Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wadau
waliohudhuria mkutano wa siku mbili wa Usalama barabarani katika ukumbi wa Mwl.
Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB) Bw. Joseph Haule akitoa taarifa ya udhibiti wa ajali za barabarani kwenye mkutano wa wadau wa usalama barabarani uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akiongea na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano wa Namibia Mhe. Sankwasa James Sankwasa wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akizungumza na
Mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa kinachoshughulika na masuala ya barabara Dkt. Kiran Kapila wakati wa mkutano wa siku
mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wanafunzi aliyeshinda tuzo ya uchoraji wa picha ya usalama barabarani Veronica Shirima akitoa maelezo kwa wadau wa usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Usalama barabarani mara baada ya kufungua mkutano huo, Jijini Dar es Salaam.
WAZIRI wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa usafirishaji
kuweka mikakati dhabiti ya kupunguza ajali za barabarani nchini ili kuokoa maisha
ya watanzania wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na ajali hizo.
Waziri Mbarawa ametoa
agizo hilo alipofungua mkutano maalumu wa kanda wa kujadili na kutathmini
changamoto za usalama barabarani na jinsi ya kuzikabili unaofanyika jijini Dar
es salaam.
Profesa Mbarawa
amesema kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikikatisha maisha ya watanzania
wengi kila mwaka ambao wengi wao ni vijana na nguvu kazi ya taifa hivyo ni
jukumu la wadau kubadilisha hali ya usalama barabarani.
“Kama tukijifunza
vizuri na kuyafanyia kazi mafunzo haya tunaweza kubadili hali ya usalama
barabarani kwani inaumiza kuona vifo vya watu wengi vinavyotokana na ajali za
barabarani hivyo ni wakati wa Jeshi la Polisi, na Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini
SUMATRA kushirikiana kukomesha ajali hizi”. Amesisitiza Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa
Serikali itatoa kipaumbele kwa yale yatakayojadiliwa na kuamuliwa katika
mkutano huo ili kuongeza kasi ya udhibiti wa ajali za barabarani hapa nchini na
kupunguza idadi ya ajali zinazoepukika.
Naye Mwenyekiti wa
Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule amesema kuwa Bodi hiyo inashirikiana
na taasisi nyingine katika kuhakikisha ubora wa miundombinu ya barabara inakuwa
salama na kupitika wakati wote.
Kwa upande wake
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani hapa nchini Mohamed Mpinga amesema
kikosi cha usalama barabarani kitaendelea kuhakikisha kuwa ajali za barabara
zinadhibitiwa.
“Suala la ajali za
barabarani ni jukumu letu sote kwa pamoja hivyo tukiungana kwa pamoja na
kushirikiana tutaweza kupunguza ajali hizi kwa kiwango kikubwa”. Amesema Kamanda Mpinga.
Mkutano huo wa siku
mbili ulioanza leo jijini Dar es salaam umewakutanisha wadaau mbalimbali wa
kimataifa wa masuala ya ujenzi na usimamizi wa usalama wa watu na mali wawapo
barabarani.
(Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)
No comments:
Post a Comment