TANGAZO


Wednesday, October 16, 2013

Rais Dk. Shein ahudhuria Swala, Baraza la Idd

*Awataka Wanzanzibari kuyachukua mafunzo ya Ibada ya Hijja kuwa muongozo wa maisha yao


Baadhi ya waumini wa Dini ya Kiislamu, waliohudhuria katika Swala ya Idi El Hajji, iliosaliwa Kitaifa huko katika kitongoji cha Marumbi, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati Unguja.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (wapili kushoto), akiwa pamoja na viongozi na wananchi mbalimbali katika Swala ya Idi El Hjji, iliyoswaliwa kitaifa leo, huko katika kitongoji cha Marumbi, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati Unguja. 
Baadhi ya viongozi wanawake pamoja na wananchi mbalimbali, waliohudhuria katika Baraza la Idi El Hajji, lililofanyika huko Tunguu, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati Unguja, wakiwa katika hafla hiyo.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, akitoa hotuba katika Baraza la Idi El Hajji, lililofanyika huko Tunguu, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati Unguja.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein (kulia), akiwa pamoja na Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, mara baada ya kumalizika kwa Baraza la Idi El Hajji lililofanyika huko Tunguu, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati Unguja. (Picha zote na Yussuf Simai Ali - Habari Maelezo, Zanzibar)

Na Mwandishi maalum, Zanzibar                                                                   
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wazanzibari kuyachukua mafunzo ya ibada ya hijja kuwa miongozo ya maisha yao ya kila siku huku wakihimizana wajibu wao wa kulinda amani, umoja na utulivu nchini pamoja na kuimarisha upendo na ushirikiano baina yao.

Dk. Shein ameeleza hayo leo, wakati alipokuwa akizungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA) huko Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba yake hiyo ambayo alitilia mkazo umuhimu wa wananchi kuishi kwa upendo na kulinda amani na utulivu Dk. Shein aliwaambia wananchi wa Zanzibar kuwa wasichezee  amani iliyopo iwe kwa kauli zinazohatarisha amani hiyo ama kwa vitendo.

“Tusichezee wala tusidharau amani tuliyonayo badala yake tuitunze na tuiendeleze, kwani inapotoweka inachukua muda mrefu na inakuwa vigumu kuirejesha tena hali hiyo” Dk. Shein alisema.

Aliwakumbusha wananchi wa Zanzibar kuwa wao ni watu wamoja hivyo hawana budi kuishi kwa misingi ya udugu,umoja na masikilizano  na kusisitiza kuwa bila ya amani Zanzibar haiwezi kufikia malengo iliyojiwekea ya kuendeleza ustawi wa nchi na watu wake.

Alifafanua kuwa wageni wakiwemo watalii na wawekezaji wanaokuja nchini miongoni mwa vivutio vikubwa ni hali ya utulivu, amani na ukarimu wa watu wa Zanzibar hivyo vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na sifa hizo zinaweza kuathiri uchumi na ustawi wa Zanzibar.


“watalii wanakuja kwetu kwa sababu wanavutiwa na amani tuliyonayo, wanavutiwa na umoja tulionao, wanatamka wazi wazi jinsi watu wa Zanzibar wanavyopendana na  wanavyopenda wageni. Aidha tunavutia wawekezaji kwa kuwaambia kuwa kivutio kimoja kikubwa kwetu ni amani na utulivu na wanapofika Zanzibar yote hayo wanayaona” Dk. Shein alifafanua.

Kwa hivyo aliwahakikishia wananchi na wageni kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinatekeleza wajibu wake wa kusimamia ulinzi lakini akatanabahisha kuwa vyombo hivyo vinahitaji ushirikiano toka kwa jamii ili viweze kutekeleza wajibu ipasavyo.

Dk. Shein alitahadharisha kuwa wale watakaobainika wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kisheria za nchi.

Alikemea vitendo kama vya kuwamwagia watu tindikali na kuvieleza vitendo hivyo kuwa ni vya kikatili na kinyama na kuongeza kuwa hapana dini inayoruhusu matendo kama hayo.

“Kwa hakika vitendo hivi ni vya kikatili na ni lazima sote kwa pamoja tuvilaani na kuvikemea. Naamini hakuna dini inayowaelekeza waumini wake kuwadhuru na kuwafanyia hujuma viumbe wengine seuze wanadamu wenzao”Dk. Shein alieleza.



Rais wa Zanzibar alitumia fursa hiyo kueleza hali ya uchumi ilivyo hivi sasa ambapo alieleza kuwa mwenendo wa ukuaji wa uchumi umeendelea kuwa mzuri ambapo uchumi ulikuwa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011 hadi asilimia 7 mwaka 2012.

Hivyo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo  pamoja na kushirikiana katika kukabiliana na changamoto zilizopo.

Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wakulima na kuzifanyia kazi hatua kwa hatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo nchini.

Kwa upande wa zao la karafuu Dk. Shein alisema Serikali itahakikisha huduma zote muhimu na vifaa vinavyohitajika kwa shughuli ya uvunaji wa zao hilo zinapatikana  na akawaomba wananchi kushirikiana na serikali kupambana na vitendo vya uuzaji wa karafuu kwa niia za magendo.

Baraza la Iddi lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharrif Hamad na Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume.

Kabla ya hapo Rais alihudhuria sala ya Iddi iliyofanyika huko kijiji cha Marumbi, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment