Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akiangalia moja ya vifaa vilivyoko kwenye chumba cha kuendeshea kivuko katika kivuko cha MV. Kazi kinachojengwa jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho, kitakabidhiwa tarehe 15, mwezi huu. Wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), Dkt. Musa Mgwatu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akifafanua jambo kwa Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha MV Kazi ambacho kinatengenezwa jijini Dar es salaam na Kampuni ya Songoro Marine Transport.
Mafundi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, wakiendelea na kazi ya kufunga mashine katika Kivuko cha MV Kazi. Kivuko hicho, kitakamilika na kukabidhiwa wiki ijayo na kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.
Kivuko
cha MV. Kazi kikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake. Kivuko hicho, kitakamilika na kukabidhiwa tarehe
15, mwezi huu na kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.
WAZIRI wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Wakala wa
Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kushiriki kikamilifu shughuli za matengenezo ya
vivuko ili kupata ujuzi wa ufungaji wa mifumo kutoka Kampuni zinazotengeneza
vivuko vya Serikali.
Akizungumza na
waandishi wa habari mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuvko kipya
cha MV Kazi, Bandarini jijini Dar es Salaam, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa kupitia mafunzo hayo Serikali itaweza kuokoa fedha nyingi ambazo kwa sasa inatumia
kulipa kampuni binafsi zinazojenga na
kukarabati vivuko.
“Hakikisheni mnapata
ujuzi kama walionao hawa, hatutaki kutumia fedha za Serikali kwa ajili ya
kukarabati au kutengeneza vivuko wakati nyinyi TEMESA mpo”, amesema Waziri
Prof. Mbarawa
Pamoja na ujenzi wa
kivuko hicho Waziri Mbarawa amewataka Temesa kuhakikisha wanasimamia na
kukitunza kivuko hicho ili kiweze kudumu kwa muda mrefu.
Aidha, Profesa Mbarawa
ameuagiza Wakala huo kuhakikisha wanakamilisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa
njia ya kielektroniki ili ili kudhibiti mianya ya rushwa.
Kuhusu huduma za
kivuko mkoani Lindi Serikali imesema itahakikisha inapelekea huduma haraka
iwezekanavyo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa mkoa huo.
Kwa upande wake
Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Dkt. Musa Mgwatu, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya
Songoro Marine Transport kuhakikisha
anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kivuko hicho kwa muda uliopangwa.
Dkt. Mgwatu amefafanua
kuwa kukamilika kwa kivuko hicho kutarahisisha usafiri kwa wakazi wa Kigamboni
na maeneo mengine ya jiji la Dar es salaam ambao wamekuwa wakitumia huduma hiyo
katka shughuli zao za kila siku.
Nae, Meneja Mradi wa
Kampuni ya Songoro Marine Transport, Bw. Major Songoro amemhakikishia Waziri
Mbarawa kumaliza kivuko hicho kwa wakati ambapo amesema ifikapo tarehe 15 mwezi
huu kivuko hicho kitakabidhiwa kwa Serikali.
Bw. Songoro amefafanua
kuwa kwa sasa mafundi wanamalizia kazi ndogo ndogo zilizobaki ikiwa ni pamoja
na kumalizia ufungaji wa injini.
Kivuko kipya cha MV
Kazi kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni Saba na kina uwezo wa kubeba abiria
800 na magari 22 kwa wakati mmoja.
(Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano)
No comments:
Post a Comment