Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angellah Kairuki
Na Said Ameir-Maelezo
SERIKALI imesema ingependa kuona sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuweka wazi
takwimu zao ikiwa ni njia mojawapo ya kuchochea dhana ya uwajibikaji na vita
dhidi ya rushwa nchini.
Akifungua
Mkutano wa siku moja kuhusu Mpango wa Uendeshaji Shughuli za
Serikali kwa Uwazi na Takwimu Huria kama kichocheo cha uwajibikaji na
vita dhidi ya rushwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Angellah Kairuki amesema ushirikiano ambao Serikali inataka kuujenga kati
yake na wadau wengine katika takwimu huria ni ule utakaokuwa katika misingi ya
uwazi na kuaminiana.
Amesema
kuwa ni muhimu kwa washirika wa maendeleo, taasisi za kijamii, mashirika yasiyo
ya kiserikali kuweka wazi takwimu zao zikiwemo mikataba, hesabu zao
ziliyokaguliwa na manunuzi.
“Serikali
ya Awamu ya Tano imedhamiria kutekeleza shughuli zake kwa uwazi hivyo inawaomba
wadau wengine nao wafuate nyayo za Serikali kwa kufungua takwimu zake kwa
dhamira ya kuimarisha uwazi”, Waziri Kairuki alieleza.
Waziri
huyo alisema kuwa Serikali haiwezi kufanyakazi pekee (kwa kujitenga) kwa hivyo
suala la kujenga ushirikiano na wadau wengine ni la lazima na kusisitiza kuwa ushirikiano
huo sharti uwe katika misingi ya uwazi na kuaminiana.
Alibainisha
kuwa Tanzania imeamua kujiunga na mpango wa takwimu huria na inauona mpango huo
kama fursa nzuri kwake kuimarisha demokrasia na utawala bora kwani chini ya
mpango huo, Serikali imebuni na kuchukua hatua maalum za kuhimiza uwazi na
uwajibikaji.
Alitaja
baadhi ya mafanikio ya mpango huo wa takwimu huria kuwa ni pamoja na kuanzisha
Tovuti ya Takwimu Huria na kutayarisha seti za takwimu 163 ambazo tayari
zimeshawekwa katika tovuti na wadau wameanza kuzitumia. Alizitaja takwimu hizo
kuwa ni za sekta ya elimu, afya na maji.
Waziri
Kairuki alitumia fursa hiyo kuwashukuru waandaaji wa mkutano huo pamoja na
wafadhili wakiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa
Maendeleo la Uingereza(DfID) ambao alisema michango yao imeiwezesha Tanzania
kuwa kinara katika Uendeshaji
Shughuli za Serikali kwa uwazi na masuala ya takwimu huria katika bara
la Afrika.
Awali
akimkaribisha Waziri kufungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu
(NBS) Dk. Albina Chuwa aliwashukuru washiriki wa mkutano huo ambao ni miongoni
mwa wadau wakuu wa takwimu kwa ushirikiano wao kwa miaka miwili sasa, tangu
kufanyika Mkutano wa Kwanza wa Afrika wa Takwimu Huria uliofanyika hapa nchini ambao ulihudhuriwa na washiriki wengi.
Alibainisha
kuwa tangu kufanyika kwa mkutano huo, wadau hao wameshiriki katika kutayarisha
Tovuti ya Takwimu Huria ambamo takwimu za sekta za afya, elimu na maji zimeweka
wazi kwa matumizi ya kila mtu.
Kazi
nyingine walizofanikiwa kuzifanya kwa pamoja ni kutayarisha Rasimu ya Sera ya
Takwimu Huria, Mkakati wa Utekelezaji wake na Mkakati wa Mawasiliano. Aidha
alieleza kuwa baadhi ya wadau hao walifanikiwa kusaidia katika kujenga uwezo wa
baadhi ya taasisi katika kuandaa na kuchapisha takwimu huria.
Dk.
Chuwa aliwahakikishia wadau hao kuwa pamoja na ufadhili wa mradi huo kupitia
Benki ya Dunia kuwa utamalizika mwezi ujao, Serikali na NBS zitaendelea kufanya
kazi na wadau wapya ili kuhakikisha kuwa kazi ya uzalishaji na usambazaji wa
takwimu pamoja na kuimarisha ubora wake inafanyika.
Akizungumza
kufunga mkutano huo, Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa NBS, Irenius
Ruyobya alieleza kuwa Sera ya Takwimu ambayo imo katika hatua za mwisho
kukamilika imepitia hatua zote za ushirikishwaji wadau kama taratibu zinaelekeza.
“Mchakato
wa utungaji Sera umepitia hatua zote za uwashirikishwaji wadau kwa njia
mbalimbali zikiwemo mikutano na kupitia mitandao ambao mwitikio ulikuwa mkubwa”,
alisema na kusisitiza kuwa utaratibu ni kuwa rasimu ya Sera haiwezi kufikishwa
ngazi za maamuzi bila ya kipengele cha ushirikishwaji wadau kutekelezwa.
Aidha,
Bwana Ruyobya aliwaeleza washiriki kuwa Sheria ya Takwimu haipo kuwadhibiti
wakusanya takwimu bali jukumu lake kubwa ni kuratibu utoaji wa takwimu rasmi za
Serikali au zile ambazo zitatumiwa katika kutolea maamuzi, ufatuatiliaji na
utekelezaji wa mipango ya Serikali.
Mkurugenzi
huyo alibainisha kuwa wanatakwimu wote ni “wadau wa NBS” na kusisitiza kuwa kumekuwepo na ushirikiano
wa karibu kati ya Ofisi yake na wadau mbali mbali wa takwimu lengo likiwa ni
kuhakikisha takwimu wanazozitoa zinakidhi viwango na vigezo vilivyowekwa.


No comments:
Post a Comment