Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Viwanda na Biashara Nicodemus Mushi (kulia), akieleza kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu utoaji wa leseni za biashara chini ya sheria ya leseni za Biashara Na. 25 ya 1972 kwa Mfumo wa Kuhuisha na Kulipa ada, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Ofisa Biashara Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Christopher Nassari. (Picha zote na Hassan Silayo-Maelezo na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kazini wakati wa mkutano huo, ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar
es Salaam leo. Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Nicodemus Mushi (kushoto), akieleza kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu utoaji leseni za biashara chini ya sheria ya leseni za Biashara Na. 25 ya 1972 kwa Mfumo wa Kuhuisha na Kulipa ada, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO), Frank Mvungi.
Ofisa Biashara Mkuu wa Wizara ya
Viwanda na Biashara Christopher Nassari (kushoto), akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya mfumo huo wa ulipaji ada na
kuwataka wafanyabiashara kulipa ada hizo mapema kabla ya tarehe 31 Desemba 2013
ili kuepuka adhabu na faini, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya
Habari (MAELEZO), jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Ofisa Habari na Mawasiliano
wa Wizara hiyo Bw.Nicodemus Mushi.
*Yaonya wafanyabiashara kuhusu Mawakala wasio waaminifu
1. UTANGULIZI
Serikali
ilirudisha rasmi utozaji wa ada za Leseni za biashara kupitia Sheria ya Fedha
Na.5 ya mwaka 2011. Maandalizi yamekuwa yakifanyika kutoka wakati huo na ada
zimeanza kutozwa rasmi 01/07/2013 kwa mfumo wa kuhuishwa (Renewal).
Kutokana
na marekebisho hayo, utaratibu wa kutoa Leseni za Biashara BILA MALIPO uliondolewa na kusitishwa na Serikali tarehe 30 Juni,
2013. Leseni za Biashara zilizotolewa kuanzia tarehe 1 Julai, 2004 hadi 30 Juni, 2013 ambazo hazikuwa na UKOMO zinatakiwa kupelekwa kwenye
Mamlaka zilizotoa Leseni hizo, ili zihuishwe na kulipiwa ada kwa madhumuni ya kuongeza mapato kwa
Serikali.
Kila mfanyabishara mwenye Leseni ya
Biashara anapaswa kujaza Fomu ya Maombi ya Leseni ya Biashara na kuambatisha Leseni ya Biashara
aliyonayo na kuiwasilisha katika Mamlaka husika, kwa ajili ya kuhuisha na kulipia ada. Maombi yapelekwe katika Mamlaka
iliyotoa Leseni husika. Kwa Leseni za Biashara za kundi “A” kama ilivyoainishwa
kwenye Fomu ya Maombi ya Leseni ya
Biashara TFN Na. 211ya 2004 hutolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara. Maombi
hayo yawasilishwe katika Ofisi za Wizara ya Viwanda na Biashara zilizopo
Barabara ya Sokoine Jengo la NSSF-“Water
front”, Ghorofa ya Nne chumba Na. 416. Kwa wale Wafanyabiashara wa Kundi “B”
kama ilivyoainishwa kwenye Fomu ya Maombi ya Leseni ya Biashara TFN Na. 211ya 2004 wafike Ofisi
za Halmashauri za Majiji, Manispaa na
Wilaya zilizo katika maeneo yao, watapata huduma kutoka kwa Maafisa Biashara wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
2. UTARATIBU
WA KUFUATA ILI KUFANIKISHA ZOEZI NA KUPATA HUDUMA KWA HARAKA
- Kwa
wafanyabiashara wa Kundi “A” wajaze Fomu ya Maombi ya Leseni za Biashara
(fomu inapatikana katika tovuti ya Wizara sehemu ya Marketing Sector (www.mit.go.tz)
au fika Wizarani NSSF-Waterfront ghorofa ya 4 chumba Na. 416, Kwa
Wafanyabiashara wa Kundi “B” wawasilishe
maombi Ofisi za Halmashauri za Majiji, Manispaa na Wilaya zilizo katika maeneo
yao;
- Waambatishe
Leseni za Biashara za kudumu walizonazo na kuwasilisha kwenye Mamlaka
husika kama ilivyoainishwa hapo juu;
- Kwa
wafanyabiashara wa Kundi “A” wafanye malipo kupitia Benki ya CRDB mahali popote kwa kutumia
Account Number 0150413356300;
jina Revenue Collection Trading
License-MIT. Wafanyabiashara wa Kundi “B” wataelekezwa Benki ya
kulipia na Halmashauri zao;
- Kwa
wafanyabiashara wa Kundi “A” wawasilishe “pay slip” ya Benki ghorofa ya
Mezanine (NSSF-WaterFront) kwaajili ya risiti ya Serikali, Wafanyabiashara
wa Kundi “B” wataelekezwa Ofisi ya kuwasilisha ili wapewe reisiti ya
Serikali-Mweka Hazina wa Halmashauri;
- Kwa
wafanyabiashara wa Kundi “A” wawasilishe Fomu ya Maombi ya Leseni ya
Biashara, Leseni ya Biashara na risiti
ya malipo ghorofa ya 4 kwa ajili ya kuandikiwa Leseni ya Biashara,
Wafanyabiashara wa Kundi “B” wataelekezwa ofisi ya kupeleka na kuandikiwa
Leseni ya Biashara ofisi za Biashara za Halmashauri.
Waombaji wapya wa Leseni za
Biashara mnapaswa kujaza fomu ya maombi
ya Leseni za Biashara na kuambatisha nyaraka kama inavyojieleza katika fomu ya
maombi na kufuata hatua ya 1 hadi 5 kama ilivyoelezwa hapo juu.
Mnashauriwa kuhuisha na kulipia ada
Leseni za Biashara mapema kabla ya tarehe 31 Desemba, 2013 ambapo adhabu na faini kwa wafanyabiashra
watakaochelewa kuhuisha (Renew) itaanza
kutolewa tarehe 1 Januari, 2014.
- TAHADHARI
Wafanyabiashara mnatadharishwa kuwa hapa mjini
kuna mawakala wasio waaminifu maarufu kwa jina la VISHOKA. Mnashauriwa kuwaepuka
na muweke utaratibu wa kufuatilia Leseni za Biashara zenu wenyewe.
Kwa
wale ambao, wameshaletewa Leseni za Biashara na mawakala waliowatuma
mnashauriwa kwenda kwenye Mamlaka iliyotoa Leseni husika kwa ajili ya kufanya
uhakiki kwa kuwa imebainika kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya
biashara kwa kutumia Leseni batili (Feki)
TAFADHALI FIKA NA
KUFANYA UHAKIKI KWA FAIDA YA BIASHARA YAKO.
WIZARA YAVIWANDA NA
BIASHARA
No comments:
Post a Comment