TANGAZO


Tuesday, October 22, 2013

Sudan na Sudan Kusini kuzungumzia Abyei

 

Sudan Kusini inataka Bashir na AU kuwasikiliza watu wa Abyei kuhusu kutaka kujitawala
Marais wawili wa Sudan na Sudan Kusini Umar al-Bashir na Salva Kiir, wanafanya mkutano wa faragha muda mfupi baada ya Bashir kuwasili na wajumbe wake wa Sudan katika Ikulu ya Rais mjini Juba.
Kwa mujibu wa shirika la habari la SUNA, baadhi ya maswala yatakayojadiliwa kwenye mkutano huo yatakuwa, swala tete la Abyei,usalama pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
 
Mnamo siku ya Jumatatu, waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin, aliambia kituo cha redio cha Sudan CRN kuwa marais hao wawili watazungumzia mgogoro wa Abyei katika kutaka kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kuhusu swala la kura ya maoni kuhusu Abyei , waziri alisema kuwa Muungano wa Afrika hauruhusu uamuzi wa pande moja kuhusu kura ya maoni.
 
Aliongeza kuwa Kura ya maoni lazima iruhusiwe na nchi hizo mbili na kuidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
 
Aidha alisema kuwa sudan Kusini inashurutishwa na makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kwa hivyo haiwezi kuunga mkono kura ya maoni inayoshinikizwa na upande mmoja.
Hata hivyo alisema anaelewa kwa nini jamii ya Abyei iliamua kupiga kura ya maoni kujitenga na ni kwa sababu ya masaibu waliyoyapitia.
Alisisitiza kuwa Muungano wa Afrika na Sudan lazima ziisikilize jamii ya Abyei na kukubaliana kuhusu tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu kutaka kujitawala wenyewe.

No comments:

Post a Comment