TANGAZO


Wednesday, March 1, 2017

TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA YAJIDHATITI KUWAWEZESHA WASICHANA KIELIMU

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Tanzania Dkt. Fidelice Mafuniko akisisitiza jambo kabla ya kusainiana hati za makubaliano kati ya Taasisi hiyo na Shirika lisilo la Kiserikali la Marafiki wa Watoto wanaoishi na ugonjwa wa Saratani ili kuimarisha uhusiano utakaosaidia kuwapa fursa ya elimu watoto waliopo hosipitalini wakisumbuliwa na ugonjwa huo ili kuwapa haki sawa na wale walio katika mfumo rasmi.kulia ni Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. Walter Miya.(Picha zote na Frank Mvungi Maelezo)
Mkurugenzi wa shirika Shirika lisilo la Kiserikali la Marafiki wa Watoto wanaoishi na ugonjwa wa Saratani Bw. Walter Miya (kulia) akizungumza kuhusu umuhimu na Faida za Shirika hilo kushirikiana na Taasisi hiyo katika kuwawezesha kielimu watoto wanaougua ugonjwa wa Saratani. 
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Tanzania Dkt. Fidelice Mafuniko (kulia) na Meneja  wa mradi wa Elimu toka Asasi ya Kimataifa ya BRAC Maendeleo Tanzania Bw.Abdullah Mahtab wakisaini hati za makubaliano ya ushirikiano utakaowezesha  wasichana waliokosa fursa hiyo katika mfumo rasmi kupata elimu kupitia mradi huo. 
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Tanzania Dkt. Fidelice Mafuniko (kulia) na Meneja  wa mradi wa Elimu toka Asasi ya Kimataifa ya BRAC Tanzania Bw. Abdullah Mahtab wakibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano. 
Mkurugenzi wa Asasi ya Marafiki wa watoto wanaoishi na saratani Bw. Walter Miya (kulia) akibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya watu wazima Dkt. Fidelice Mafuniko.

Na Frank Mvungi-Maelezo
TAASISI ya Elimu ya Watu Wazima imejidhatiti kuwawezesha wasichana waliokosa Elimu ya Sekondari katika mfumo rasmi kutokana na kupata Mimba na Umasikini ili waweze kushiriki katika ujenzi wa Taifa kwa kuwajengea mazingira ya kupata elimu nje ya mfumo rasmi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Fidelice Mafuniko wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano baina ya Taasisi hiyo na Asasi ya Kimataifa ya BRAC Maendeleo Tanzania pamoja na Marafiki wa Watoto wanaougua Saratani.

Akizungumzia Makubaliano hayo Dkt. Mafuniko amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya majaribio ya mradi wa kuwawezesha wasichana yalikuwa ya miaka 2 kuanzia June 2014 hadi Machi 2016 ambapo mradi ulitekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Singida,Shinyanga,Mwanza,Tabora na Tanga.

Katika mradi huo jumla ya wasichana 1,950 wamenufaika na mpango huo kwa kupata elimu ya Sekondari  kwa njia ya ujifunzaji huria na masafa katika hatua ya kwanza nakuongeza kuwa awamu ya pili itahusisha walengwa 300 kutoka Mkoa wa Tanga ambao tayari wameshasajiliwa.

Awamu ya Tatu inaanza kuteklezwa kuanzia sasa kwa kipindi cha Miaka 3 na itahusisha wasichana takribani 2000 kutoka katika Mikoa ya Dar es Salaam,Singida,Shinyanga,Mwanza,Tabora na Tanga.

Mradi huu unatarajia kupanuka zaidi na kuwafikia walengwa wengi zaidi katika mikoa ya Pembezoni ikiwemo Kigoma,Rukwa na Ruvuma.

Kwa upande wake Meneja wa Elimu kwa Umma kutoka Asasi ya Maendeleo ya BRAC Tanzania Bw. Abdullaah Mahtab Khan amepongeza mpango huo na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Taasisi hiyo na Asasi yake na kutaka uendelezwe kwa manufaa ya Watanzania.

 Naye Mkurugenzi wa Asasi ya Marafiki wa Watoto wanaougua Saratani Bw. Walter Miya amesema kuwa asasi yao inatekeleza mradi wa kuwawezesha watoto wanaougua Saratani kielimu ambapo hospitali 16 zinatumika.

Alitoa mfano kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo wanafanya kazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

“Asasi yetu imejipanga kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuwawezesha watoto wenye saratani kupata Elimu kwani huu ni wajibu wetu sote kama Watanzania” Alisisitiza Miya.


Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ilianzishwa mwaka 1960,Pamoja na majukumu mengine ina jukumu la kuratibu na kutoa Elimu ya Sekondari kwa Vijana na Watu Wazima walio nje ya Shule wenye uhitaji na waliokosa elimu hiyo.

No comments:

Post a Comment