Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya mzaha na Wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Fuoni Jimbo la Dimani baada ya kulikagua Jengo jipya la Skuli hiyo litakalosaidia kupunguza idadi kubwa ya Wanafunzi madarasani.(Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Balozi Seif na Baadhi ya Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Serikali wakikagua shughuli za uwezekaji wa Jengo jipya la Skuli ya Msingi Fuoni linalojengwa kwa nguvu za Wananchi ambapo aliahidi kukamilisha ujenzi wake.
Balozi Seif Kati kati akiwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayopub Mohamed Mahmoud Kushoto yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed wakikagua ujenzi wa Nyumba za Makaazi katika Mradi wa Baghresa Group Fumba.Balozi Seif akibadilishana mawazo na Uongozi wa Timu ya CPS Live Bwana Johan Vanden Abeele na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Bibi Katrin Dietzold wanaoendesha Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Makaazi katika ukanda wa Maeneo huru ya Uwekezaji Fumba Wilaya ya Magharibi “B”.
Pango la Maji safi na salama linalotoa huduma za maji na salama na kusambazwa katika Vijiji vilivyomo ndani ya Jimbo la Dimani.
Mhandisi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Hussein Hassan Njuma wa kwanza kutoka kulia akimuelezea Balozi Seif aliyepo Kulia yake tatizo linalolikumba pango hilo la kupunguza kiwango cha idadi ya Lita zinazosambazwa kwa Wananchi kutokana na maji yake kuchanganyika na Chumvi baadhi ya wakati. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Ardhi, Maji Nishati na Mazingira Mh. Salama Aboud Talib na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Balozi Seif na Ujumbe wake akimaliza kulikagua Jengo Jipya la Soko la Samaki lililojengwa kwa nguvu za Wauvi wenyewe wa Pwani ya Kichangani.
Picha no:- 909 ni:- Haiba nzuri inayoonekana ya Jengo Jipya la Skuli ya Bwefum Jimboni Dimani linalojengwa na Muwekezaji Mzalendo ambalo kukamilika kwake litatoa huduma za kitaaluma kwa Wanafunzi wa Wilaya Nzima ya Magharibi “B”.
Meneja Mkuu wa Kiwanda cha uzalishaji wa maziwa Maeneo huru ya Uwekezaji Fumba Bwana Adson Fagundes Kulia akimtembeza Balozi Seif na Ujumbe wake ndani ya Kiwanda hicho kujionea uzalishaji wa Bidhaa hiyo muhimu kwa afya za Wanaadamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Viongozi wa Shehia zilizomo ndni ya Jimbo la Dimani katika Mkutano wake wa majumuisho ya ziara yake Jimboni humo hapo Skuli ya Kombeni.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/7/2017.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na Kamisheni ya Ardhi Zanzibar kulipima eneo lote la ardhi lililotengwa ndani ya Ukanda wa Mji Mpya wa Fumba kwa ajili ya shughuli Maalum za uwekezaji.
Alisema agizo hilo lazima lifanywe ndani ya muda wa Mwezi Mmoja kuanzia sasa na ripoti kamili ya utekelezaji wake akabidhiwe katika kipindi hicho ili kutoa fursa kwa wananchi wa maeneo hayo kuelewa mipaka halisi ya eneo hilo na yale waliyopimiwa wao kwa ajili ya shughuli za Maendeleo na Miradi ya Kijamii.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akizungumza na Viongozi wa ngazi mbali mbali katika Wilaya ya Magharibi “B” baada ya kumaliza ziara ya kutwa moja katika Jimbo la Dimani kukagua harakati za Maendeleo pamoja na kupokea kero tofauti zinazowakabili Wananchi wa Jimbo hilo hapo katika Skuli ya Kombeni.
Alisema mabadiliko makubwa ya uwekezaji Vitega Uchumi unaoendelea kuimarika kwa kasi katika kipindi hichi ndani ya ukanda huo wa Kiuchumi unatoa ishara kwa Wananchi kutambua thamani ya Ardhi kiasi kwamba pasipo na utaratibu mzuri wa mipaka sehemu hiyo inaweza kuja kukumbwa na migogoro ya ardhi inayoweza kuepukwa mapema.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haipendelei kuona kwamba migogoro ya ardhi katika maeneo mbali mbali Nchini inazidi kuongezeka jambo ambalo linaweza kuviza Maendeleo yanayokusudiwa kutandikwa kupitia rasilmali hiyo muhimu kwa Taifa na Wananchi wa Ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza katika kuitafutia ufumbuzi changamoto inayotokana na matumizi ya Ardhi ni vyema kwa Taasisi zinazohusika na usimamizi wa miradi ya Miundombinu na Uwekezaji zikazingatia kipaumbele cha kulipa fidia wananchi ambao maeneo yao kuchukuliwa kwa ajili ya kuendelezwa miradi na shughuli za Jamii .
Balozi Seif alisema kabla ya kuanza kwa ujenzi wa Mradi wowote wa Uwekezaji katika sehemu yoyote ile ya Visiwa vya Zanzibar ni lazima suala la fidia lizingatiwe kwanza ili kuepuka malalamiko ya Wananchi wanaohusika na fidia za Mali na Vipando vyao.
Aliwanasihi Wananchi kuendelea kubeba dhima ya kushirikiana na Wawekezaji wanaoamuwa kuweka vitega uchumi katika maeneo yao ili ile nia thabiti inayokusudiwa na Serikali Kuu ya kukaribisha uwekezaji iweze kufanikiwa vyema.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Viongozi pamoja na Wananchi wa Majimbo ya Dimani na fuoni kwa uamuzi wao wa kuushirikiana katika Miradi ya Kiuchumi na ile ya Ustawi wa Jamii na kupelekea kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.
Mapema Wananchi na Viongozi wa Shehia Nane zilizounda Jimbo la Dimani walisema Huduma za maji safi na salama, ukosefu wa miundombinu imara ya Bara bara, uchakavu wa baadhi ya majengo ya Skuli na Vituo vya Afya ndio mambo ya msingi yenye kuleta changamoto ndani ya Jimboni hilo.
Walisema licha ya juhudi kubwa inayochukuliwa na Serikali kuu ya kutoa fedha kwa ajili ya uimarishaji Miundombinu ya maji lakini bado tatizo hilo limekuwa sugu na kuleta usumbufu na wakaishauri Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa matumizi ya fedha ilizotoa kwa ajili ya kuendelezwa mradi wa Maji.
Hata hivyo Wananchi hao walisema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Viongozi wao wa jimbo katika kuwaletea maendeleo pia wameiomba Serikali ifanye uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliopewa maeneo kwa ajili ya Uwekezaji na wakashindwa kuyaendeleza wanyang’anywe mara moja na kupewa watu watakaokuwa na uwezo wa kuyaendeleza kwa faida ya Jamii.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya kero zilizowasilishwa na Wananchi wa Jimbo la Dimani kwenye Mkutano huo wa Majumuisho Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alishauri ni vyema changamoto zote zinazoibuka katika shehia za Jimbo hilo zikawasilishwa kwanza katika Uongozi wa Wilaya kwa hatua ya awali.
Mh. Ayoub alisema baadhi ya changamoto inawezekana kutatuliwa ndani ya ngazi za Majimbo, Wilaya na Mkoa badala ya mzigo huo kuwasilishwa moja kwa moja Serikali Kuu ambayo ina majukumu makubwa ya Kitaifa yanayohitaji kushughulikiwa.
Aliwahimiza Wananchi kuendelea kushindana katika kujiletea Maendeleo yao huku wakielewa kwamba Serikali Kuu pamoja na viongozi wa ngazi tofauti watahamasika kuunga mkono jitihada watakazoonyesha Wananchi hao.
Akigusia kero zinazowasumbuwa Wananchi za upandishwaji holela wa nauli kwa Gari za Abiria usiozingatia utaratibu uliowekwa Mkuu huyo wa Mkoa wa Mjini Magharibi alitahadharisha wazu kwamba Uongozi wake utakaa pamoja na Idara ya Leseni kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
Alisema tabia ya baadhi ya makonda wa Gari za Abiria kupandisha nauli kiholela kwa tamaa ya kuata faida ya haraka inaleta usumbufu kwa Wananchi wenye kipato cha chini na kamwe Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi haitolivumilia kero hilo kuona linaendelea.
Balozi Seif aliyeambatana na baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Watendaji Wakuu wa Serikali alikagua Jengo jipya la Skuli ya Fuoni linalojengwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe ambapo aliahidi kugharamia umaliziaji wake ili kuondoa usumbufu wa msongamano wa wanafunzi uliofurika ndani ya Skuli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia akaahidi kusaidia nguvu za Wavuvi wa pwani ya Kichangani katika ukamilishaji wa Jengo lao jipya la Soko katika Kijiji hicho lililotoa ajira za wavuvi wapatao 80 pamoja na kuona pango la Maji safi na Salama lililopunguza kasi ya usambazaji wa huduma za maji katika sehemu kubwa ya Jimbo la Dimani.
Baadae Balozi Seif akapata wasaa wa kukikagua kiwanda cha uzalishaji wa Maziwa katika eneo huru la Uchumi Fumba kilichojengwa na Muwekezaji Mzalendo na kutoa ajira kubwa kwa vijana walio wengi.
Ukaguzi huo ulikwenda sambamba na kuangalia ujenzi wa Nyumba za Kisasa za Makaazi katika eneo la Mwambao wa Pwani ya fumba zinazojengwa na Wawekezaji Wazalendo pamoja na wale wa Kigeni walioamua kuitumia fursa hiyo iliyopo Zanzibar.
Balozi Seif ambae halkadhalika aliitembelea Skuli Mpya ya Sekondari inayojengwa na Muwekezaji Mzalendo katika Kijiji cha Bwefum alielezea faraja yake kutokana na mabadiliko makubwa ya uwekezaji yanayoendelea kuchanja mbuga ndani ya Ukanda wa Maeneo huru ya Kiuchumi Fumba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru Wananchi wa Vijiji vya Bweleo, Bwefum na Fumba kwa ukarimu wao wa kukubali kuwakaribisha Wawekezaji hasa katika Sekta ya Elimu na kinachoonekana sasa kwa Wawekezaji hao katika kuunga mkono miradi ya Jamii ni matunda ya Uwekezaji huo.
Balozi Seif alisema Uwekezaji huo wa miradi mbali mbali ya Kiuchumi umewezesha kuibadilisha mandhari nzima ya sehemu hiyo na kuiona ya kuendeza kiasi kwamba ile dhamira halisi ya Serikali iliyokuwa nayo tokea miaka ya 90 ya kulifanya eneo hilo kuwa la Mji wa Kisasa imeanza kujichomoza pole pole.
No comments:
Post a Comment