Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo akitoa hotuba kwa washiriki na baadhi ya wasanii waliohudhuria wakati wa uzinduzi wa Filamu ya“He hurtsMe” iliyotengenezwa na Bi. Hilda Ngaja, filamu iliyozinduliwa katika Ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo akionyesha juu filamu ya “He hurts Me” kuhashiria uzinduzi rasmi wa filamu hiyo uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo (kushoto) akiwa pamoja na mtengenezaji wa filamu hiyo Bi. Hilda Ngaja (kuli) wakifurahi kwa pamoja wakati wakiangalia kasha la filamu ya “He hurts Me” mara baada ya uzinduzi wa filamu hiyo.
Mtengenezaji wa filamu ya “He hurts Me” Bi. Hilda Ngaja (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mme wake Mr. Mwambene (kulia) wakati wa uzinduzi wa filamu yake uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Benedict Liwenga-Maelezo, Dar es Salaam)
Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
Katibu mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo amezindua filamu mpya ya “He hurts me” (ameniumiza au amenitenda), filamu ambayo imetengenezwa na Bi. Hilda Ngaja hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Bi. Fissoo ametoa pongezi kwa msanii huyo na Kampuni ya Hilderly Straight Film kwa kuthubutu kwao na ameongeza kuwa ana imani kuwa wadau haowataendelea kuzalisha filamu bora, zenye weledi, maadili na zinazoweza kuingia katika soko la ushindani. Pia amewashukuru washiriki wote kwa kushiriki kwao kikamilifu katika kufanikisha filamu hiyo.
Bi. Fissoo amesema kuwa filamu ya “He Hurts Me” (ameniumiza au amenitenda) ni kati ya filamu zinazolenga kutoa elimu katika jamii na ni filamu inayoweza kuonwa na wanajamii kwani imejikita katika kuelimisha, kuburudisha, kuadabisha na ni filamu inayofaa kuingia sokoni.
“Maudhui mahususi ya filamu hii kwetu sote na jamii kwa ujumla ni katika kutukumbusha umuhimu wa kuwapa malezi mema watoto wetu, jamii zinazotuzunguka zina watu wa aina na tabia mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri nguvu kazi ya taifa”. Alisema Bi. Fissoo.
Aidha, Bi. Fissoo amezungumzia suala kubwa juu ya malezi kwa watoto na vijana pia akaongeza kuwa ujio wa filamu hii utakuwa ni chachu na mchango mkubwa katika malezi na umekuja wakati ambapo taifa linahitaji wazazi na walezi kushiriki ipasavyo katika kuwezesha watoto na vijana kukua katika misingi ya malezi bora.
Kwa upande mwingine Katibu Mtendaji huyo amegusia masuala ya ukuaji wa tasnia ya filamu nchini na amesema kuwa tasnia hii imeendelea kukua kwa kasi sana na hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya filamu zinazozalishwa.
“Vijana na watu wa makundi mbalimbali wamejikita katika tasnia hii. Ni ukweli usiopingika kuwa tasnia ya filamu inatoa ajira nyingi”. Alisema Bi. Fissoo.
Bi. Fissoo amegusia pia masuala ya utamaduni na jinsi gani utamaduni unavyoweza kumuathiri ama kumnufaisha mtu hivyo amesisitiza kuzienzi tamaduni zetu.
“Napenda kuwakumbusha waandaaji wa filamu na watengenezaji filamu wote nchini kutengeneza filamu zisizodhalilisha , zisizolenga kuuza tu bali ziwe zinazolinda maadili, zenye kutumia rasilimali , mandhari na lugha yetu ya kiswahili katika kutangaza utaifa na utamaduni wetu ; hata majina ya filamu zetu ni vema yawe kwa lugha ya kiswahili.Tupende na kuenzi utamaduni, maadili na lugha yetu”. Alisisitiza Bi. Fissoo.
Bi. Fissoo alimalizia hotuba yake kwa kuwaasa wadau wote wa filamu wakiwemo watengenezaji na wasambazaji wa filamu kuheshimu Sheria na Kanuni zinazosimamia tasnia ya filamu nchini ambapo kwa sasa mwitikio wake umeanza kuwa mkubwa pia amewasihi kupeleka sokoni filamu zilizokamilisha taratibu zote na zilizowekwa stamp za TRA kwani Stamp hizo zina lengo la kuondokana na wizi wa kazi za wasanii pia amewasihi wadau wote kuunga mkono juhudi za serikali za kurasimisha tasnia za filamu na muziki kwani nia ya urasimishaji huu ni kurejesha nidhamu na hadhi katika tasni hizi na kuondokana na kilio cha muda mrefu ambacho kwa kiasi kikubwa kimefanya wasanii wa filamu na muziki kutonufaika na jasho lao.
Filamu ya “He hurts Me” (ameniumiza au amenitenda) imekaguliwa na Bodi na kupewa daraja 16 yaani inaruhusiwa kuonwa na watu kuanzia miaka 16 nakuendelea.
No comments:
Post a Comment