TANGAZO


Thursday, March 29, 2012

SMZ yakanusha kuibuka kwa Mv. Spice Islander 1

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar, SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kuwa taarifa zilizozagaa Zanzibar za kuibuka na kuonekana kwa Meli ya Mv.Spice Islander 1 iliyozama Septemba Mwaka jana katika mkondo wa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja siyo za kweli.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Hamad Masoud Hamad ameyasema hayo hivi leo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Zanzibar wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na utendaji kazi wa Wizara yake.
Amesema kuwa ni kweli kuna Meli imeonekana katika mkondo huo lakini siyo meli ya Mv.Spice Isalnders 1 bali ni meli ya uvuvi ya Komoro ambayo ilizama siku nyingi yenye namba za usajili 2NCT 4/2905.
Akielezea kuhusu Meli hiyo na kuzagaa kwa taarifa amesema taarifa zilikuja toka jana jioni ya saa 12.30 kutoka kwa wavuvi wa Nungwi ambao waliiyona Meli hiyo ambapo Wizara chini ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bahari Zanzibar Abdallah Kombo walitafuta uhakika wa jambo hilo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi huyo amesema walifanya mawasiliano na kutuma kikosi kazi ambacho kilibaini kuwa Meli hiyo ya kivuvi ilizama Februari 3 na kuibuka katika Mkondo wa Bahari ya Hindi Machi 20 kabla ya kuonekana tena siku ya jana katika maeneo ya Mkondo wa Nungwi.
Aidha Kombo amesema wameshafanya mawasiliano na vyombo mbalimbali vya bahari kwa lengo la kuwapa taarifa kuhusu meli hiyo ambayo inaendelea kuzagaa katika bahari.
Kwa upande mwengine Waziri huyo wa Miundo mbinu amesema jumla ya Tshs 900 Milioni zimetumika kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi ambao nyumba zao zimepakana na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume Zanzibar na kwamba ambao bado hawajalipwa fedha zao utaratibu unaendelea kwa awamu.
Amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha inawalipa fidia wale wote ambao nyumba zao zinatakiwa kubomolewa ili kupitisha ujenzi wa Uwanja huo ambapo kiasi cha Milioni 500 za fidia zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha awamu  nyengine ya malipo ya wale ambao nyumba zao zitaathirika na zoezi hilo.
Akizungumzia kuhusu suala la kusimamishwa kwa Mkandarasi ambaye amepewa jukumu la kujenga Uwanja huo amesema jambo hilo si kweli bali ujenzi huo unaendelea kwa awamu ambapo viongozi wa Wizara hiyo wakiongozwa na Naibu waziri wake wako nchini China kuendelea kujadiliana na Mkandarasi huyo jinsi ya kuendeleza ujenzi huo.
Waziri huyo amesema wizara yake imejipanga vyema kuhakikisha kuwa wanatimiza maelngo waliyojiekea chini ya Idara za Wizara hiyo ambapo amewaomba wananchi na wadau mbalimbali kuonesha ushirikiano katika kutimiza malengo ya Wizara.
Waziri Hamad Masoud amefanya mkutano huo na waandishi wa habari ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza agizo lililotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein kwamba kila kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha anawafikishia taarifa wananchi juu ya utendaji kazi wa Ofisi yake.

No comments:

Post a Comment