Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Hassan Abbasi akizungumza wakati
wa hafla fupi ya kukabidhi Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili kwa Maafisa
Habari wa Idara hiyo leo jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi huyo amenunua Kamusi
hizo ili kuwajengea uwezo maafisa hao kutumia maneno sahihi ya lugha ya
Kiswahili kama njia ya kuhamasisha matumizi sahihi ya lugha hiyo, kulia ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Sehemu ya Huduma za Habari na
Picha, Bw. Rodney Thadeus.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya hiyo, Sehemu ya Huduma za Habari na Picha, Bw. Rodney Thadeus wakionyesha nakala za Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili kwa Maafisa Habari wa Idara hiyo (hawapo pichani) mara baada ya makabidhiano ya Kamusi hizoyaliyofanyika katika Ofisi za Idara hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kamusi hizo zimekabidhiwa na Dkt. Abbasi kwa lengo la kuwajengea uwezo Maafisa hao katika matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Sehemu ya Huduma za Habari na Picha, Bw. Rodney Thadeus akiwasisitizia Maafisa Habari wa Idara ya Habari (Maelezo) kutumia Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili alizokabidhiwa na Mkurugenzi wa Idara ya hiyo Dkt. Hassan Abbasi leo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni njia ya kuhamasisha matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya hiyo, Sehemu ya Huduma za Habari na Picha, Bw. Rodney
Thadeus wakisoma nakala za Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili mbele ya
Maafisa Habari wa Idara hiyo (hawapo pichani) mara baada ya makabidhiano ya
Kamusi hizo yaliyofanyika katika Ofisi za Idara hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Kamusi hizo zimekabidhiwa na Dkt. Abbasi kwa lengo la kuwajengea uwezo Maafisa
hao katika matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Na Lilian Lundo - Maelezo
MKURUGENZI wa Idara
ya Habari (Maelezo) Dkt. Hassan Abbasi leo amekabidhi Kamusi Kuu ya Kiswahili
kwa watumishi wa Idara ya Habari (Maelezo) katika ofisi za Idara hiyo zilizopo
Jijini, Dar es Salaam.
Dkt. Abbasi amesema
mojawapo ya jukumu la idara hiyo ni kuhabarisha Umma, hivyo kamusi hiyo itakuwa
msaada mkubwa katika uandishi wa habari za kila siku.
“Kamusi hii ina
maneno mpaka yaliyoaanza kutumika hivi karibuni, kama vile bajaji. Pia ina
misamiati mingi ambayo haitumiki, hivyo kwa kuitumia kamusi hii kutaongeza
idadi ya misamiati ya Kiswahili kwa watumiaji wa lugha ya Kiswahili,” amesema
Dkt. Abbasi.
Ameitaka Idara ya
Habari kuitumia Kamusi hiyo kama nyenzo muhimu katika kutangaza lugha ya
Kiswahili ndani na nje ya nchi pamoja na kutumia misamiati mipya.
Hata hivyo, Dkt.
Abbasi alitoa ufafanuzi wa neno Mbashara kuwa ndio neno sahihi lenye maana ya inayorushwa
hewani moja kwa moja au kuonwa kwa wakati huohuo kupitia redio na televisheni
na sio Mubashara kama ambavyo limekuwa likitumika na vyombo vingi vya habari.
Aidha alitoa mfano wa
misamiati mingine iliyopo katika kamusi hiyo kuwa ni neno sharubati
linalomaanisha kinywaji laini ambacho hutengenezwa kwa maji ya matunda au
sukari na kisha kutiwa rangi. Neno lingine ni mnyange ambalo linamaana ya mtu
mwenye mwonekano mzuri, maridadi, mtanashati, mrembo, mlimbwende.
Dkt. Abbas amewataka
watumishi wa idara hiyo kuwa chemchem ya kutumia misamiati iliyoko katika
kamusi hiyo ili kukuza lugha ya Kiswahili.
Kamusi Kuu ya
Kiswahili ilizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim
Majaliwa Juni 19, mwaka huu, Bungeni Mjini Dodoma.






No comments:
Post a Comment