Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo
Jovina Bujulu-
Maelezo
SERIKALIimewataka
wachapishaji wote nchini waliojiandikisha kwa Msajili wa Makampuni ( BRELA) na
Mamlaka ya Mapato (TRA), kufika katika
ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili wajiorodheshe na watambuliwe na Serikali na wananchi kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mpiga
Chapa Mkuu wa Serikali ndugu Cassian Chibogoyo alipokuwa akizungumzia kuwepo
kwa wimbi kubwa la wachapishaji hewa nchini.
Chibogoyo amesema
kuwa hatua hiyo inafuatia uwepo wa utitiri wa wachapishaji ambao hawatambuliki
na Serikali, kwa sababu baada ya kujiandikisha kwa mamlaka husika kama kampuni,
utawakuta wana mitambo ya uchapishaji ambayo mara nyingi wanaitumia kuchapisha
nyaraka bandia za Serikali bila kuwa na kibali kutoka katika mamlaka yenye
dhamana ya uchapishaji.
“Kwa sasa tumeanzisha utaratibu maalum wa
kuwatambua wachapishaji ambapo wanatakiwa kujiorodhesha kwa Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali, hii ni kutokana na kuwepo kwa uchapaji holela na bandia wa nyaraka za
Serikali” alisema Chibogoyo.
Aliongeza kuwa chini
ya utaratibu uliowekwa sasa wachapishaji wanatakiwa kuwasilisha nyaraka halali
za kampuni, shughuli wanazofanya, historia ya kampuni na mahali kampuni
inapofanyia kazi zake.
Adha, Chibogoyo
alisema kuwa faida za wachapishaji kujiandikisha ni pamoja na kutambuliwa
kisheria na Serikali ili hata wanaposhutumiwa waweze kulindwa na Serikali,
kukumbushana majukumu yao , wigo wao wa kazi, na pia wataelimishwa kuhusu
nyaraka wanazopashwa kuchapisha maana si kila nyaraka wanapashwa kuzichapisha.
Zaidi ya hayo, Chibogoyo
alitaja madhara ya kuchapisha nyaraka bandia kuwa ni pamoja na kuikosesha Serikali
mapato kutokana na uchapishaji wa stakabadhi mbalimbali bandia, uvamizi wa
mawasiliano ya Serikali uchapishaji wa vyeti vya usajili wa makampuni, na
uchapishaji bandia wa vyeti vya elimu ambavyo hupelekea mtu kuajiriwa kwa kazi
ambayo hana ujuzi nayo.
Akizungumzia hatua
ambao zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wachapishaji wa nyaraka bandia, Chibogoyo alisema
kuwa ni pamoja na kutaifisha mitambo ya wahusika.
Akizungumza suala
hilo hivi karibuni katika kipindi cha “Tujikumbushe”, Chibogoyo alisema kuwa
makosa ya uhalifu wa nyaraka bandia yanaangukia katika sheria za ushahidi,
sheria ya makosa ya jinai, sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970, pamoja na
sheria ya nembo na alama za Taifa.
Mpiga Chapa huyo Mkuu
wa Serikali alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kupambana na vita
hii kwa kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi ili kutokomeza janga
hilo.
“Tunawaomba wananchi
tuwe na mshikamano katika kufichua janga hili la uchapishaji holela na bandia
kwani ni janga la kitaifa, linagusa maslahi ya nchi na wananchi, nalifananisha
na ujambazi wa hali ya juu” alisisitiza Chibogoyo.
Baadhi ya nyaraka
ambazo zimekuwa zikighushiwa mara kwa mara ni pamoja na vyeti vya elimu katika
ngazi mbalimbali, risiti za serikali, vyeti vya kuzaliwa na ndoa, kadi za
magari na pikipiki, mihuri na nembo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment