeza nguvu iliyoshereheshwa na viongozi wake wa kitaifa kwa kupitia kampeni ya M4C Operasheni Pamoja Daima kufanya kampeni katika kata hizo.

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe walifanya kampeni katika kata hizo kwa kutumia helkopta yao wakiwa na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho huku  wakiwa  na matumaini makubwa  ya kata  hiyo ya Nduli ,Ibumu na Ukumbi kuchukuliwa na Chadema jambo ambalo limekuwa kinyume.

Pamoja na viongozi hao wabunge kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa na yule wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao waligawana majukumu katika kata hizo.

Wakati Mchungaji Msigwa akifanya kampeni katika kata ya Nduli na mara moja moja katika kata hizo zingine,  Abwao kwa upande wake alikita zaidi katika kata ya Ibumu na Ukumbi.
Katika kampeni zake kata ya Nduli, Mchungaji Msigwa aliahidi kugawa mbolea kwa wananchi wa kituo cha kupigia kura ambacho Chadema ingeongoza kwa kura ahadi  ambayo  wananachi wa Nduli  wanaisubiri  hasa  kituo  Mitaba  ambacho  Chadema  waliongoza.

Hata hivyo kati ya vituo tisa vya kata hiyo ya Nduli, Chadema ilifanikiwa kuongoza kwa kura katika kituo kimoja tu cha Mibata kwa mgombea wake kupata kura103.

Akitangaza matokeo katika kata ya Nduli, Msimamizi wa Uchaguzi, Simba Nyunza alisema kati ya kura zote zilizopigwa, Mgombea wa CCM, Bashir Mtove alipata kura 810 huku Ayubu Mwenda wa Chadema akiambulia kura 491.

Huko wilayani Kilolo matokeo yaliyothibitishwa na mawakala wa CCM yanaonesha chama hicho kimepata ushindi mkubwa.

Katika kata ya Ibumu, mgombea wa CCM Gift Msumule ameibuka kidedea baada ya kupata kura 1,400 huku mgombea wa Chadema, Juli Mpungula akiambulia kura zaidi ya 400.

Katika kata ya Ukumbi, mgombea wa CCM, Hemed Mbena ameshinda kwa kishindo baada ya kuzoa kura 1479 dhidi ya kura 829 alizopata mgombea wa Chadema, Oscar Ndale.  

Huku  mbunge  Msigwa  akikiri  chama  chake kushindwa  katika uchaguzi  huo kata ya Nduli kwa madai kuwa  polisi  imekisaidia  chama  tawala  kushinda katika uchaguzi  huo.

Mbunge Msigwa  alitoa kauli  hiyo katika taarifa  yake  aliyoitoa kwenye  ukrasa  wake wa fecabook juzi jioni  baada ya matokeo kuonyesha chama  chake kimeshindwa  Nduli.

No comments:

Post a Comment