TANGAZO


Monday, May 20, 2013

Boko Haram watawanyika kutoka ngome zao



Jeshi linasema kuwa wapiganaji wametawanyika kufuatia operesheni kali dhidi yao
Jeshi la Nigeria limesema kuwa wapiganaji wa kiisilamu Kaskazini Mashariki mwa Nchi, Boko Haram, wametawanyika huku baadhi wakiondoka nchini humo baada ya jeshi kuanza operesheni dhidi yao.
Katika taarifa yake, jeshi lilisema kuwa wapiganaji 14 wameuawa na wengine ishirini kukamatwa tangu Jumamosi.
Wanajeshi wake watatu walifariki katika mapambano na wapiganaji hao. Mwandishi wa BBC mjini Abuja anasema kuwa sio rahisi kuthibitisha taarifa hiyo.
Jeshi bado halijatoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake wakati huduma za simu za mkononi nazo zikiwa zimekatizwa katika baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa jeshi, wanajeshi 1,000 zaidi watatumwa kwenda kukabiliana na wapiganaji hao.
Jimbo la Adamawa ni moja ya majimbo ambako sheria ya hali ya hatari ilitangazwa, wiki jana.
Takriban wanajeshi 2,000, walipelekwa katika eneo hilo, wiki jana katika operesheni kubwa kuwahi kushuhudiwa dhidi ya wapiganaji hao wa kiisilamu.
Maafisa wanasema kuwa takriban watu 2,000, wametoroka kufuatia operesheni hiyo wakati wengine wamevuka na kuingia Cameroon.
Juhudi zimefanywa ili kufunga mipaka lakini bado kuna uwezekano wa watu kuuvuka na jeshi linasema kuwa na wakati mgumu kutofautisha kati ya wapiganaji wa Boko Haram na raia wa kawaida .
Duru zinasema kuwa ushahidi wa kuonyesha kuwa Boko Haram walikuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha harakati zao ni kuwa wana magari yao kambini ambayo wanajaribu kuyahamisha na kuwa yamelengwa kushambuliwa na wanajeshi.

No comments:

Post a Comment