(CUF – Chama Cha Wananchi)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU JUHUDI ZA CUF ZA KUENDELEZA AMANI NA UTULIVU BAADA YA
SALA YA IJUMAA TAREHE 2 NOVEMBA 2012Siku ya Alhamis nikielekea Muhimbili kumpeleka shangazi yangu hospitali nilipata taarifa kuwa Imam wa msikiti wa Masjid Haq (ulioko jirani na Afisi Kuu ya CUF na ambapo nasali sala ya Ijumaa nikiwa Afisi Kuu) na watu wengine watatu akiwemo Sheikh Ramadhan S. Sanze (ambaye namfahamu kwa muda mrefu). Sadik Gogo na Mzee Abdillah wamekamatwa na wamefikishwa kituo cha polisi cha kati (Central Police Station). Nilistushwa na kamata kamata hii na nikahofia kuwa inaweza kuongeza jazba miongoni mwa waumini wa Kiislam. Baada ya shangazi kupata tiba katika hospitali ya Muhimbili nilimrudisha nyumbani na nikampigia simu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na mahusiano ya umma, Abdul Kambaya, tukutane kituo cha polisi cha kati kuulizia sababu za kukamatwa Imam wa Masjid Haq na wenzake watatu na kama tunaweza kuwawekea dhamana.
Tulipofika kituo cha polisi tulibaini kuwa Imam wa
Msikiti wa Masjid Haq hajakamatwa bali kuna muumini mwingine kwa jina la Mkadam
Swalehe ndiye aliyekamatwa. Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu
kuachiliwa kwa wale waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi wafanyiwe
mahojiano na baadaye wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe ambaye ana faili
jingine pale polisi linaloendelea kufanyiwa upelelezi. Tulifahamishwa kuwa
nitume mtu saa 10:30 jioni ili aweze kufuatilia utaratibu wa kuachiliwa watuhumiwa
watatu akiwemo Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee Abdillah.
Nilishauriana na Wakurugenzi wa CUF walioko Dar es Salaam
na Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za kukamatwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na kupandisha jazba ya Waislam wengi. Tulipata
wasiwasi kuwa jazba hii inaweza kupelekea Waislam wengi kuandamana baada ya sala
ya Ijumaa. Ikiwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wataachiwa na Waislam
wakapata taarifa hiyo inaweza kusaidia kupunguza jazba na watu wasishiriki
maandamano baada ya sala ya Ijumaa.
Nilimpa jukum Abdul Kambaya afuatilie Central
PoliceStation, suala la kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake. Niliwasiliana naye
kwa simu na kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik
Gogo na Mzee Abdillah wataachiwa baada ya kukamilisha mahojiano. Ilikuwa
inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha Press Conference haukuwepo.
Tukakubaliana Naibu Katibu Mkuu awasiliane na wahariri wa habari wa vituo vya
televisheni Channel 10, TBC1, Star TV, Mlimani TV na ITV ili niweze kutoa
taarifa ya kuwasihi Waislam warudi majumbani na kwenye shughuli zao baada ya
sala ya Ijumaa. Niliweza kufanya mahojiano na
Channel 10, TBC1, na ITV. Kwa bahati mbaya Camera person wa Star TV
alikuwa kwenye shughuli nyingine na kwa
hiyo sikuweza kufanya mahojiano na Star TV. Vilevile wapiga picha wa Mlimani TV
hawakuwepo kwenye studio. Pia nilipata bahati ya kuzungumza na Radio Iman
inayosikilizwa na Waislam wengi na kueleza maoni yangu kuwa Waislam wasiandamane baada ya
sala ya Ijumaa.
Baada ya kutoa taarifa kwenye vituo vitatu vya
televisheni na Radio Iman kuwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wataachiliwa na
kuwasihi Waislam wasishiriki maandamano
baada ya sala ya Ijumaa nilimpigia simu Abdul Kambaya kuulizia kama
naweza kuzungumza na Sheikh Ramadhan Sanze. Kambaya akanieleza mambo
yamebadilika na hawajaachiwa. Niliwasiliana na RCO na nikabaini kuwa suala hilo
haliko tena chini ya uamuzi wake na litakamilishwa siku ijayo.
Usiku wa alhamisi kuamkia Ijumaa nilijaribu kuwasiliana
na Rais Kikwete kupitia wasaidizi wake ili nimfahamishe mantiki na sababu ya
hatua nilizochukua na atumie uwezo wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake waachiliwe. Kwa bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa simu na
akanipigia simu saa 6:50 usiku na kunifahamisha atajitahidi kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe. Rais ili
nipate kuongea naye kuhusu jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili
kupunguza jazba na kuepusha shari. Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais
alikuwa Arusha na ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata
fursa ya kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa.
Siku ya Ijumaa Abdul Kambaya aliendelea kufuatilia
kuachiwa kwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake Central Police Station. Nami
katika kuhangaika ili waliokamatwa waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na
IGP na kumfahamisha sababu ya juhudi nilizochukua na mategemeo yangu kuwa
Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa. Ninakiri kuwa katika mazungumzo ya simu,
IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu sana katika kauli yake. Alinishukuru kwa
kauli niliyoitoa katika vituo vya televisheni na kuwa atafuatilia suala
nililomueleza. Hatimaye Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake waliachiwa.
Naamini kama Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wangeachiwa
ingesaidia sana kupunguza jazba. Hata hivyo Waislam wengi na wananchi wengine
kwa ujumla walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika maandamano.
Baadhi wamenikosoa na kushauri kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya maandamano kufanyika
na kama patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe tamko la kulaani vitendo vya
polisi na serikali.
Katika mitandao ya kijamii wengine wamekejeli juhudi
zangu. Nilikubali kushiriki katika kipindi cha Makutano show kinachoendeshwa na
Bi. Fina ambapo hupata maswali toka Jamii Forum. Moja ya swali lililotolewa ni
“Muulize very very solid, kuna agenda gani kati ya Cuf na uislam? mtaani leo
wanasema kauli ya Lipumba ya jana kusitisha maandamano wameitii, na ukiangalia
mikutano yake pale jangwani utafikiri kuna mawaidha ni balaghashia na baibui.”
Fina hakupata muda wa kuniuliza swali hili. Jibu lake ni la wazi. CUF
inasimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi ambao ni Waislam
na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao. Kuhusu balaghashia na
baibui ni vyema vijana wakatazama picha za umati wa watu uliokuwa unahutubiwa
na Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa nchi hii. Picha hizo pia
zinaonyesha waliokuwa wakipigania uhuru wengi walivaa balaghashia na baibui
hata Mwalimu Nyerere alipewa zawadi nyingi za balaghashia na akaamua kuzivaa.
Kushamiri kwa demokrasia ya kweli msingi wake mkubwa ni
amani na utulivu. Amani ya kweli haipatikani bila kuwepo haki. Kesi ya Sheikh
Ponda msingi wake na madai ya kiwanja. Ki msingi kesi ya madai ya kusuluhishwa
na Mahakama ya ardhi. Sheikh Ponda ana haki ya msingi ya kupewa dhamana hata
kama kauli zake haziifurahishi serikali.
Nasikitika sana katika kipindi hiki tete, viongozi wa
serikali wameshindwa kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na Maimam wa
misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake wameachia
kauli za vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano kati ya serikali na
Waislam. Ni vyema serikali ikatumia busara na kuwasiliana na Maimamu wa
misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kuelewa hoja na malalamiko yao.
Hatimaye nimepata fursa ya kuzungumza na Mheshimiwa Rais
leo asubuhi na nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza kupunguza jazba na
kuwaomba Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala ya Ijumaa. Ni wazi
hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana Mheshimiwa Rais na
ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta suluhisho.
Katika kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na
jitihada za kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete.
Nitazungumza na viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi wa
Makanisa ya Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu ni kuwafahamisha mantiki ya
juhudi nilizofanya na kushauriana misingi muhimu ya Waumini wote kuheshimiana
na kuvumiliana ili tujenge Tanzania yenye haki sawa kwa wote.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti
Novemba 4 2012


No comments:
Post a Comment