WADAU wa afya nchini
wametakiwa kuacha kutegemea wahisani katika kutokomeza magonjwa mbalimbali
yanayoikumba jamii ikiwemo yale yasiyopewa kipaumbele.
Hayo yamesemwa leo na
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi wakati akifungua semina kwa Viongozi na
Watendaji wa Afya Mkoa wa Dodoma iliyolenga kujadili Mpango wa Taifa wa
Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele. Magonjwa hayo ni pamoja na
Matende, Minyoo ya tumbo, Kichocho, Usubi, Trakoma, Malale, Kichaa cha Mbwa na
Tauni .
Dkt. Nchimbi amesema
kuwa kumekuwepo na dhana potofu miongoni mwa jamii ya kusubiri Ufadhili
kutoka katika Mashirika mbalimbali kwaajili ya kupata msaada wa
kushughulikia maswala ya afya jambo ambalo amesema linarudisha jitihada
za kutokomeza magonjwa yanayoikumba jamii.
“Lazima tujue kujitegemea wenyewe kwani ulinzi
wa wananchi ni afya bora hivyo tuachane na dhana ya kutegemea wafadhili na tuwe
wa kwanza katika kuisaidia jamii yetu katika kuondokana na magonjwa
haya”alisema Nchimbi.
Aidha amewataka
watendaji hao kuunganisha nguvu kwa pamoja kwa kutumia mbinu mbalimbali ili
elimu iwafikie wananchi waweze kutambua namna ya kujikinga na magonjwa
yasiyopewa kipaumbele hasa katika ugonjwa wa upofu wa macho ambao umekuwa
kitambulisho cha Mkoa wa Dodomani kutokana na tatizo hilo kuwa kwa watu wengi
mkoani hapa.
Dkt. Nchimbi pia ametoa
wito kwa watu wanaougua magonjwa hayo wazingatie masharti ya umezaji dawa
pamoja kwenda Hospitalini na kwenye vituo vya afya ili waweze kupatiwa matibabu
bila ya gharama yoyotepamoja na kuzingatia
masharti ya umezaji dawa na kujitokeza ili kutibiwa mapema kwakuwa wengi wao
wamekuwa wakisingizia gharama za matibabu ambazo hutolewa bure katika vituo vya
afya nchini.
“Magonjwa haya hayana nafasi katika jamii yetu
hivyo wale wenye tatizo wajitokeze kwa wingi katika vituo vya afya ili waweze
kutibiwa bure kwani wapo wengine wanatumia kisingizio cha malipo ya dawa
kushindwa kupata matibatu katika vituo vyetu vya afya”alisema Dkt. Nchimbi.
Semina hiyo imewashirikisha pia watendaji wa
Serikali ikiwemo wakuu wa wilaya za mkoa wa Dodoma,Wenyeviti wa
Halmashauri,maofisa elimu na maofisa mipango imefadhiliwa na Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kupitia mpango wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele.
No comments:
Post a Comment