TANGAZO


Wednesday, September 11, 2013

Darasa la Saba wilayani Handeni wafanya mitihani yao

 

Wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Chanika iliyopo Halmsahauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wakipata chakula baada ya kufanya mtihani wa Sayansi, Kiswahili na Hisabati wilayani hapa leo, wanafunzi wa darasa hilo wanafanya mtihani wa kitaifa wa kuhitimu elimu ya msingi ambapo kesho watahitimisha kwa kufanya mitihani mitatu.

Na Dotto Mwaibale, Handeni
JUMLA ya wanafunzi 5725 waliosajiliwa wilayani hapa jana walianza kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba ambao unafikia tamati leo nchini kote.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muingo Lweyemamu, Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani hapa Mochiwa Mgaza alisema wanafunzi walioanza kufanya mtihani huo kuwa wavulana ni 2660 na wasichana 3065.
Alisema wanafunzi hao ni kutoka shule 139 zilizopo wilayani hapa kati ya shule 147 ambapo shule saba hazijafanya mitihani hiyo kwa sababu hazijafikisha darasa la saba.
Alisema maandalizi ya kupeleka vifaa na mitihani hiyo katika shule mbalimbali tayari yamefanyika na hakuwa na taarifa zozote mbaya.
Mgaza alisema misafara ya kupeleka mitihani hiyo iligawanywa katika makundi 26 na kila kundi kuwa na mkuu wa msafara pamoja na askari wa kumlinda pamoja na vifaa.
Alisema mitihani hiyo ilifika salama na kuhifadhiwa katika maeneo maalumu yaliyotengwa katika shule mbalimbali na kuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Alisema kuhusu idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani huo na wale ambao hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali itafahamika leo jioni kupitia fomu maalumu walizopewa wasimamizi wa mitihani hiyo.

No comments:

Post a Comment