TANGAZO


Friday, May 17, 2013

Rais Jakaya Kikwete ainusuru PSPF

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika picha ya pamoja na wadau pamoja na viongozi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, iliyofanyika mjini Dodoma leo. (Picha zote na Freddy Maro)

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa katika picha ya pamoja na wadau pamoja na viongozi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, iliyofanyika mjini Dodoma leo.


.Asema haijafilisika, aeleza chanzo cha mfuko kuyumba 
.Aahidi Serikali kulipa bil. 50 katika bajeti ijayo

Na Joyce Kasiki, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSPF, haupo mahututi isipokuwa ni kwa sababu inadai shilingi Trilioni 6 kutoka Serikalini.

Dk. Kikwete alitoa kauli hiyo leo, wakati akizungumza kwenye kilele cha  maadhimisho ya wiki ya Mifuko ya Hifadhi  ya Jamii yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Kumbukumbu ya Nyerere vilivyopo mjini Dodoma.

Alisema kuwa kuna baadhi ya waliokuwa wanasema kuwa mfuko huo, umefilisika jambo ambalo alisema siyo kweli.

"PSPF haijafilisika, naongea hivi kwa sababu wapo baadhi ya watu wanaosema kwamba  PSPF imefilisika, ukweli wa jambo hili ni kwamba, mwaka 1999 wafanyakazi wote wa Serikali, walipoingizwa kwenye kundi la Pensheni wakati wengine walikuwa hawakuchangia kwenye mifuko ya Hifadhi ya jamii ndio waliosababisha Serikali kuingia kwenye deni hilo kwani ilikuwa ni lazima walipwe," alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo alisema, Serikali itaanza kulipa deni hilo katika  mwaka ujao wa Fedha, Serikali italipa shilingi Bilioni 50 ili kuunusuru mfuko huo na uendelee kutoa huduma zake za Mafao kama kawaida.

Amewatoa hofu wananchi na kusema kila aliyechangia pesa zake kwenye mfuko huo atalipwa Mafao yake kwani nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.

Pensheni kwa wazee

Katika hatua nyingine Rais Kikwete ameitaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA) kuongeza kasi katika kukamilisha mpango wake wa Pensheni kwa wazee.

Pia alitaka kuwepo kwa vyanzo vya mapato ili zoezi hilo   liwe endelevu pindi litakapoanza huku akiwaonya kutojaribu kufanya jambo hilo kama wanaona hawawezi kulimudu.

"Tunataka wazee kuanzia miaka 60 ambao hawakuwahi kuajiriwa nao wapate Pensheni ,lakini ikumbukwe wazee hawa hawakuwahi kuwa waajiriwa hivyo hawana michango yoyote,cha msingi hapa ni kuhakikisha mnaweka misingi imara ya kulifanya zoezi hilo kuwa endelevu,lakini kubwa kuwa na vyanzo vya mapato." alisema.

 Alienda mbali zaidi kwa kuwataka watendaji wa zoezi hilo kuwa waadilifu kwa kulipa wale wanaostahili tu pindi zoezi hilo litakapoanza na siyo kulipa na mamluki.

"Mnapofanya  jambo hili lazima mlitazame kwa kina huku mkienenda katika maadili,walipwe wale waliokusudiwa,wazee tunaowazungumzia hapa ni wale wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea,sasa lazima mjue kwamba  kila mwenye mvi siyo mzee na kila asiyekuwa na mvi siyo kijana." 

Aliwaasa  kuutathimini mpango huo ili usilete athari ya watu wengine kujitoa kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii wakitegemea watakapokuwa wazee wataingizwa kwenye mpango wa Pensheni. 

Pia  Dk. Kikwete ameiagiza mamlaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini (SSSRA) kuhakikisha mifuko hiyo inafanya tathmini katika uwekezaji  wake.

Alisema kuwa ni vema kwa mamlaka hiyo kuhakikisha inafanya tathmini ili kujiridhisha kama uwekazaji ambao unafanywa na mifuko hiyo inafaida au la. 

Hata hivyo Kikwete aliitaka mamlaka hiyo kutoa miongozo kwa mifuko hiyo katika suala zima la uwekezaji.

No comments:

Post a Comment