Na Frank Mvungi
SERIKALI imesema pato la Taifa limeendelea kukua kwa asiliamia 7 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2013 kutokana na mikakati mizuri ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kuzingatia dira ya Taifa ya maendeleo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa fedha Mh.Saada Mkuya Salum wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Saada alibainisha kuwa katika robo ya tatu ya mwaka 2013 kiwango halisi cha ukuaji wa uchumi kilikuwa asilimia 6.5 ikilinganishwa na asilimia 7.2 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2012.
Katika hatua nyingine Saada alisema kuwa Serikali imejipanga kuongeza pato kwa ufanisi zaidi ili kuongeza pato la Taifa na kupunguza ukwepaji wa kodi kwa kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi na kuwa ya kisasa zaidi.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) itaendelea kutoa elimu ya matumizi ya mashine za kielektroniki ili kusaidia wananchi kuelewa umuhimu wake kwa maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo alibainisha kuwa Serikali imekubaliana na wafanyabiashara kuwa mwisho wa kuanza kutumia mashine za kielektroniki umesogezwa hadi tarehe 30 januari, 2014 ili kuwapa wananchi muda wa kujiandaa na kuanza matumizi ya mashine hizo.
Pia alitoa rai kwa wadau wote kutoa ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa azma ya kuboresha mapato ya Serikali ili kuwaletea wananchi maendeleo endeleo.
Wizara ya Fedha imekuwa ikitimiza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUKUTA) malengo ya maendeleo ya Milenia (MDGs) Ilani ya Uchaguzi mkuu ya CCM ya mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment